Dar es Salaam. Baada ya dereva Mtanzania, Juma Maganga (45) kufikishwa mahakamani nchini Sudan Kusini Aprili 3, 2025 kwa shitaka la kuua bila kukusudia katika ajali, amesema hakuna alichoelewa kutokana na lugha iliyotumika; na hakuwa na mwakilishi.
Akiwa amefikisha siku 52 leo Aprili 7, 2025 akishikiliwa na Jeshi la Polisi nchini humo tangu Februari 14, 2025 amesema anahisi kukata tamaa, akijiona ataendelea kuishi katika Taifa hilo.
Maganga ambaye kwa sasa yuko Sudan Kusini na mwanaye anayemsaidia, anatakiwa kulipa fidia ya Sh938.7 milioni.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Aprili 7, Maganga amesema anahisi kukata tamaa kwani sheria za nchi hiyo mtu anapoua bila kukusudia hutakiwa kulipa fidia ya mifugo ambayo hubadilishwa kwa thamani ya fedha.
Familia ya marehemu katika ajali hiyo inadai fidia ya Pauni ya Sudan milioni 213.06 (sawa na Sh938.71 milioni) ambazo zinajumuisha gharama zilizotumika katika msiba.
“Hela yenyewe iliyotajwa ni kubwa ukilinganisha na hali yangu ilivyo, nahisi kama sina msaada wowote ninaoweza kuupata, najisikia uchungu sana. Hata, nikizungumza na watu kama wewe (mwandishi) naona kama najielezea ila hakuna msaada wowote ninaopata,” amesema Maganga.
Amesema anaishi maisha magumu akiwa rumande, huku akitegemea michango kutoka kwa baadhi ya madereva wenzake walioko Tanzania ili kupata chakula cha asubuhi na mchana.
“Bila michango hii unaweza kufa kwa njaa, mahabusu za huku si kama za Tanzania ambazo mnapikiwa chakula, huku unajitafutia mwenyewe, ndiyo maana hata simu unapewa kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa alasiri ili uwasiliane na watu uweze kupata chochote kitu,” amesema.
Amesema mtoto wake aliye Sudan Kusini amepata dada ambaye amekuwa akimpatia fedha kidogo, hivyo huwapikia chakula kila siku.
“Sijui nikitoka nitamlipa nini, wema alionitendea ni mkubwa ambao siwezi kuuelezea,” amesema.
Maganga amesema licha ya kutibiwa majeraha aliyopata baada ya kushambuliwa na wananchi baada ya ajali kutokea, bado amekuwa akipitia maumivu makali ndani ya makovu hasa joto linapokuwa kali.
“Ninachoomba nisaidiwe, kama ni Serikali au wananchi wenye uwezo, nimekuwa kama nimepoteza mwelekeo, sielewi kesho yangu katika nchi za watu nikiwa mwenyewe bila msaada,” amesema Maganga aliyepeleka mzigo wa mahindi nchini humo.
Amesema kwa sasa mahindi hayo yameshushwa na kupelekwa kwa wahusika, huku gari likiendelea kushikiliwa.
Alivyofikishwa mahakamani
Maganga aliyefikishwa mahakamani kwa ajili ya kesi yake kutajwa amesema mwanasheria aliyetarajiwa kumwakilisha hakutokea na shauri liliendeshwa kwa lugha ambayo hakuielewa.
“Lakini wao wanataka walipwe hela, Serikali ingekuwa na uwezo ingeongea na ndugu wa marehemu ili niweze kuachiwa kwa sababu huku ukilipa hela unaachiwa hata kama ulikuwa umehukumiwa miaka mitano ukakaa miwili ukilipa hela unatoka, vinginevyo naweza kuishia huku milele,” amesema.
Mmiliki wa gari hilo, Gabriel Kiliki amesema baada ya kesi kuahirishwa walimtafuta wakili aliyekuwa amekubali kumwakilisha dereva wake, lakini hawakumpata.
“Simu yake haikupatikana kabisa hadi leo, sijui shida gani imetokea,” amesema Kiliki.
Amesema dereva wake hakuelewa chochote kilichozungumzwa mahakamani kwani mazungumzo yalifanyika kwa lugha inayofanana na Kiarabu.
Kiliki amesema anaangalia namna nyingine ya kupata wakili atakayesimamia kesi hiyo.
Amesema kuna aliyempata hata hivyo, alimwambia ni ngumu yeye kufika katika eneo ambalo dereva huyo anashikiliwa kutokana na hali ya usalama ilivyo barabarani.
“Alinishauri nitafute mwingine eneo lile, nafanya kila linalowezekana kupata mwingine kabla ya tarehe ya Mahakama (Aprili 11, 2025) ili aweze kusimama na dereva wakati kesi itakapotajwa,” amesema Kiliki.
Kiliki amesema wakili ambaye awali alikubali kumwakilisha dereva huyo alitaka alipwe Dola za Marekani 1,000 (Sh2.6 milioni).
Kwa mujibu wa Kiliki, Mahakama aliyofikishwa ni ya kimila na alielezwa na wakili huyo kuwa kwa kawaida adhabu huwa fidia ya ng’ombe 31 kwa mtu aliyeua bila kukusudia ambayo inakadiriwa kuwa sawa na Dola za Marekani 27,000 (sawa na zaidi ya Sh71.5 milioni).
“Mmoja wa maofisa wa ubalozi nchini Uganda alinipigia simu siku chache nyuma kabla hajafikishwa mahakamani, nikamueleza hali ilivyo na akaahidi kuwa wanafuatilia, nipo nasubiri pia mrejesho kutoka kwao ili niweze kujua kinachoendelea kwa sababu nilimuunganisha na mtoto wa dereva huyu ambaye naye yuko huko Sudan,” amesema Kiliki.
Rehema Mongi, mke wa Maganga kwa sasa ndiye anayebeba mzigo wa kuhudumia familia ya watoto wanne ambapo kati yao, watatu ni wadogo wakiwa shuleni na mwingine ni mchanga.
Mtoto aliye Sudan naye ameacha mke na mtoto mchanga wa miezi sita aliye nyumbani kwa Maganga.