Ushauri wa Profesa Lipumba kwa Bunge

Dar es Salaam. Wakati kikao cha Bunge la Bajeti kinatarajiwa kuanza kesho Jumanne, Aprili 8, 2025, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, ameshauri kuwa ili kuwatendea haki Watanzania, hotuba zake zijikite kuchambua sababu za kutofanikisha malengo ya Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo.

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025. Ulizinduliwa mwaka 1999 kutokana na hali ya kiuchumi iliyopitiwa na nchi kati ya miaka ya 1980 hadi 1990. Lengo lake lilikuwa ni kuunganisha juhudi za taifa katika kufikia malengo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Msingi wa hoja ya Profesa Lipumba ni kwamba mara nyingi bajeti za Serikali zinaandaliwa kwa kuzingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26), Dira ya Maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2050, Ajenda ya Maendeleo ya Afrika 2063, na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030. Kwa kuwa nchi haijafanikiwa, ni muhimu waeleze.

Akizungumza Dar es Salaam jana kwenye mkutano na vyombo vya habari, Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi, alisema ni lazima tathmini ifanyike kwa kuwa mpango huo ulioanza 2021/22 hadi 2025/2026 ni wa mwisho katika utekelezaji wa Dira ya 2025, wenye lengo la kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kipato cha kati unaotegemea viwanda.

“Kama mchumi nasema kimsingi hatujafanikiwa kujenga uchumi wa viwanda. Mchango wa sekta ya viwanda (manufacturing) katika pato la taifa umepungua kutoka asilimia 9.4 mwaka 2012 na kufikia asilimia 7 mwaka 2023. Ukuaji wa sekta ya viwanda kati ya 2021–2023 ulikuwa asilimia 4.4 tu. Kimsingi Tanzania ya viwanda bado ni ndoto ya mchana,” alisema.

Kulingana na maelezo ya Profesa Lipumba, alisema ili kuwatendea haki Watanzania, hotuba ya Waziri Mkuu ianze kwa kutoa ufafanuzi wa kwa nini malengo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo hayatafikiwa.

“Mawaziri wa sekta pia wajikite katika kuwaeleza Watanzania kuhusu kushindwa kwa Serikali kutekeleza Mpango wa Tatu wa Maendeleo katika sekta zao. Utaratibu wa zamani wa hotuba za Bunge la Bajeti ulianza na hotuba za Waziri wa Mipango na Waziri wa Fedha kueleza hali ya uchumi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo pamoja na mapendekezo ya mapato na matumizi.

“Hivi sasa hotuba hizi hutolewa mwisho katika Bunge la Bajeti. Anayefungua dimba ni Waziri Mkuu ambaye anaeleza utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa ujumla,” alisema.

Profesa Lipumba, aliyewahi kuwa mshauri wa masuala ya uchumi kwa Serikali ya awamu ya pili chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi, alisema lengo kuu la mipango mitatu ya Maendeleo ya Taifa lilikuwa kukuza uchumi na kuubadilisha kuwa uchumi wa kisasa wa viwanda utakaoongeza ajira na kutokomeza umaskini.

Alisema mpango wa tatu ulipanga ukuaji wa uchumi ufikie asilimia 8 kila mwaka, lakini wastani wa ukuaji wa Pato la Taifa kati ya 2021 na 2024 ni asilimia 5.0 kwa mwaka. Ukuaji huo haujarudi kwenye kiwango cha wastani wa asilimia 6.9 ilivyokuwa kabla ya janga la Uviko-19.

“Hali ya umaskini wa kipato ni ya juu. Benki ya Dunia inakadiria kuwa asilimia 45 ya Watanzania (sawa na watu milioni 26.8) wanaishi katika dimbwi la umaskini,” alisema na kuongeza:

“Kwa kutumia kigezo cha umasikini cha Serikali cha mtu mzima anayetumia Sh50,000 kwa mwezi si maskini, asilimia 26.4 sawa na Watanzania (Bara) milioni 16.8 wanaishi katika dimbwi la umaskini. Asilimia 80 ya nguvu kazi ya Tanzania imeajiriwa katika sekta isiyo rasmi yenye kipato duni.”

Alisema mchango wa sekta ya viwanda kwa tafsiri pana inayojumuisha uchimbaji madini, viwanda, umeme, maji safi na maji taka kwenye pato la taifa, ulitarajiwa kufikia asilimia 30 ifikapo 2023. Hata hivyo, mchango huo ni asilimia 16.5 pekee.

“Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yalipangwa kuongezeka hadi Dola za Marekani bilioni 14.8 ifikapo 2025/26. Mpaka kufikia mwaka 2023/24, mauzo ya bidhaa za nje yalikuwa dola bilioni 7.9,” alisema.

Profesa Lipumba alibainisha maeneo ambayo mpango wa tatu unayazingatia, ikiwamo kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ubunifu katika viwanda, kukuza ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo.

“Pia kuhakikisha maendeleo jumuishi na shirikishi kwa jamii yote, kuendeleza mafanikio ya awali katika kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kipato cha kati, kuwekeza katika sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuongeza tija na ushindani wa uchumi.

“Kukuza uwekezaji na biashara kwa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji katika Afrika Mashariki na Kati, kuimarisha sekta binafsi kama mshirika mkuu wa maendeleo, kuongeza mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi, kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi wote hasa wanawake, vijana na makundi maalumu, na kuimarisha utawala bora na usimamizi wa rasilimali,” alisema.

Related Posts