IMANI POTOFU ZINAVYO KWAMISHA KUFIKIWA USAWA WA KIJINSIA

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi maalumu Dkt. Dorothy Gwajima.

Kulia ni mwandishi wa Makala hii akifanya mahojiano kuhusu usawa wa kijinsia.

Kushoto ni mwandishi wa Makala hii akizungumza na Jeneroza Tunati.

…………………

Na Daniel Limbe,Chato

 “MAENDELEO hayawezekani bila mabadiliko ya kifikra, na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanayofikiri hawawezi kubadili kitu chochote,”

Hiyo ni kauli ya Mwanafalsafa wa Ireland George Benard Shaw aliyoitoa akionyesha umuhimu wa fikra za maendeleo duniani.

Kwa mujibu wa Shaw, mabadiliko yoyote katika jamii yanapaswa kuungwa mkono na serikali, taasisi mbalimbali, viongozi wa dini, jamii na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kuchochea usawa,haki, maendeleo na ustaarabu.

Mbali na mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi,elimu, sayansi na teknolojia nchini, bado zipo haki za msingi za kijamii ambazo zinakiukwa kwa kujua au kutojua kutokana na baadhi ya watu kuendekeza imani potofu na mfumo dume kwa kundi la wanawake na watoto.

Aidha ni muhimu ifahamike kuwa jukumu la kulinda na kusimamia haki zote za binadamu,usawa wa kijinsia ikiwemo haki za watoto ni la jamii nzima, pasipo kuliacha mikononi mwa vyombo vya dola pekee.

Hatua hiyo itasaidia jamii kuishi kwa amani,upendo na mshikamano pasipo kubaguana kwa jinsia,rangi kabila wala tofauti zetu za dini.

Licha ya ukweli huo, zipo baadhi ya jamii ambazo haziwathamini wanawake kwa kuamini kuwa hawana haki ya usawa ikilinganishwa na wanaume, jambo linalorudisha nyuma jitihada za wanawake kujikomboa kisiasa, kiuchumi, ki elimu na kiutamaduni.

Ifahamike kuwa kwa miongo kadhaa, wanawake walibaki nyuma kimaendeleo na kifikra kutokana na mila na tamaduni potofu zilizotumika kuaminisha umma kuwa mwanamke ni chombo cha starehe pekee na asiyeweza kuongoza, kufikiri wala kutenda kama mwanaume.

Hatua hiyo ni kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kwani inatamka kuwa binadamu wote ni sawa.

Kwa mujibu wa Ibara ya 12 (1) cha Katiba hiyo, “Binadamu wote huzalia huru,na wote ni sawa (2) Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake,”

Kwa msingi huo wa Katiba, kutowathamini na kutowapatia wanawake haki zao za msingi kwenye maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii ni kutweza utu wao sanjari na kukiuka sheria mama ya nchi ambayo ni Katiba.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, kuhusiana na watu wenye uwezo wa kufanya kazi Tanzania(ILFS) kwa mwaka 2021, ulibainisha kuwa sekta ya umma imeajiri jumla ya watu 529,557 ambapo wanaume ni 301,266 sawa na aslimia 56.9 huku wanawake wakiwa ni 228,291 sawa na asilimia 43.1 ikifuatiwa na sekta binafsi aslimia 72 ya wanaume na aslimia 28 ya wanawake.

Takwimu hizo zinaonyeaha wazi kuwa wanawake wengi wanajishughulisha na ajira nyingi zisizo rasmi na zenye ujira mdogo ikilinganishwa na wanaume.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa wanaume wana kipato kikubwa kwa mwezi cha wastani wa shilingi 396, 885 kuliko wanawake ambao wanapata kwa wastani wa shilingi 378, 469 katika aina zote za ajira ikihusisha kazi zenye ujira au ajira binafsi katika sekta ya kilimo.

Hata hivyo baada ya serikali kuanzisha Taasisi ya uongozi mwaka 2011 ambayo ililenga kutoa mafunzo kwa wanawake katika uongozi,ilisaidia baadhi ya wanawake kushiriki katika nafasi mbalimbali ambapo idadi ya Wabunge wanawake wa kuchaguliwa na kuteuliwa viti maalumu ilifikia 143 kati ya Wabunge wote, ikiwa ni na aslimia 37.4 kwa mwaka 2023 ikilinganishwa na aslimia 16 kwa mwaka 2000.

Aidha kwa mujibu wa taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) ya mwaka 2020, ushiriki wa wanawake katika nafasi za udiwani, wanawake 260 walichaguliwa kati ya madiwani 3,953 sawa na asilimia saba, huku wale wa viti maalumu wakiwa 1,374 sawa na asilimia 25 ya madiwani wote nchini.

Hiyo ni sawa na kusema kuwa jumla ya madiwani wote wanawake ni 1,634 kati ya madiwani 5,587 sawa na asilimia 29.

Waziri wa Maendeleo ya jamii, Jinsia na Makundi maalumu,Dk. Dorothy Gwajima,anasema mabadiliko chanya katika jamii yanakuja kwa kueleweshana pamoja na kuzingatiwa kwa sheria zilizopo.

Anasema Tanzania imeweka misingi kwenye Katiba ya nchi kuhusu ajenda ya maendeleo yenye usawa wa kijinsia na mahsusi uwezeshaji wa wanawake na wasichana kupitia sekta mbalimbali.

Akizungumzia mkutano wa kimataifa uliofanyika Machi 12, mwaka huu nchini Marekani na kuwahusisha wajumbe wa jumuiya za Umoja wa mataifa kwa lengo la kujadili nafasi ya mwanamke katika nchi zao ikiwa ni miaka 30 baada ya azimio la Beijing,Dk. Gwajima anasema Tanzania inaendelea kupiga hatua kubwa kwa kuboresha sera,mikakati na sheria zinazowagusa wanawake na wasichana.

Anazitaja sera zilizoleta mabadiliko ya ustawi kwa mwanamnke kuwa ni Sera za maendeleo ya Wanawake na Jinsia kwa Tanzania bara na Zanzibar, Sera ya Taifa ya Biashara inayohakikisha usawa wa kijinsia kwenye biashara, Sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo pamoja na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa inayotaka mamlaka hizo kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyokuwa na riba kwa Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu.

Dk Gwajima anasema uwepo wa Sheria ya Manunuzi ya Umma inayohakikisha asilimia 30 ya zabuni zinawanufaisha wanawake na Makundi maalumu, ambapo uamuzi huo huwapa fursa wanawake kupata tenda mbalimbali ambazo zinawasaidia kukuza kipato chao.

Mbali na hayo, anasema Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kutambua kosa la Ukatili wa Kijinsia katika Changuzi “Violence Against Women in Elections” kama kosa la Uchaguzi.

“Kupitia kifungu cha 135 kinatambua unyanyasaji wa Kijinsia ni kosa katika Uchaguzi,” anasema Dk. Gwajima.

*MAONI YA WADAU*

Ofisa Ustawi wa jamii wa hospitali ya wilaya ya Chato,Lucia Lusambo, anasema kitendo cha baadhi ya watu kuamini kuwa wanawake wenye vipato vikubwa na wenye ajira ndoa zao hutawaliwa na migogoro mingi,kuwa siyo kweli na kwamba huo ni mtazamo tu kwa sababu hakuna utafiti unaothibitisha hilo.

“Ukweli ni kwamba mume na mke wakiwa na vipato sawa inawasaidia kuimalisha ndoa yao na kusaidiana katika matunzo ya familia ikiwemo malezi bora,” anafafanua.

Lusambo anasema hatua hiyo itasaidia kupunguza wimbi la watoto wanaodhurura mitaani, kwa sababu watakuwa wamepata malezi kutoka kwa wazazi bora badala ya watoto kutelekezwa kutokana na migogoro ya kifamilia.

 Mfanyabiashara wa samaki na Mwendesha bodaboda Jeneroza Tunati, na mkazi wa Chato mkoani Geita anasema haikuwa rahisi kufikia uamuzi wa kufanya biashara hiyo ambayo awali iliaminika kuwa inafanywa na wanaume pekee.

Anasema aliifanya biashara hiyo baada ya kuamua kutosikiliza jamii inamtazama na kumjadili kwa namna gani, badala yake aliendelea kujituma huku baadhi ya watu wakimwona kama mwanamke asiye na heshima katika ndoa yake.

“Ninamshukuru sana Mungu kwa hatua hii ya kimaendeleo niliyo nayo,maana nimefanikiwa kujenga nyumba, ninasomesha watoto pasipo kumtegemea mume wangu,wanakula, wanavaa na ninawapatia mahitaji mengine muhimu ya kifamilia,”

Anafafanua kuwa tangu mwaka 2012 alipojiajiri na kazi hiyo licha ya kupata mafanikio lakini bado jamii yake ilikuwa inamshangaa kwa kumuona akiendesha pikipiki kwa umbali mrefu kwa ajili ya kuuza samaki kiasi kwamba wapo waliosema anafanya kazi hiyo kwa ajili ya kutafuta wanaume.

Anasema mtazamo hasi uliojengeka katika jamii wa kuwaona wanawake kuwa hawawezi kufanya kazi ngumu,zenye ubunifu, uongozi na uzalishaji mali unaendelea kuchochea ubaguzi na kudhoofisha malengo ya milenia ya kumkomboa mwanamke dhidi ya usawa wa kijinsia.

Christina Lemoi,anasema wanawake wanastahili kuheshimiwa na kupewa fursa sawa na wanaume na kwamba kuendelea kukumbatia Mila na Tamaduni zinazokandamiza usawa wa kijinsia ni kuchelewesha maendeleo ya nchi.

Akitoa mfano wa baadhi ya michezo kama ngumi za kulipwa, mpira wa miguu na riadha kuwa awali zilijulikana kuwa ni michezo ya wanaume pekee ukilinganisha na hali ilivyo sasa baada ya wanawake kuanza kupata fursa hizo.

“Ndiyo maana sasa siyo ajabu kuwakuta mafundi wanawake wakichanganya zege,kujenga nyumba, wakichimba Madini ya dhahabu, wamiliki wa maduka na hata viongozi wakubwa katika taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi,” anaeleza.

Anasema hatua zote hizo zinaonyesha ni jinsi gani wanawake wakipewa fursa wana uwezo mkubwa wa kufanya shughuli mbalimbali badala ya jamii kuendelea kuwaona viumbe dhaifu wanaohitaji kuhurumiwa na wanaume.

“Huu ni wakati wa wanawake kuzikimbilia fursa za maendeleo badala ya kusubiri kuletewa,” anasema Lemoi 

Chibuga Masato ambaye ni mkazi wa kijiji cha Mbuye,anasema ni muhimu kuwathamini wanawake kwa kuwapatia haki zao za msingi pasipo ubaguzi kwa kuwa ni watu wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kaya,jamii na ulimwengu kwa ujumla.

Anasema pamoja na kuwepo kwa usawa wa kijinsia bado jamii inapaswa kuendelea kuheshimu na kulinda mila na tamaduni njema ambazo zimeendelea kuimalisha umoja,upendo na mshikamano wa kitaifa.

“Yapo maadili yasiyofaa ambayo ni muhimu sana kuyaepuka ikiwemo suala la wanawake kusagana,kuvaa mavazi yanayo waacha utupu, kujiuza kwa lengo la kujipatia kipato, unyanyasaji kwa wanaume ikiwemo vipigo na vitendo vya mauaji,” anahitimisha Masato.

NINI KIFANYIKE

Wadau wa maendeleo Stella Emmanuel na Zacharia Kahema, wanashauri serikali, viongozi wa dini na taasisi mbalimbali kuendelea kutoa elimu kwa umma kutambua thamani ya usawa wa kijinsia kwa manufaa ya jamii.

“Viongozi wa dini watumie nyumba zao za Ibada kuhubiri usawa wa kijinsia na umuhimu wa kulinda ndoa na matunzo bora ya watoto wao,” anasema Stella na kuitaka serikali isimamie kwa uthabiti sheria zilizopo katika kutokomeza ukatili na usawa wa kijinsia.

Kahema anaitaka serikali itumie mikusanyiko ya mikutano kuelimisha umuhimu wa wanawake na wasichana kutumia fursa zilizopo kujiondolea umaskini wa vipato na elimu.

Aidha Kahema anavitaka vyama vya siasa nchini viweke kipaumbele kwa kila mgombea wa nafasi ya ubunge na udiwani kueleza mkakati wake katika suala la usawa wa kijinsia iwapo atachaguliwa kushika wadhifa huo.

          Mwisho.

Related Posts