Wahudumu wa afya waonywa lugha chafu kwa wagonjwa Mbeya

Mbeya. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Elizabeth Nyema ametoa angalizo kwa watoa huduma kwenye hospitali za Serikali, vituo vya afya na zahanati kuepuka matumizi ya lugha chafu za kukatisha tamaa  kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma.

Hatua hiyo imetajwa kusababisha malalamiko ya wananchi jambo linalowafanya kuona vituo vya afya sio  kimbilio la kupata huduma bora za afya.

Dk Nyema ambaye ni Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 7,2025 kwenye kikao kazi kilichohusisha waganga wafawidhi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati mkoani hapa.

“Waganga wafawidhi mlioshiriki kikao hiki rejeeni kusimamia nidhamu kwa watoa huduma kwa kuhakikisha wateja wanafurahia na kuwa kimbilio kwa kutambua Serikali ya awamu ya sita chini ya  Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa sekta ya afya hususani upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ,” amesema.

Dk Nyema amesema umefika wakati sasa wataalamu wa kada ya afya kutoa huduma kwa weledi mkubwa na kuachana na matumizi lugha chafu zisizostahili kulingana na kanuni na taratibu na mwongozo wa sheria za utumishi.

“Endapo watabainika hatutoweza kuwavumilia, lazima hatua zichukuliwe ili kurejesha nidhamu ya utendaji kazi, badala yake watoe huduma kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu sehemu za kazi,” amesema Dk Nyema.

Dk Nyema amesema lengo la kikao kazi hicho ni kujadili masuala mbalimbali na kuweka mikakati ya kudhibiti na kukabiliana na magonjwa ya milipuko ukiwamo Mpox, Marburg na kipindupindu.

“Niwaombe wekeni mikakati maalumu sambamba na kushughulikia malalamiko ya wananchi haraka ili kufanya huduma zinazotolewa kuwa  kimbilio la Watanzania,”amesema.

Dk Nyema amesema, Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya  na  kuchochea  tija kubwa katika kuboresha utoaji huduma bora kwa wananchi.

“Masuala mengine ambayo tumejadili  ni pamoja na uboreshwaji wa mifumo ya dawa na vifaa tiba, ulipaji wa madeni katika Bohari ya Dawa (MSD) na utoaji wa stahiki za watumishi kwa wakati, “amesema.

Wakati huohuo, amehimiza waganga wafawidhi kusimamia utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ikamilike kwa wakati na kutoa huduma bora za afya kwa jamii.

Kauli hiyo ya Mganga Mkuu imeungwa mkono na wananchi ambao wameeleza  itakuwa suluhisho la utoaji huduma bora za afya na kusisitiza wananchi washirikishwe ili waweza kufanikisha kuwabaini.

Peter Fredy, mkazi wa Sabasaba jijini hapa amesema kuna  vituo vya afya watoa huduma wamesahau majukumu yao kwa kuwa na lugha za kukatisha tamaa kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma.

“Tunashukuru Serikali kwa kuliona hilo ili kupunguza malalamiko ya wananchi iwekwe mifumo shirikishi ili ya kutoa taarifa kwenye mamlaka husika na si eneo maalumu la kuweka maoni,” amesema Fredy.

Related Posts