Serikali yaweka msimamo hatima ya mgodi wa dhahabu Magambazi

Handeni. Serikali imesema itaendelea na msimamo wa kutozihuisha leseni za Kampuni ya PMM Tanzania Limited inayoendesha na kumiliki mgodi wa kati wa dhahabu wa Magambazi, uliopo wilayani Handeni, mkoani Tanga, kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wake.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Nyasa, Kata ya Kang’ata, Wilaya ya Handeni, jana Jumapili, Aprili 6, 2025, alipofanya ziara ya kukagua utendaji kazi wa kampuni hiyo na kuongea na wananchi.

Amesema baada ya kusikiliza pande zote za Kampuni ya PMM na CANACO zinazohusika katika mgodi huo, ameona ni muhimu kuchukua hatua ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaleta manufaa kwa wananchi wa Nyasa, Handeni, na taifa kwa ujumla, kwani ni muda mrefu hakuna manufaa yoyote.

Waziri Mavunde ametoa siku 30 kwa Kampuni ya PMM Tanzania Limited inayoendesha na kumiliki mgodi wa kati wa dhahabu wa Magambazi, kuwasilisha taarifa za kifedha na kiufundi ili kuthibitisha uwezo wake wa kuendesha mgodi huo kwa viwango vinavyohitajika kisheria.

“Serikali imeendelea na msimamo wa kutozihuisha leseni hizi mpaka mambo yafuatayo yafanyike kwa mujibu wa taratibu. Cha kwanza, tumekubaliana ndani ya siku 30, Aprili 8 mpaka Mei 7, 2025, iwasilishwe kwangu taarifa ya kifedha na kiufundi kama sheria inavyoelekeza ya uendeshaji wa mgodi huu ndani ya siku 30,” amesema Mavunde.

Amesema kuwa sheria hiyo inaelekeza kuwa yule anayemiliki na kuendesha mgodi huyo lazima athibitishe uwepo wa kiasi cha fedha za Kitanzania kwa mujibu wa maandiko ya mradi, ambazo ni zaidi ya Sh30 bilioni, na inapaswa ionekane kwenye vitabu vitakavyowasilisha kwake ndani ya muda huo.

Kadhalika, amewaelekeza wamiliki hao kuhakikisha katika kipindi hicho cha siku 30, kama kampuni haitakuwa na uwezo wa kuendesha mgodi, itoe taarifa ili apewe mwekezaji mwenye uwezo wa kiufundi na kifedha kuendesha mgodi huo kwa tija, na kwamba kinyume na hapo, Serikali itachukua hatua za kutangaza mgodi huo kwa wawekezaji wengine wenye sifa.

Pia, amemwelekeza Mkuu wa Wilaya ya Handeni kuandaa utaratibu maalumu wa kuhesabu fedha za asilimia mbili kutoka mauzo ya awali ya dhahabu na kuhakikisha zinawekwa kwenye akaunti ya maalumu kwa ajili ya wachimbaji wadogo waliopisha maeneo hayo ya uchimbaji kama walivyokubaliana awali.

Kuhusu alichokisema Waziri, Mkurugenzi wa Kampuni ya PMM Tanzania Limited, Spendi Ulimbakise, amesema wapo tayari kuanza kufanya uzalishaji isipokuwa walikuwa na changamoto ya kutokuwa na mpango kazi mgodini.

Amesema baada ya kuchukua mgodi huo, hawakupewa baadhi ya taarifa muhimu za mgodi, ikiwemo mpango kazi, hivyo ilibidi kuanza mchakato upya uliohusisha kufuatilia wizarani ili kuanza kazi. Tayari baadhi ya taratibu zimeanza kukamilika ili kuanza kwa shughuli za uchimbaji katika mgodi huo wa Magambazi.

“Sababu hizo na nyingine za kiutendaji ndizo zimesababisha kushindwa kuanza kazi kwa wakati mpaka sasa, na kutokana na baadhi ya changamoto kupatiwa ufumbuzi, wapo tayari kwa msaada wa Serikali kuanza kazi ya kuchimba dhahabu, kwani utafiti unaonyesha ipo ya kutosha,” amesema.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahaya Samamba, amesema sababu iliyotolewa na mwekezaji huyo sio kweli, kwani katika shughuli za uchimbaji, kuna kazi zinazoweza kufanyika bila hata kusubiri miongozo ya Serikali, lakini mpango kazi wa mgodi wa Magambazi upo.

Amesema walichoombwa wao pamoja na migodi mingine ni taarifa kuhusu utendaji kazi wao, kuonyesha wamevuna kiasi gani au hawakuvuna na shughuli nyingine, ambapo hiyo haizuii wao kuendelea na uchimbaji, kwani ni taarifa za kiutendaji.

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando, amesema madhara yanayotokana na migogoro inayofanyika mgodini hapo ni wananchi kukosa ajira, kukosa fursa za shughuli za maendeleo, na huduma muhimu za kijamii, hivyo lazima uamuzi ufanyike.

Amesema hakuna sababu ya Serikali kuruhusu wawekezaji, lakini wananchi wanakosa huduma kama maji safi, elimu bora, na miundombinu mingine wakati upo mgodi unaozalisha dhahabu na nao wakanufaika.

Mgodi wa Magambazi uligunduliwa na wachimbaji wadogo mwaka 2003, ambapo baadaye waliondolewa na kupewa kampuni ya Canaco Tanzania Ltd. Ikaingia kampuni ya Tanzania Gold Field, na sasa ipo Kampuni ya PMM Tanzania Limited, lakini wakati huo kumekuwa na migogoro baina yao na Serikali kwa kushindwa kufanya shughuli za uchimbaji.

Related Posts