******
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetaka Hotuba za Bajeti mwaka huu zichambue sababu za kutofanikisha malengo ya Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa Jana Aprili 6, 2025 na Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba Wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juu ya mtazamo wa CUF kuhusu Bajeti ya Mwisho ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22 hadi 2025/26.
Prof. Lipumba amebainisha kuwa utaratibu wa zamani wa hotuba za Bunge la Bajeti ulianza na hotuba za Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha kueleza hali ya uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo na mapendekezo ya mapato na matumizi.
“Hivi sasa Hotuba hizi ni za mwisho katika Bunge la Bajeti. Anayefungua dimba ni Waziri Mkuu ambaye anaeleza utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa ujumla. Ili kuwatendea haki Watanzania Hotuba ya Waziri mkuu ianze kutoa ufafanuzi wa kwa nini Malengo ya Mpango wa tatu wa Maendeleo hayatafikiwa,” amesema Prof. Lipumba na kuongeza,
“Mawaziri wa Sekta pia wajikite katika kuwaeleza Watanzania kushindwa kwa Serikali kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo katika sekta zao,”.
Awali Prof. Lipumba alieleza kuwa kikao cha Bunge la Bajeti kinatarajiwa kuanza Aprili 8, 2025 na kwamba hii itakuwa Bajeti ya mwisho ya utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo 2021/22 – 2025/26 na mwaka wa mwisho wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Hata hivyo alisema bajeti za Serikali hazijajikita katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.
Alieleza kwamba katika Hotuba za bajeti Waziri mara kwa mara hueleza “Bajeti ya Serikali imeandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030; pamoja na nyaraka, miongozo na makubaliano mengine ya kikanda na kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.”
Hivyo alieleza kuwa Bajeti inayozingatia mlolongo wa nyaraka nyingi ni wazi haiongozwi na Mpango wa Maendeleo.
Alibainisha kuwa Machi 11, 2025, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, aliwasilisha Bungeni mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2025/26.