MIAKA 53 BILA KARUME:SOMA MKASA ULIVYOTOKEA MPAKA AKAUAWA KWA RISASI

MIAKA 53 BILA KARUME: Mkasa ulivyokuwa siku ya tukio

By Ngilisho Tv 


Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

APRILI 7 mwaka 1972 visiwa viwili vya Unguja na Pemba pamoja na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huzuni kubwa ilitanda kutokana na kuuawa kwa kupigwa risasi Rais wa Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume.

Mzee Karume wakati anauawa, alikuwa ana cheo kingine kikubwa. Ndiye alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais wa Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Luteni wa Jeshi Homuod Mohamed Homoid ndiye aliyeingia katika ofisi za Makao Makuu ya ASP zilizoko Kisiwandui, kisiwani Unguja  kutimiza nia yake ovu iliyokatisha ghafla maisha ya kiongozi mpendwa wa Zanzibar.

Haijafahamika hadi leo ni kwanini mwanajeshi huyo katili aliweza kutenda shambulio ambalo liliacha majonzi makubwa katika jamii ya watanzania na wazanzibari, japo kuna tetesi kwamba alilipiza kisasi kutokana na kuuliwa kwa baba yake.

Mwanajeshi huyo alipigwa risasi na askari wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kabla hajatoka ndani ya geti la Makao Makuu ya ASP.

Licha ya kuwahishwa na kufikishwa katika Hospitali  Kuu ya Zanzibar huko Mnazi mmoja (Karimjee Jivanjee), Mzee Karume alikata roho na kuwaacha watanzania wakiwa kwenye vilio ambavyo vimekosa mnyamazishaji hadi leo.

Inaelezwa katika vitabu vya historia ya Zanzibar kuwa wakati mwanajeshi huyo anavamia ofisi za Makao Makuu ya ASP, alimkuta Mzee Karume akiwa ameketi huku wakicheza dhumna na baadhi ya wazee wenzake na viongozi wa ngazi za juu wa ASP.

Kati ya wazee hao, alikuwapo pia Makamo wa Rais wa ASP, Hayati Mzee Mtoro Rehani Kingo na Katibu Mkuu wa ASP, Sheikh Thabit Kombo Jecha, Sheikh Mohsin bin Ali na wazee wengine kadhaa mashuhuri wa ASP.

Hamoud alifika Kisiwandui kwa dhamira kuu ya kukatisha maisha ya Mzee Karume, jambo ambalo linatajwa kuwa limeirudisha nyuma Zanzibar katika harakati zake za maendeleo na kiuchumi kwa miaka 20.

Kilikuwa kifo kilichokatisha ndoto nyingi za Mzee Karume katika kuifanya Zanzibar kuwa na maendeleo aliyowahi kuyaona katika nchi nyingi alizowahi kufika wakati akiwa baharia.

Kwa muda wa miaka minane ya utawala wake, Zanzibar ilipanda chati na kuyavuka maendeleo ya karne mbili yaliyoletwa na utawala wa kisultani katika visiwa vya Zanzibar.

Taarifa za msiba wa Mzee Karume ziliitingisha Afrika Mashariki nzima, vilio vilihanikiza kwa watu wote, wake kwa waume na watoto katika maeneo ya mijini na vijijini.

Kiongozi kipenzi cha watu wote ambaye anatajwa hakuwa mbaguzi, alikuwa kiungo kikuu katika jamii. Ndiye kiongozi anayetajwa “kama si yeye, pengine Muungano wa Tanganyika na Zanzibar usingekuwapo”.

Ni Rais Karume aliyemwambia Mwalimu Nyerere muungano ufanyike haraka na Nyerere, tena akimwomba awe Rais wa kwanza katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

KUHUSU KARUME 

Ndiye Rais wa Pili wa chama cha African Association, akimrithi Rais wa kwanza, Hayati Agostino Ramadhan. Mzee Karume alizaliwa mwaka 1905 visiwani Zanzibar. Alipata elimu ya msingi kisha akaanza kujishughulisha na kazi za ubaharia.

Akiwa kwenye ubaharia, kiongozi huyo ambaye wazazi wake wana asili ya Nyasaland (Malawi), alikuwa anawashawishi waafrika wenzake kukataa kutawaliwa na hivyo wapiganie uhuru wao.

Aliwaunganisha waafrika wenzake kupitia bendi ya muziki na mchezo wa soka katika klabu maarufu ya African Sports ya Zanzibar.

African Association chini ya uongozi wa Mzee Karume ndio iliyoanzisha uhusiano na ushirikiano na Tanganyika African Association ya Tanganyika katika pirikapirika za kutaka waafrika kujitawala wenyewe.

Baada ya kushamiri vuguvugu la kisiasa kufuatia kuvuma kwa kasi upepo wa mabadiliko ya kupigania Bara la Afrika, Tanganyika African Association (TAA) ilijibadili na kuunda chama cha kisiasa cha TANU, yaani (Tanganyika African Association) Julai 7 mwaka 1954.

African Association kwa upande wa Zanzibar nayo ililazimila kujibadili na kuwa chama cha kisiasa na kuwa kwa chama cha Afro Shiraz Party (ASP).

Kuundwa kwa ASP ni matokeo ya kuungana kwa jumuiya mbili za African Association na Shiraz Union na kuzaliwa chama cha kisiasa cha ASP Februari 5, 1957.

Kizazi hiki na kijacho kitaendelea kumkumbuka Mzee Karume si kwa sababu nyingine yoyote zaidi ya kuleta ukombozi wa Zanzibar toka katika utawala wa kisultan uliolindwa na Uingereza.

Akiwa anaendelea kukumbukwa siku zote jinsi alivyoweza kuwaunganisha wazanzibar chini ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, pia watanzania katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katu haiwezekani kuzungumzia amani, umoja na mshikamano wa miaka 61 ya Muungano bila kutambua mchango mkubwa uliotolewa na Hayati Mzee Karume ambaye ndiye aliyekuwa kinara wa kuunda taifa jipya la Tanzania.

Wazanzibar na watanzania wanaamini kuwa kilichokufa ni mwili wa Mzee Karume, lakini fikra, maono na mtazamo wake kwa yale yote mema alioyaanzisha, yataendelea kuenziwa na kutekelezwa kwa vitendo.

Related Posts