WAKATI Ligi ya Wanawake ikiishia raundi ya 15 kutokana na mapumziko ya kalenda ya FIFA kwenye fainali za AFCON (Women’s Futsal Cup of Nations 2025) zitakazofanyika Morocco mwezi huu, Bunda Queens ni timu pekee iliyocheza mechi chache.
Bunda imecheza mechi 11 kati ya 15 zilizocheza baadhi ya timu, ikishinda mechi mbili, sare tatu na kupoteza sita ikiwa nafasi ya tisa na pointi tisa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa timu hiyo, Alley Ibrahim alisema baadhi ya mechi ziliahirishwa kutokana na wachezaji wao muhimu kuitwa timu za taifa.
Ibrahim aliongeza, waliuomba uongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) kusogeza mbele mechi hizo ili kuwasubiri nyota watakaotoka kwenye majukumu ya taifa.
“Ni kweli mechi zetu ziliahirishwa sababu ni wachezaji wetu watano wako timu ya taifa U-17 karibu kikosi kizima kinachoanza kwenye timu kiko kwenye majukumu,” alisema Ibrahim na kuongeza;
“Ndiyo maana mmeona kwenye timu 10 za ligi, sisi Bunda ndiyo tumecheza mechi chache na hiyo ndio sababu, Bunda ina vijana wengi wadogo ambao ni muhimu kwenye taifa, tusingeweza kuwazuia kwa sababu wanawakilisha nchi zao.”