Saba wahukumiwa kunyongwa hadi kufa ndani ya miaka minne mkoani Mbeya

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limesema kwa miaka minne iliyopita linajivunia mafanikio mengi, ikiwamo watuhumiwa saba waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na matukio ya mauaji.

Mafanikio mengine ni kupata askari wapya 351 waliohitimu mafunzo ya kijeshi, huku wengine 1,162 waliokuwa katika nafasi mbalimbali wakipandishwa vyeo.

Leo Jumatatu, Aprili 7, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema katika kipindi hicho wamefanikiwa katika operesheni, misako na doria, na watuhumiwa wa uhalifu walikamatwa na mali zilizoibiwa zikarejeshwa kwa wahusika.

Amesema mafanikio mengine ni kupata magari 14 kwa ajili ya shughuli za doria na kuimarisha usalama, pamoja na pikipiki 14 kwa ajili ya wakaguzi, hali inayoongeza ufanisi katika majukumu ya jeshi hilo.

“Watuhumiwa saba walipatikana na hatia na kuhukumiwa kunyongwa hadi kufa kutokana na matukio ya mauaji. Tulikamata silaha 40 zisizo na kibali na nyara za Serikali zenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Jumla ya askari 1,162 walipandishwa vyeo katika nafasi mbalimbali, huku tukipokea askari wapya 352 waliohitimu mafunzo ya kijeshi. Haya ni mafanikio makubwa katika miaka minne ya jeshi letu Mbeya,” amesema Kuzaga.

Kamanda huyo ameongeza kuwa katika ajali, jeshi hilo limefanikiwa kupunguza kwa asilimia 2.8, huku upande wa uhalifu ukipungua hadi asilimia tatu, na hiyo ni kutokana na vitendea kazi vya kisasa walivyopata na kuimarisha mfumo wa kidijitali na kusogeza huduma kwa wananchi kupitia ujenzi wa vituo vya polisi.

“Watuhumiwa 133 wa mtandao wa wizi wa mtandaoni walikamatwa. Tumepunguza mlundikano wa mahabusu magerezani. Madini ya zaidi ya Sh1 bilioni yaliyokuwa yakitoroshwa yalikamatwa na watu tisa kushikiliwa, na bidhaa za magendo zenye thamani ya zaidi ya Sh390 milioni zilikamatwa.

“Wahamiaji haramu 174 walikamatwa, lakini watuhumiwa 23 wa matukio ya kubaka na kulawiti walipatikana na hatia na kufungwa maisha gerezani,” amesema Kamanda huyo.

Mmoja wa wadau wa maendeleo jijini Mbeya, Gift Mbelwa, amesema pamoja na mafanikio ya jeshi hilo, linapaswa kuongeza nguvu hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu kwa kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali.

“Kipindi cha uchaguzi matukio huwa ni mengi. Kwa kuwa jeshi linafika maeneo yote, lijipange zaidi kuzuia uhalifu na matukio mengine ambayo mara kadhaa yamekuwa yakijitokeza, ikiwamo mauaji ya wasio na hatia,” amesema Mbelwa.

Related Posts

en English sw Swahili