Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Mkoa wa kichama Ilala, kimewaagiza viongozi wake wa matawi kuwaandikia barua makada wake saba akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki na Mawasiliano ya Mambo ya Nje, John Mrema wajieleza kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu baada ya kujitokeza hadharani kupinga msimamo wa chama hicho.
Mbali na Mrema makada wengine walioingia kwenye kundi hilo la kulimwa barua ni Joseph Wamajiwa, Tausi Mroso, Blakwelu Kayuni, Patrick Assenga, Rechael Mkadala na Asia Msangi .
Katika kukazia maagizo hayo pia kimewaagiza makatibu wa wilaya kufuatilia utekelezaji wake kwa ukaribu hadi kesho wawe wamefikishiwa barua hizo na wajieleze ndani ya siku 14 na kutoa mrejesho ofisi za mkoa huo.
Sababu ya kuandikiwa barua hizo ni kitendo cha Mrema na wenzake wanaounda kundi la G55 kutoka hadharani jana Jumapili Aprili 6, 2025 kupinga kampeni ya chama hicho ya ‘No reforms, No election’ inayolenga kuishinikiza Serikali kufanya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi ndipo uchaguzi mkuu ufanyike.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jumatatu Aprili 7,2025 jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Mkoa huo, Mwenevyale Waziri amesema kupinga maamuzi halali ya vikao vya chama kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ni kosa.
“Hivyo nawaagiza viongozi wote wa matawi katika maeneo yote ambayo wanatoka makada wanaounda G55 katika majimbo yote matatu, Ukonga, Segerea na Ilala na walijitokeza hadharani akiwemo Mrema waandikiwe barua ya kujieleza ndani ya siku 14, na makatibu wangu nawaagiza wafuatilie utekelezaji wake hadi kesho ziwafikie na mtoa mrejesho ofisi za mkoa,” amesema.
Waziri amesema kada yeyote mwenye maoni anatakiwa kutumia vikao halali kuwasilisha hoja yake kwa kuwa Mrema na wenzake ni wanachama wa kawaida, walipaswa kutumia vikao vya matawi na viongozi wao wayafikishe ngazi ya juu.
“Lakini wao wameanzisha kundi ambalo chama hakijui malengo yake na hawajakitaarifu huu ni usaliti. Na kupinga ajenda ya chama hadharani ni usaliti wa pili lakini kukataa ajenda ambayo baadhi yao walishiriki kuipika ni usaliti na kwa mujibu wa katiba yetu makada hawa lazima wachukuliwe hatua za kinidhamu.”
“Vilevile kama kuna waliopo ngazi ya majimbo basi nawaelekeza nao wachukue hatua hizo wajieleze kwa nini wasichukuliwe hatua za kinidhamu kwa kupinga msimamo wa chama,” amesema .
Akinukuu vifungu vya katiba ya chama hicho, Waziri amesema ibara ya 5:3 kwenye wajibu wa mwananchama kipengele cha tano, kinasema kila mwanachama anawajibu wa kushiriki vikao vya chama vinavyohusu shughuli zingine za chama kadri inavyowezekana.
“Kama walikuwa na hoja walitakiwa kuhudhuria vikao vya chama vya ngazi zao na watoe hoja, na viongozi watapeleka ngazi ya juu,” amesema