Arusha. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanza mchakato wa kuanzisha Kituo cha Onyo la Mapema, kitakachofanya kazi ya kulinda amani na utulivu katika nchi zote wanachama na kuzuia mauaji ya halaiki.
Hayo yamesemwa leo Aprili 7,2025 jijini Arusha na Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, kwenye maadhimisho ya miaka 31 tangu kutokea kwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda mwaka 1994.
Mauaji hayo ya kimbari yalitokea Rwanda kuanzia Aprili hadi Julai 1994 zaidi ya watu milioni moja, hasa Watutsi na Wahutu wenye msimamo waliuawa kikatili na wanamgambo wa Kihutu.
Mauaji hayo yaliendeshwa na chuki za kikabila zilizokuwa zimejengeka kwa muda mrefu, na hadi leo Rwanda inaendelea kujenga mshikamano wa kitaifa kupitia maridhiano na haki.
Nduva amesema kituo hicho ni sehemu ya juhudi za EAC kuhakikisha hatua madhubuti zinachukuliwa ili kuzuia mauaji ya kimbari katika siku zijazo katika nchi zote za EAC za sasa na zijazo.

“Hii ni sehemu ya sera ya EAC inayolenga kuzuia mauaji ya kimbari,” amesema.
“Lengo letu ni kuhakikisha hatujirudii tena katika majanga kama haya. Tunatanguliza mikakati ya kuzuia na sera imara ili kituo hiki kiweze kuanza kazi.”
Nduva amezionya nchi wanachama dhidi ya kupanda mbegu za chuki au kukuza migawanyiko ya kikabila au kijamii, akisema tabia hizo zinaweza kuchochea umwagaji damu au mauaji ya halaiki.
Aidha, amevitaka vyombo vya habari katika ukanda huu kuwa makini na maudhui wanayochapisha au kutangaza, kwa kuhakikisha yanachangia kujenga amani, usalama na mshikamano wa kitaifa na kikanda.
“Taifa lolote la EAC linapaswa kuwa makini dhidi ya aina yoyote ya uchochezi unaogawa watu kwa misingi ya kabila, siasa, dini au mengineyo. Tumeona jinsi vyombo vya habari vilivyotumiwa Rwanda kueneza kampeni za chuki, hali hiyo isijirudie kamwe, vyombo vya habari vina jukumu la kueneza ujumbe wa amani na utulivu,” amesema Nduva.
Amesema EAC tayari imeweka mnara wa kumbukumbu wa mauaji ya kimbari na huadhimisha Aprili 7 kila mwaka ili kujifunza na kukumbushana umuhimu wa kulinda amani na kuchukua tahadhari dhidi ya viashiria vya mgogoro.
Rosemary Haule, mwakilishi wa vijana wa Tanzania katika jumuiya hiyo, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuwajumuisha vijana katika shughuli zote za maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“Kwa mfano, Tanzania mwaka huu tuna uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais. Ni lazima vijana nao wahusishwe katika kila hatua ya utekelezaji ili wawe na umiliki na kupunguza migogoro,” amesema Rosemary.
Amesisitiza kuwa, vijana wanapaswa kuwa mabalozi wa amani na utulivu ili kuhakikisha nchi inabaki salama kwa maendeleo ya vizazi vya sasa na vijavyo.