Kilwa. Mvua zinazoendelea kunyesha katika Mkoa wa Lindi hasa wilayani Kilwa, zimesababisha kukatika kwa baadhi ya madaraja likiwamo la Somanga – Mtama na la Mto Matandu ambalo awali liliharibiwa na mvua zilizoambatana na Kimbunga Hidaya, Mei 5, 2024.
Mvua na Kimbunga Hidaya vilileta madhara katika barabara ya kusini na kufunga mawasiliano kwa siku tatu, hata hivyo Serikali ilijitahidi kufanya marekebisho kwa haraka na mawasiliano yalirejea.
Madaraja hayo yamekatika tena Aprili 6, 2025, Daraja la Somanga – Mtama lilikatika saa 12 asubuhi Aprili 7, 2025 huku Daraja la Mto Matandu lilikatika na kufunga mawasiliano kwa mikoa ya kusini.

Akizungumza eneo la tukio leo Jumatatu Aprili 07, 2025, abiria aliyekuwa anatoka Lindi kwenda Mkoa wa Pwani, Hamis Juma amesema walipofika eneo la Mto Matandu walikuta daraja limekatika, hivyo wakasitisha safari yao.
“Nimetoka Lindi naelekea Mkoa wa Pwani, sasa tumefika hapa saa 12 asubuhi, leo tumekuta limekatika (daraja),” amesema Juma.
Sabrina Alex, ameiomba Serikali kufanya matengenezo haraka ili kurudisha mawasiliano na kuendelea na safari ya kwenda Dar es Salaam.
“Hadi sasa madaraja mawili tayari yamekatika, sisi tumekwama hapa Mto Matandu, tunaiomba Serikali ijitahidi kurudisha mawasiliano haraka ili tuendelee na safari,” amesema Alex.

Licha ya changamoto hizo, makandarasi wanaendelea na matengenezo katika Mto Matandu ili kurudisha mawasiliano kwa muda.
Endelea kufuatilia Mwananchi kupitia tovuti na mitandao yake ya kijamii