Mashahidi kutotajwa kesi ya mauaji ya bilionea wa madini, mwanaye

Songea.  Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, imetoa maagizo sita yanayozuia kutajwa majina na mahali wanapoishi mashahidi wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya watu wawili inayomkabili Hussein Kadari na wenzake sita.

Lengo la upande wa mashitaka kuwasilisha ombi la kuzuia kutolewa utambulisho wao ni kwamba, mashahidi ni ndugu wa karibu na washitakiwa na wanafahamiana vizuri, hivyo inaweza kuathiri kesi ya Jamhuri.

Hata hivyo, kwa mujibu wa kiapo cha Mwendesha Mashtaka wa Mkoa (RPO), Kauli Makasi na Mrakibu wa Polisi (SP), Essau Ikamaza, mashahidi wako katika vitisho, huku aliye muhimu alishakufa kifo cha ajabu.

Kesi hiyo imekuwa ikivuta hisia za wadau wa haki jinai na wananchi wengine kutokana na namna vifo vilivyotokea, ikidhaniwa walifariki dunia kwa ajali lakini baada ya uchunguzi, polisi waliona yalikuwa mauaji ya kukusudia.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika shitaka la kwanza, washitakiwa wanadaiwa Agosti 29, 2023 wakiwa eneo lisilofahamika kati ya Mbeya na Songea katika Barabara Kuu ya Mbeya-Songea, walimuua John Masese, ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara wa madini.

Katika shitaka la pili, inadaiwa Agosti 29, 2023 katika Kijiji cha Lilondo wilayani Songea, Mkoa wa Ruvuma, washtakiwa walimuua Marwa Senso.

Usikilizwaji wa awali ili kuihamishia kesi Mahakama Kuu umepangwa kufanyika Aprili 9, 2025.

Taarifa zilizotolewa awali wakati wa tukio, zilieleza kuwa Marwa alikuwa mfanyabiashara wa madini.

Uamuzi wa kuzuia kutajwa majina ya mashahidi na maeneo wanapoishi ulitolewa Aprili 3, 2025 na Jaji Emmanuel Kawishe baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuwasilisha maombi ya jinai namba 7498 ya mwaka 2025.

Maombi hayo yaliyosikilizwa upande mmoja (Ex-Parte) bila washitakiwa kuwepo, yalikuwa dhidi ya wajibu maombi ambao ni Kadari, Erasto Swai, Joseph Komba, Alfred Milinga, Grace Senso, Sarah Bundala na Elizabeth Ndunguru.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, DPP aliwakilishwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Generosa Montano na Wakili wa Serikali, James Robby waliosisitiza mashahidi na washitakiwa ni ndugu na wengine ni wa damu.

Generosa alimweleza Jaji kuwa, mshitakiwa wa pili, Erasto Swai, Joseph Komba (wa tatu) na Elizabeth Ndunguru (wa saba) ni ndugu wa mama mmoja, wakati mshitakiwa wa kwanza, Kadari ni mume wa mshitakiwa wa sita, Sarah Bundala.

Alisema mshitakiwa wa tano, Grace Senso ni mama mzazi wa mshitakiwa wa sita na mmoja wa marehemu katika hati ya mashitaka, Marwa Senso ni kaka wa mshitakiwa wa tano.

Marehemu John Masese, anayedaiwa kuuawa na washitakiwa, ilielezwa alikuwa mwajiriwa wa mama mzazi wa mshitakiwa wa kwanza, hivyo kutolewa maelezo ya washitakiwa kuwatambulisha mashahidi.

Wakili alisema hadi maombi hayo yanasikilizwa, mmoja wa mashahidi muhimu wa Jamhuri ambaye hata hivyo hakumtaja, amekufa kifo cha ajabu na kwa mazingira hayo aliomba majina ya mashahidi wote yalindwe na yasitajwe.

Katika uamuzi, Jaji Kawishe amesema kifungu cha 188(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinaipa Mahakama mamlaka ya kuzuia kutolewa maelezo ya mashahidi pale inapopokea maombo ya DPP.

Jaji Kawishe amesema ulinzi kwa mashahidi walioko katika kitisho cha usalama ni suala linalokubalika duniani na kwamba, linakubalika chini ya sheria za kimataifa na sheria za Tanzania.

“Sababu kuu ya kulinda mashahidi ni kwamba, wanachukuliwa kama nguzo ya Mahakama katika kutoa haki. Katika haki jinai, mashahidi hawana manufaa wanayopata isipokuwa kama hawatalindwa, maisha yao yanaweza kuwa hatarini.

“Kwa hiyo, mashahidi ni macho na masikio ya haki kwa kigezo kuwa, Mahakama imepewa wajibu wa kuhamasisha na kutoa haki kwa mujibu wa sheria, lakini inayo mamlaka pia ya kuwalinda mashahidi,” amesema Jaji Kawishe.

Jaji Kawishe amesema: “Katika maombi haya, wakili wa Serikali kupitia wasilisho lake na hati ya viapo, alieleza mashahidi wa Jamhuri wako katika tishio na ni ndugu wa karibu wa washtakiwa, hivyo kuwataka kutahatarisha maisha yao.”

Jaji Kawishe amesema  maelezo yaliyopo katika viapo hivyo yanaonyesha usalama wa mashahidi uko hatari kwa kuwa kumekuwapo majaribio kutoka kwa washirika wa washitakiwa, kupata majina ya mashahidi kwa lengo la kuwapa vitisho.

“Hii inaweza kufanya mashahidi hao wanaokusudiwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola wakati wa usikilizwaji wa kesi hii na imeelezwa kuwa shahidi mmoja muhimu tayari amekufa kifo cha ajabu,” amesema.

Jaji Kawishe amesema kwa kuzingatia aina ya kesi ambayo washitakiwa wanadaiwa kula njama ya kupata majina ya mashahidi, kuruhusu watoe ushahidi wao wazi bila kuwalinda ni kuwasababishia hatari wao na familia zao.

Kutokana na uzito wa hoja za DPP, Jaji ametoa amri ya kuzuia kutolewa kwa utambulisho wa mashahidi na mahali walipo, wakati wa usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea wa kuihamishia kesi Mahakama Kuu.

Mbali na amri hiyo, ameamuru kutowekwa wazi maelezo ya mashahidi na nyaraka nyingine yoyote itakayosababisha mashahidi kutambulika wakati wa usikilizwaji wa awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.

Pia, ameamuru usikilizwaji huo wa awali wa kesi (PI) ili kuihamishia Mahakama Kuu iwe faragha na hakuna kusambaza au kuchapishwa ushahidi wa nyaraka au ushahidi wowote utakaowatambusha mashahidi wa Jamhuri.

Mbali na amri hiyo, ameamuru ni marufuku kusambaza taarifa zozote zinazoweza kubainisha eneo, makazi au mahali walipo mashahidi wa Jamhuri katika kesi hiyo au kuwataja ndugu wa karibu na washitakiwa.

Jaji Kawishe amesema kwa minajili ya kutenda haki, wakati wa usikilizwaji wa shauri hilo, washtakiwa watapatiwa muhtasari tu wa ushahidi ambao Jamhuri itauegemea bila kutaja majina, utambulisho au mahali walipo mashahidi wa Jamhuri.

Wakili Peter Madeleka anayemtetea mshitakiwa wa kwanza, Hussein Kadari alipoulizwa na Mwanachi leo Aprili 7, 2025 kuhusu uamuzi huo amesema hana taarifa kwa kuwa maombi yalisikilizwa upande mmoja, hivyo watakutana Mahakama Kuu.

Related Posts