Afrika Kusini. Baada ya miezi 10 ya juhudi za ufuatiliaji, hatimaye mtoto wa Kitanzania, Juma, maarufu Joel, mwenye umri wa miaka 13 aliyekuwa akiishi kwenye kituo cha watoto yatima huko Johannesburg, Afrika Kusini, atarejeshwa nchini kuungana na baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Aprili 7, 2025 na Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, juhudi za kuwatafuta wazazi wa mtoto huyo zilianza Juni 8, 2024 baada ya mamlaka za Afrika Kusini kuomba msaada wa kidiplomasia kutokana na kifo cha bibi aliyekuwa akimlea Juma na ndugu zake kutofahamika.
“Mtoto huyo alifikishwa kwenye kituo cha watoto yatima baada ya kufiwa na mlezi wake na hakuna taarifa za familia zilizokuwa zinapatikana kwa wakati huo,” amesema Balozi wa Tanzania nchini humo, James Bwana.

Mtoto Juma akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana
Kupitia juhudi za ubalozi, kijana mmoja Mtanzania aliyejitambulisha kwa jina la Brayan alijitokeza na kudai kuwa ndiye baba mzazi wa mtoto huyo.
Februari, 2 mwaka huu, Bryan alisafirishwa hadi Afrika Kusini kwa usaidizi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kufanyiwa vipimo vya vinasaba (DNA) na kuthibitisha uhusiano na mtoto huyo.
Majibu ya vipimo hivyo, yaliyowasili rasmi ubalozini leo Alhamisi Aprili 7, 2025 yameonyesha kwa asilimia 99.99 kuwa Bryan ni baba mzazi wa Juma.
Balozi Bwana ameongeza: “Tuna furaha kubwa kutimiza wajibu wetu wa kusimamia masilahi ya Taifa letu na raia wetu walioko nje ya nchi. Tumeanza hatua za mwisho za kuratibu safari ya mtoto kurejea nyumbani kuungana na familia yake,”
Kwa mujibu wake, ubalozi sasa unaendelea kufuatilia taratibu za kupata kibali cha mahakama ya Afrika Kusini iliyoruhusu kufanyika kwa vipimo vya DNA, pamoja na kumwandalia mtoto hati ya dharura ya kusafiria (ETD) kabla ya safari ya kurejea Tanzania.

Mtoto Juma akiwa na baba yake
Jitihada za kuwakutanisha zilikuwa hivi…
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini uliombwa na mamlaka za Afrika Kusni usaidie kuwapata ndugu au wazazi wa mtoto huyo, kwa mujibu wa kituo cha kulelea watoto kilichopo Johannesburg Afrika Kusini.
Mtoto huyo alipelekwa Afrika kusini akitokea Tanzania akiwa na umri wa miaka 6 aliyempeleka alifariki hivyo kulelewa katika vituo mbalimbali vya malezi ya watoto, huku pakiwa hakuna taarifa za ziada wala nyaraka kumuhusu au taarifa zaidi kuhusu wazazi wake.
Ubalozi uliombwa ujaribu kuwapata ndugu zake ili iwapo watamtambua na kuthibitishwa unasaba naye aweze kurejeshwa.
Kwa wakati huo mtoto Juma/Joel hakuwa na taarifa zaidi kuhusu wazazi wake zaidi ya jina moja tu la mama yake Mariam na Baba yake Brayan.
Katika hatua nyingine ubalozi umetoa shukurani kwa wadau wote waliosaidia katika mchakato huo na kumtakia mtoto huyo maisha mema na yenye furaha zaidi akiwa na familia yake halisi.