Katika tukio hilo lililofanyika mwishoni mwa wiki mjini Morogoro, mgeni rasmi alikuwa Mtetezi wa Haki za Wanawake na Wasichana, Georgia Mutagahywa, ambaye aliwasilisha hotuba yenye msukumo mkubwa kwa wahitimu, akiwahimiza kuthamini elimu, kuwa wavumilivu na kuamini katika ndoto zao.
“Hamkufika hapa kwa bahati mbaya. Mmefanya kazi. Hilo ndilo la muhimu,” alisema Mutagahywa huku akishangiliwa na umati wa walimu, wazazi na wanafunzi.
Katika hatua ya kuonyesha mshikamano na kuunga mkono elimu ya wasichana, Mutagahywa alitangaza msaada wa kompyuta 15 mpya kwa ajili ya kuimarisha chumba cha TEHAMA shuleni hapo, msaada uliotolewa na Kampuni ya Ujenzi ya Fuchs. Tangazo hilo lilizua shangwe na baadhi ya wanafunzi walishindwa kujizuia na kumwaga machozi ya furaha.
“Wakati Bi Georgia anatangaza msaada wa kompyuta, nililia. Ilionekana kama kuna mtu ametusikia,” alisema Kate Malindi, mwanafunzi wa Kidato cha Tano anayesomea mchepuo wa PMC na pia ni Kiranja Mkuu wa shule.
Kwa kutambua mchango wake mkubwa katika kuhamasisha elimu ya wasichana, shule hiyo ilimtunukia tuzo maalum Mutagahywa kama ishara ya shukrani kwa juhudi zake zisizo na kuchoka.
Aliwahamasisha wahitimu kupitia hadithi yake binafsi ya kupanda Mlima Kilimanjaro, safari aliyokutana nayo na vikwazo lakini hakukata tamaa hadi alipotimiza azma yake mwezi Desemba 2024 akiwa ameambatana na mwanawe wa miaka 18. “Utakutana na milima mingi maishani – lakini usiogope, tafuta msaada, simama tena na uendelee kupanda,” aliwahimiza wahitimu.
Katika mahafali hayo, Mkuu wa Shule Bi. Mary Lugina alitunukiwa tuzo ya heshima kwa uongozi wake wa kimaono ulioleta mafanikio kwa shule hiyo. Walimu pia walipongezwa kwa juhudi zao katika kuwalea wanafunzi kuwa viongozi wa kesho.
Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kilakala, iliyoanzishwa mwaka 1957, imeendelea kuwa kinara katika ubora wa kitaaluma na uzalishaji wa viongozi wanawake katika nyanja mbalimbali nchini na kimataifa.
Wakati wahitimu wakijiandaa kuendelea na safari ya elimu ya juu, ujumbe kutoka kwa mgeni rasmi ulikuwa wazi: mafanikio hayaji kwa urahisi, bali kwa uthabiti, mahusiano thabiti na uwajibikaji.
“Usiruhusu ulimwengu ukufafanue – ujifafanue,” alihitimisha Mutagahywa huku akinukuu maneno ya Maya Angelou na Chimamanda Ngozi, akihimiza wema, ukweli na kuweka mipaka kama misingi ya uongozi bora wa maisha.
Mgeni rasmi katika Mahafali ya 55 ya shule ya sekondari ya Wasichana ya Kilakala , Georgia Mutagahywa, akimkabidhi cheti mmoja wa mhitimu katika mahafali ya shule hiyo Mjiini Morogoro hivi karibuni.
Mgeni rasmi katika Mafahali ya 55 ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kilakala , Georgia Mutagahywa, akizungumza na wahitimu wa kidato cha sita wa shule hiyo mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki .
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas akizungumza kwenye mahafali ya 55 ya shule hiyo.