WALIOSHINDWA KUREJESHA MAWASILIANO SOMANGA KUCHUKULIWA HATUA: ULEGA

****

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesisitiza kuwachukulia hatua kali za kinidhamu wataalam kutoka Wakala wa Barabara (TANROADS) 

waliouhusika na uzembe wa kushindwa kurejesha kwa wakati mawasiliano ya barabara kuu ya Dar es Salaam – Lindi eneo la Somanga Mtama Mkoani Lindi

Ulega ameeleza hayo Mkoani Lindi wakati alipofika na kukagua kazi za urejeshaji wa mawasiliano hayo yaliyokatika tarehe 06 Aprili, 2025 na kutoridhishwa na kasi ya urejeshaji wa mawasiliano hayo na kuelekeza wataalam kutoka kwa TANROADS kutoondoka eneo hilo hadi mawasiliano hayo yatakaporejea.

“Nimekagua na nimeona namna kazi inavyoendelea, mimi kama Kiongozi nimeona kuna jambo ambalo bado halijafanyika kisawasawa, uko uzembe uliofanyika, nitachukua hatua kali ili siku zingine yatakapotea mambo ya dharura kama haya yachukuliwe kidharura”, amesema Ulega.

Ulega ametoa salamu za pole kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na Dar es Salaam waliokumbwa na kadhia hiyo na kuwahakikishia kuwa timu ya wataalam iliyopo itafanya kazi haraka iwezekanavyo ili kuruhusu wananchi waliokwama kuendelea na safari zao. 

Halidhalika, ameipongeza timu ya wataalam ya TANROADS Mkoa wa Lindi kwa kuchukua jitihada za dharura mara baada ya tukio hilo kutokea na kusisitiza kuongezwa kwa idadi ya malori ya mawe hadi kufika magari 100 ili yasaidie kwa haraka urejeshaji wa barabara katika eneo hilo.

Akizungumza na wananchi wa Somanga, Ulega ameeleza kuwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameidhinisha zaidi ya Shilingi Bilioni 130 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja yaliyokatika katika Mkoa wa Lindi na kubainisha kuwa hatua za ujenzi wa madaraja matano zinaendelea na yapo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Ameongeza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na katika mwaka mpya wa fedha 2025/2026 itakarabati na kuziba mashimo katika maeneo korofi ya Marendego, Somanga, Njia Nne, Matandu, Ikwriri – Nyamwage – Chumbi ili kurahisisha huduma za usafiri wa abiria na mizigo.

Vilevile, Serikali itaanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara kwa njia nne kuanzia Kongowe – Mbagala Rangi tatu ambapo tayari Mkandarasi ameshapatikana na pia ujenzi wa barabara kuanzia Kongowe hadi Mkuranga itajengwa kwa njia nne ili kupunguza msongamano wa magari uliopo sasa.







 

Related Posts

en English sw Swahili