Ulimwengu aeleza mfanano wa G55 ya Chadema na ile ya CCM

Dar es Salaam. Wakati uamuzi wa watia nia wa ubunge wa Chadema wa kujiita G55 ukitajwa kuwakosea heshima waasisi wa jina hilo, aliyekuwa Katibu wa G55 ya mwaka 1993, Jenerali Ulimwengu amesema hakuna tatizo, huku akionyesha mfanano wa muktadha kati ya muungano wa sasa na wa zamani.

Kwa mujibu wa Ulimwengu, G55 ya sasa ni kundi linalojenga hoja mbadala ndani ya Chadema kupinga kuzuia uchaguzi, wakati ile ya zamani ilijenga hoja mbadala ndani ya CCM kushawishi kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano.

Licha ya hicho kinachotajwa kuwa ni mfanano wa muktadha, rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi anasema kutumika kwa jina hilo na vikundi vya sasa ni kunajisi historia ya taifa na kuwakosea heshima wazalendo.

Asili ya jina G55 ni muungano wa wabunge wa CCM mwaka 1993, waliotofautiana na msimamo wa chama chao, wakidai kuundwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Serikali ya Muungano.

Jina hilo limeibuka tena sasa, lakini katika mazingira tofauti, wakati huu likihusisha muungano wa watia nia wa ubunge wa Chadema wanaopinga ajenda ya kuzuia uchaguzi, ambao ni msimamo wa chama chao.

Hata hivyo, Chadema iliwaita na kusisitiza msimamo wake kuwa, iwapo mabadiliko ya kisheria hayatafanyika, hakutakuwa na uchaguzi mwaka huu.

Kuibuka kwa kundi hilo nyakati hizi kumeibua mijadala katika mitandao ya kijamii, baadhi wakipinga jina hilo kunasibishwa kati ya kundi la zamani na la sasa.

Mwabukusi ni miongoni mwa wanaopinga jina hilo kutumika, akisema kimantiki G55 ya awali ilikuwa harakati ya kizalendo inayohusisha wanamapinduzi waliokuwa wakidai jambo lenye maslahi ya Watanganyika wote.

Kwa mujibu wa Mwabukusi, harakati hiyo ililenga kupigania maslahi ya taifa na ilifanywa na watu walioamua kuweka pembeni itikadi zao za kisiasa kupambania Watanganyika.

“Kwa sababu za kimantiki na umuhimu, pia uzito wa ile harakati ya G55 ya miaka ya 1990, hatupaswi kuruhusu watokee walevi wajinasibishe hivyo. Eti kikundi cha walevi wakikaa waamue kujiita G55, tunapoteza historia,” anasema.

Anasema suala la Muungano ni kubwa na muhimu kwa Watanganyika, na G55 ndilo kundi pekee lililojikaza kuzungumza kwa maslahi ya Watanganyika.

“Hoja za G55 ziliilazimisha Serikali kutengeneza mazingira ya kuitenga hoja na kuiua, ingawa haijawahi kufa, na hatujawahi kuwa na kundi muhimu kama lile,” amesisitiza.

Kwa umuhimu wa kundi hilo, amesema si sawa kitokee kikundi chochote kwa sasa kijinasibishe kwa jina hilo, kwani itasababisha lipoteze mantiki yake.

Kwa ajili ya manufaa ya vijana hasa wa miaka ya sasa, amesema ni muhimu kusiwepo watu wanaoharibu mantiki ya G55 ya mwaka 1993.

Mwabukusi anasema kinachochanganya zaidi ni kwamba G55 ya sasa inalalamikia jambo ambalo kwa sehemu kubwa ya wanamuungano huo walikuwepo wakati linapitishwa.

“Huwezi kuwawekea watu chakula mezani halafu ukaanza kuhoji usafi wa mpishi, wakati wewe ni sehemu ya hao wapishi. Kama walipika kibichi wasije mtandaoni kutuchanganya, warudi kwenye mifumo yao ya chama kuweka mambo yao sawa,” anasema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, aliyekuwa Katibu wa G55 ya zamani, Jenerali Ulimwengu anasema haoni tatizo kwa wanachama hao wa Chadema kutumia jina hilo ili kuyapa mawazo yao ushawishi.

“Katika mazingira tofauti watu wakitumia majina ya zamani kwa sababu labda yanapendeza au wanalenga kuyapa mawazo yao ushawishi wa aina fulani, hiyo haiondoi maana ya G55 ya mwaka 1993, ila inavuta kidogo ushawishi wa watu fulani waliofuatilia G55 na historia yake,” anasema.

Hata hivyo, Ulimwengu anasema pengine kuna mwangwi wa miaka 30 iliyopita unaosikika ndani ya G55 ya sasa, ingawa mantiki inaweza kuwa tofauti.

Anasema G55 ya wakati huo ilikuwa harakati ya kuleta mawazo yanayotofautiana na msimamo wa CCM, ndivyo ilivyo hata kwa kundi lililojipa jina hilo kwa sasa—linaibua fikra tofauti ndani ya Chadema.

“Huu wa sasa ni ubishi ndani ya Chadema na ile ya wakati ule ulikuwa ubishi ndani ya CCM,” anaeleza.

Anakwenda mbali zaidi na kueleza kuwa G55 ya sasa inasema haitofautiani na chama kuhusu uhitaji wa ‘reforms’, kama ambavyo ya zamani ilisema haitofautiani na chama kuhusu Muungano.

“Wao wa sasa wanasema wanatofautiana na chama kuhusu kuzuia uchaguzi, nasi tulisema tunatofautiana na chama kwa kujenga hoja kuwa Muungano utaimarika zaidi kama tukiwa na Serikali ya Tanganyika kama ilivyo Serikali ya Zanzibar,” anasema.

Ulimwengu anasema hawakuanza harakati hizo kwa kujiita G55, jina hilo lilitungwa na Profesa Issa Shivji katika moja ya makala zake zilizohusu kundi hilo na linachokipigania.

“Katika moja ya makala zake (Profesa Shivji), ulifika wakati akatuandika kwa jina la Group 55 na ndipo ilizaliwa G55. Na muda huo tulishafika karibu 60 na jina likaganda na likapendwa, tukawa tunaitwa hivyo, ikaendelea hadi likawa rasmi.

“Mimi nilikuwa Katibu na ndiye niliyekuwa nawasainisha wabunge. Najua kuna wakati tulifika 60 na kuna wakati 45 na zaidi ya hapo,” anasema.

Anasimulia harakati za G55 ya wakati huo zilianzia kwa wabunge wawili, Arcado Ntagazwa na Njelu Kasaka, walipoamua kupeleka barua kwa Spika kutoa ilani kwamba watapeleka muswada bungeni kujadili hoja binafsi ya kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Serikali ya Muungano.

“Sisi tuliona kuna haja ya hoja hiyo kupewa nguvu na wabunge walio wengi, na tukataka tusainishe wabunge na kuzuia uwezekano wa wabunge wawili hao kufanya dili na Serikali, pengine kuteuliwa na hatimaye hoja kupotea,” anasema.

Harakati za kusainisha wabunge, anasema, zikafikisha idadi ya wajumbe 20, wakaenda kwa Spika kutaka hoja hiyo ibadilishwe kutoka kuwa ya wabunge wawili na sasa iwe ya wengi kwa kuwa waliongezeka.

Kuhusu yanayoendelea Chadema, anasema kama ndani ya chama kuna mkondo wa mawazo tofauti na unawahusisha wengi, ni vema ukasikilizwa.

Akizungumzia sababu za jina hilo, Katibu wa G55 ya sasa, Edward Kinabo anasema uamuzi huo umetokana na historia ya G55 ya zamani iliyobebwa na uthubutu wa wabunge wa CCM mwaka 1993 kujitokeza kudai Serikali ya Tanganyika.

“Sisi ndani ya chama chetu (Chadema), katika ajenda ya No Reforms, No Election, ambao ni msimamo wa chama chetu, tumekuja na mawazo tofauti kidogo. Tumeona tusikae kimya, tuthubutu kushauri bila kuogopa, na kwa sababu uthubutu huu hauiachi CCM ipite bila kupingwa,” anasema.

Anasema mpango wa kuzuia uchaguzi unaiweka Chadema katika hatari ya kushindwa kushiriki uchaguzi, kwa kuwa hawaoni kama watafanikiwa kuuzia.

“Kufanya hivyo tunaona kama tunamsusia mbwa bucha, na atakula nyama zote. Tunachotaka ni kupigania mageuzi ya sheria, wakati huohuo tujiandae na uchaguzi,” anasema Kinabo.

Sababu ya pili ya jina la G55, anasema ni kuwa watu wa kwanza waliokutana na kujiona na mawazo yanayofanana walikuwa 55, na ndio vinara na wawakilishi wa awali wa msimamo huo, ingawa kwa sasa wameshafikia zaidi ya watia nia wa ubunge 200.

Related Posts