Siku 75 za uongozi wa mwenyekiti mpya wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, na timu yake zimekuwa za moto kweli kweli kutokana na kusimamia bila kupepesa macho kauli mbiu ya ‘No Reforms No Election’ (Bila mabadiliko, hakuna uchaguzi).
Hakuna ubishi kuwa Lissu na wenzake wanatekeleza msimamo wa chama uliopitishwa katika vikao halali kuanzia Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu, lakini hakuna ubishi kuwa kwa namna ulivyo, hautekelezeki.
Siku zote nasema na leo narudia kuwa ukweli una sifa moja kuu kwamba hata ukiuchukia au kuukataa, haugeuki kuwa uongo. Kwa hiyo, ‘No Reforms No Election’ inaweza kuwa ilikuwa na dhamira njema, ila haieleweki na haitekelezeki.
Njia pekee ya kufanya tena kwa haraka, kwa Chadema kubadili gia angani na kurudi mezani na kuelimisha kwanza wanachama wake na viongozi kuelewa maana ya mkakati huo na kuushirikisha umma.
Hata kundi la wanachama la G55, ambao naamini baadhi yao walikuwepo wakati mkakati huo unatangazwa Desemba 12, 2024 na Freeman Mbowe, watakubaliana nami kuwa Lissu na wenzake wanasimamia msimamo wa chama.
Kinachobishaniwa sasa ni kwamba wakati Mbowe anatangaza msimamo huo wa chama, hakusema watazuia uchaguzi, bali wakati uchaguzi ukifika Oktoba 2025 na hakuna mabadiliko ya mifumo ya chaguzi, Chadema wangefanya maamuzi.
Katika kutekeleza huo mkakati, Mbowe alikuwa wazi kabisa kuwa wao Chadema wangekaa na wadau wengine kuweka agenda ya kitaifa, lakini akamaliza kwa kusisitiza ‘No Reforms, No Election’.
Nakubaliana na John Mrema wa G55 aliyekuwa mmoja wa waasisi wa ‘No Reforms No Election’ huko nchini Kenya mwaka 2020 kwamba, hata Mbowe hakusema watazuia uchaguzi, bali wangefanya maamuzi muda wa uchaguzi ukifika.
Ukimsikiliza vizuri Mrema, anasema mkakati huo ulikuwa unaambatana na shughuli mbalimbali, ikiwamo kushirikisha wadau wengine vikiwamo vyama vya siasa, nchi wahisani, mabalozi na umma katika kushinikiza mabadiliko hayo.
Mpaka sasa sioni chama chochote kingine cha upinzani kinachowaunga mkono Chadema na siwaoni Watanzania (kwa uzoefu) watakaojitokeza kuzuia uchaguzi huo ambao umebakiza miezi michache kufanyika. Watanzania wanafahamu jinsi ya kulia, lakini hawataki kudai haki, wanataka wapewe.
Rejeeni maandamano ya kupinga kupotea kwa watu, utekaji na mauaji kunakofanywa na watu wasiojulikana, ambalo limgusa kila jamii yetu hawakujitokeza, hili la kuzuia uchaguzi ambao upo kikatiba watajitokeza kweli?
Ninachokiona kinapewa nguvu kubwa sasa ni kauli za kuzuia uchaguzi, lakini wanaobeba agenda hiyo hawasemi watazuiaje uchaguzi bila kumwaga damu za raia wasio na hatia, angalau hawa G55 wameonyesha njia ya kupita.
Kinachoonekana hata viongozi wenyewe wa Chadema baadhi yao wamebeba agenda ya ‘No Reforms, No Election’ bila kuielewa, wakisimama katika “kuzuia uchaguzi” au “Kususia uchaguzi”. Kususia ni haki yao, ila kuzuia itakuwa ni ndoto za mchana.
Chadema wanaweza kutafutana uchawi kuwa wapo miongoni mwao wamepewa fedha ili kukivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi kama ambavyo wameanza kulipa jina baya kundi la G55, lakini ukweli mkakati huo hautekelezeki.
Bahati mbaya sana, kelele nyingi za mkakati huu unakutana nazo kwenye mitandao ya kijamii zaidi na mikutano ya hadhara ya Lissu na timu yake tu, niwaulize, ni kiongozi gani wa kanda, mkoa au kata ameshusha huu mkakati huko chini?
Ukisoma Ibara ya 5(1) inasema kila raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 ana haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania na wananchi. Maana yake hii ni haki ya kikatiba, utazuiaje uchaguzi ukijua ni kuvunja Katiba?
Ibara ndogo (2) inasema hakuna sababu nyingine yoyote inayoweza kumzuia raia asitumie haki ya kupiga kura usipokuwa kama si raia wa Tanzania, ni mgonjwa wa akili, ametiwa hatiani kwa makosa fulani kutokuwa na kitambulisho cha kura.
Katiba na sheria zetu zinasema uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utafanyika kila baada ya miaka mitano, maana yake kutofanya uchaguzi mkuu Oktoba, 2025 itakuwa ni uvunjwaji wa Katiba ambayo ndio sheria mama.
Njia pekee inayoweza kuzuiwa kufanyika kwa uchaguzi ni kupitia Ibara ya 32 ya Katiba kwa Rais kutangaza hali ya hatari au kupitia ibara ya 44 kwa Rais kutangaza kuwapo kwa hali ya vita kati ya Jamhuri ya Muungano na nchi yoyote.
Ukiacha Katiba yetu, ukisoma kifungu cha 129 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024 inazungumzia kuwa ushawishi mbaya ni kosa na ushawishi huo ni pamoja na kumzuia mtu asipige kura.
Kifungu hicho kinasema mtu ambaye kwa dhahiri au kwa kificho, yeye mwenyewe au mtu mwingine kwa niaba yake, anatumia au kutishia kutumia nguvu, vurugu au kizuizi, ili mtu apige kura au asipige kura anatenda kosa chini ya sheria hiyo.
Hii ni pamoja kama mpiga kura huyo amepiga kura au ameacha kupiga kura katika uchaguzi wowote au ambaye, kwa kumteka nyara, vitisho au hila ya aina yoyote, kumkwamisha au kumzuia kutumia uhuru wa kupiga kura mpiga kura yeyote.
Sasa kwa Katiba na sheria nilizozinukuu hapo, Chadema watazuiaje uchaguzi kama sio kupoteza muda ama kukaribisha vyombo vya dola yakiwemo majeshi yetu kukabiliana nao. Nasema hivyo kwa sababu ukitizama kwa sura ya kisheria, wakitekeleza wanachokisema itakuwa ni uasi na vyombo vilivyopewa wajibu wa kulinda amani kisheria zitaingia kazini kutekeleza wajibu wake kisheria.
Binafsi nawaelewa Chadema na ACT-Wazalendo kutokana na madhila ambayo wao na wafuasi wao wamepitia katika kuenguliwa, baadhi kujeruhiwa na wengine kufunguliwa kesi ambazo ninathubutu kuziita ni za “kisiasa”.
Ninakubaliana na Chadema na wanaharakati wengine kuwa njia halali na za kisheria za kupinga sheria mbovu za uchaguzi zimekwaa kisiki mahakamani na nyingine kubadilishwa, sasa je, ni halali kudai haki kwa kuvunja Katiba na sheria za nchi? Tunatokaje hapa?
Kwa maoni yangu, Chadema wabadili gia angani na waitishe mikutano ya dharura ya Kamati Kuu, Baraza Kuu na Mkutano Mkuu kabla ya Bunge kuvunjwa, ili wapitie upya “No reforms, no election” na kuja na mikakati inayotekelezeka bila kuleta madhara.
Hadi ninapoandika makala hii leo Aprili 7, 2025, Chadema wenyewe sio wamoja tena tangu kumalizika kwa uchaguzi wa viongozi wa kitaifa, mkakati huo haueleweki si tu kwa wanachama na wafuasi, bali hata viongozi wao nao hawajui utatekelezwaje.
Kauli ya John Mrema kuwa mkakati huo ulikuwa ni kama amshaamsha na ulikuwa na vipengele vingi tu na kuwa hata Mbowe wakati anautangaza Desemba 2024 hakutamka kuwa watazuia uchaguzi, unadhihirisha kutoeleweka mkakati huo.
Ni kweli Ibara ya 8(1) (a) ya Katiba ya Tanzania inasema wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi, sasa kama kuna kundi limekengeuka wananchi tufanyeje?
Ndio maana nilitangulia kusema Chadema wabadili gia angani na kwa kutumia katiba yao, waitishe vikao vya kikatiba kujadili mkakati huo.
Inapaswa irudi mezani ijadili namna itakavyotekeleza mkakati huo katikati ya uwepo wa kundi lingine ndani ya chama linalopinga mkakati huo. Kundi hilo linakubaliana na mkakati wa kudai mabadiliko, lakini sio kuzuia uchaguzi.
Kwa mazingira yalivyo, na wakaenda kichwa kichwa watajitengenezea kesi za uhaini kwa sababu kuzuia uchaguzi ni kosa kubwa la kuvunja Katiba ya nchi, ila umma kama umma ukiamua, hakuna wa kuzuia maamuzi yake.