Wachezaji Yanga Princess wapewa siku 15

NYOTA wa Yanga Princess wamepewa likizo ya siku 15 kutembelea familia zao kabla ya kujiunga na kambi Aprili 15 kuendelea na michezo ya Ligi ya Wanawake.

Timu hiyo iko nafasi ya tatu kwenye msimamo na pointi 33, ikicheza mechi 15, ushindi mechi 10, sare tatu na kupoteza mbili.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo alisema kutokana na mapumziko ya ligi, timu hiyo imeamua kutoa wiki mbili za mapumziko kwa nyota hao kuanzia Machi 31 hadi Aprili 15.

Aliongeza, baadhi ya wachezaji pia hawakusheherekea sikukuu na familia zao hiyo pia ni sababu ya kutoa mapumziko kwa timu hiyo inayopambania kumaliza nafasi ya pili.

“Wachezaji wako likizo hadi tarehe 15 watakapoanza maandalizi ya kumaliza ligi, kuna umuhimu mkubwa wa kutoa likizo kwa wachezaji kutokana na wanachokifanya uwanjani miili nayo inahitaji mapumziko,” alisema Kibwana.

Mechi ya mwisho Yanga kucheza ilikuwa Machi 30 kwenye Sikukuu ya Eid, timu hiyo iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya Mlandizi Queens inayoburuza mkiani.

Related Posts