Lindi. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameagiza kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa wataalamu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), waliokwamisha kwa uzembe urejeshaji wa mawasiliano katika barabara kuu ya Dar es Salaam–Lindi, eneo la Somanga Mtama mkoani Lindi.
Akizungumza baada ya kukagua kazi za urejeshaji wa mawasiliano yaliyokatika tangu Aprili 6, 2025, Waziri Ulega amesema hajaridhishwa na kasi ya ukarabati unaoendelea kwenye eneo hilo na kuwataka wataalamu kutoondoka eneo hilo hadi mawasiliano yatakaporejea kikamilifu.
“Nimekagua na kuona namna kazi inavyoendelea, nimebaini hapa kuna uzembe, na tutachukua hatua ili siku nyingine dharura kama hizi zichukuliwe kwa umakini mkubwa,” amesema Ulega.
Waziri huyo pia ametoa salamu za pole kwa wananchi wa mikoa ya kusini na Dar es Salaam waliokumbwa na adha hiyo, akiwahakikishia kuwa Serikali iko kazini na mawasiliano yatarejea haraka.
Pia, ameipongeza Tanroads Mkoa wa Lindi kwa hatua za haraka walizochukua baada ya tukio hilo kutokea, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza idadi ya malori ya kubeba mawe kufikia 100 ili kuharakisha ukarabati wa barabara hiyo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Mrakibu Msaidizi Joseph Mwasabeja, amesema kuwa hadi sasa hakuna maafa, huku akiwataka wananchi kuacha kwa muda kwenda shambani hasa kipindi hiki ambacho mvua bado zinaendelea.

“Niwaombe wananchi kwa sasa wasiende shambani ili kuepuka madhara ya kusombwa na maji. Wavumulie hadi mvua zikatike,” amesema Mwasabeja.
Mfanyabiashara wa samaki katika eneo la Nangurukuru, Husna Chilumba, ameiomba Serikali kujitahidi kurudisha mawasiliano kwenye eneo hilo, kwani biashara zao za samaki haziwezi kuendelea kwa kukosa wateja.

“Sisi tunategemea wasafiri wa mikoani kununua samaki, kwa sasa tumeathirika sana kutokana na kukosa wateja. Tunaiomba Serikali ijitahidi kurejesha mawasiliano kwa wakati ili tuendelee na biashara,” amesema Chilumba.