Dodoma. Kadiri muda unavyosonga, Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linakaribia ukingoni mwa safari ya uhai wake wa miaka mitano tangu lianze mwaka 2020.
Katika kipindi hiki limekuwa jukwaa la mijadala mikali ya kisera na kufikia uamuzi muhimu wa kitaifa.
Hata hivyo, sambamba na majukumu yake ya kikatiba, kipindi hiki pia kimeshuhudia matukio kadhaa ya ukiukwaji wa taratibu, miiko na kanuni za Bunge kutoka kwa baadhi ya watunga sera hao.
Matukio haya yaliwalazimu viongozi wa Bunge kutumia mamlaka yao kuchukua hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni zilizopo.
Wabunge watatu kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge walipewa adhabu ya kutohudhuria vikao na mikutano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kusema uongo na uchonganishi.
Walioadhibiwa ni wabunge wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM), Luhaga Mpina wa jimbo la Kisema aliyepewa adhabu ya kutohudhuria vikao 15 vya Bunge.
Wengine ni Jerry Silaa wa Ukonga na Josephat Gwajima wa Kawe ambao walisimamishwa kuhudhuria mikutano miwili mfululizo vya Bunge kila mmoja.
Gwajima na Silaa waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge kujibu tuhuma mbalimbali, ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya Bunge.
Taarifa ya Agosti 21, 2021 ya Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Bunge, ilieleza wabunge hao waliitwa mbele ya kamati kwa agizo la Spika wa Bunge, wakati huo akiwa Job Ndugai.
Walitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 4 (1) (a) na (b) ya nyongeza ya nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la Juni 2020 ambayo inaipa mamlaka Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuchunguza mambo yanayohusu maadili ya wabunge yanayopelekwa na Spika.
Gwajima alitakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Agosti 23, 2021 saa saba mchana na Silaa Agosti 24, saa saba kamili mchana.
Sababu zilizowatia hatiani
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Agosti 31, 2021 mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka ambaye ni mbunge wa Tabora Mjini alisema Silaa hakuthibitisha kauli yake kuwa mishahara ya wabunge haikatwi kodi na aliuzwa iwapo mshahara wake unakatwa kodi au haukatwi alisema kuna sehemu inakatwa kodi na kuna sehemu haikatwi kodi.
Mwakasaka alisema kamati ilithibitisha kuwa alikuwa na nia ovu ya kulidharau na kulidhalilisha Bunge na kuchonganisha Bunge, Serikali, uongozi wa Bunge na wananchi.
Aliadhibiwa kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge mfululizo na aliondolewa katika nafasi ya uwakilishi wa Bunge katika Bunge la Afrika (PAP).
Gwajima alikuwa akikabiliwa na tuhuma za kuvunja haki za Bunge, kudharau mamlaka yake na kugonganisha mihimili, akidaiwa kwa nyakati tofauti, Julai 25, 2021, Agosti 8 na Agosti 15, 2021 akiwa katika maeneo ya Ubungo jijini Dar es Salaam, alitoa kauli mbalimbali kuhusu chanjo ya ugonjwa wa Uviko-19.
Alitiwa hatiani na kupewa adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili ya Bunge.
Juni 24, 2024, Bunge lilitoa uamuzi kuhusu Mpina kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuwa alisema uongo kuhusu sakata la utoaji wa vibali na uagizaji sukari nje ya nchi.
Bunge chini ya Spika, DK Tulia Ackson liliazimia aadhibiwe kutohudhuria vikao 15 vya Bunge.