Chaumma yashauri marekebisho Tume ya Uchaguzi

Mbeya. Pamoja na kuthibitisha kushiriki uchaguzi mkuu wa 2025, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimependekeza na kuishauri Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) baadhi ya mambo ya kufanyiwa marekebisho kabla ya shughuli hiyo.

Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Oktoba 25, 2025 kuwapata madiwani, wabunge na Rais huku chama hicho kikitarajia kusimamisha wagombea katika nafasi zote.

Akizungumza leo Aprili 7, 2025 na waandishi wa habari jijini hapa, Katibu Mwenezi wa Chaumma Taifa, Ipyana Njiku amesema katika kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho cha Februari 19, 2025 kiliazimia kushiriki uchaguzi huo katika nafasi zote na kutoa mwelekeo wa nchi kwa miaka mitano ijayo.

Amesema pamoja na uamuzi huo, wamependekeza na kuishauri INEC kufanya mabadiliko kwa wasimamizi wa uchaguzi badala ya makamishna na wakurugenzi.

 “Wakurugenzi wasiwe wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo kwa kuwa, hao ni makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), wasimamizi wa uchaguzi kwenye vituo wasipangwe watumishi wa Umma na mawakala wa vyama wasipewe usumbufu kama ambavyo imejitokeza huko nyuma,” amesema Njiku.

Katibu huyo amewaomba wananchi kujiandaa na kushiriki vema uchaguzi huo huku akiwaomba vijana wenye sifa kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi huo.

Amefafanua kuwa, Chaumma haishirikiani wala kufungamana na chama chochote cha siasa huku akieleza kuwa, hawaelekezwi au kuagizwa na mtu yeyote kufanya uamuzi kwani ni chama chenye katiba na usajili wake binafsi.

“Kumekuwa na mnong’ono kwamba tunashirikiana na chama fulani na ni mawakala, huu ni uongo na uzushi, sisi tunafanya kulingana na katiba yetu kwa kuwa usajili unatambulika kwa msajili,” amesema katibu huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Mbeya.

Amesema iwapo chama hicho kitashinda dola, hoja yao ni kutoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi chuo na sera ya “ubwabwa” itakuwa katika meneo yote ikiwamo hospitalini.

 Mwenyekiti wa vijana wa chama hicho mkoani Mbeya, Lusako Mwakilumwa amewaomba vijana, makada wa vyama vya siasa na wananchi wanaohitaji nafasi za uongozi kujiunga na chama hicho ili kukipa nguvu kuelekea uchaguzi mkuu.

“Wapo makada wa vyama vya upinzani ambao wanateseka kwenye vyama vyao wakihitaji nafasi za uongozi, niwaombe kuanzia vijana wenzangu na wananchi kwa jumla, waje kutimiza ndoto zao huku katika uchaguzi mkuu,” amesema Mwakilumwa.

Mchambuzi na mlezi wa vyama vya siasa mkoani Mbeya, Chifu Prince Mwaihojo ameviomba vyama vyote vya siasa nchini kushiriki uchaguzi mkuu kwa masilahi ya nchi akieleza kuwa, misimamo ya chama chochote kutoshiriki kinaweza kupotea.

“Chama kimoja hakiwezi kuzuia uchaguzi, fujo za kwenye siasa zipo duniani kote, kikubwa ni kila mmoja kujipanga kulinda kura zake, sisi machifu tunajivunia watu tulionao,” amesema Mwaihojo.

Related Posts