Wamachinga warudi katikati ya mji Iringa

Iringa. Serikali imeeleza kutoridhishwa na baadhi ya wamachinga kurejea katikati ya mji wa Iringa kinyume na maelekezo ya awali kwamba, waende kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili yao.

Kauli hiyo imetolewa jana Jumamosi Aprili 6, 2025 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe  alipozungumza katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa mkoa, wilaya, Manispaa ya Iringa, pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara na wamachinga.

Kigahe amesema Serikali haiwezi kuvumilia hali ya biashara holela katikati ya miji, kwa kuwa inaleta usumbufu kwa watumiaji wengine wa miundombinu ya jiji.

‎ Kigahe amesema Serikali itachukua hatua kali kwa wale watakaoshindwa kufuata maagizo hayo kwa kufanya biashara maeneo yasiyoruhusiwa huku akiahidi kuboresha mazingira yao.

‎”Serikali itaendelea kufanya juhudi za kuboresha miundombinu katika maeneo rasmi ya biashara ili kufanya mazingira ya biashara kuwa bora na salama kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla,” amesema Waziri Kigahe.

Hata hivyo, baadhi ya wamachinga waliozungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 7, 2025 wamesema wamelazimika kurudi katikati ya mji baada ya biashara zao kutofanya vizuri katika maeneo yaliyopangwa na Serikali.

‎Maeneo ya katikati ya mji ambayo yamejaa wamachinga ni kando ya Soko la Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mashine Tatu, Stendi ya Zamani ya mabasi ya mikoani na eneo la Miyomboni.

‎Wafanyabiashara hao kwa mara ya kwanza waliondolewa Januari 2023 katikati ya mji kutokana na msongamano wa biashara na athari kwa mazingira, jambo hilo lililozua sitofahamu kati yao na mamlaka za Serikali.

“Maeneo kama Mlandege na Lavera ni mbali na makazi ya watu, wateja hawafiki kwa wingi. Biashara zetu zinashuka sana,” amesema Amina Ngando, mmoja wa wamachinga waliorejea kutoka Soko la Mlandege.

Baadhi ya wamachinga wakionekana wamepanga bidhaa zao mbalimbali nje ya maduka ya Wafanyabiashara katika eneo la pembezoni mwa soko kuu la halmashauri ya Manispaa ya Iringa wakiendelea na biashara hali ambayo inapingwa na wafanyabiashara. Picha na Christina Thobias

Amesema katikati ya mji kuna watu wengi na msongamano wa wateja, hivyo ni mahali muafaka kwa biashara ndogo.

Wafanyabiashara waliopo kwenye maduka rasmi nao wamelalamikia hali hiyo, wakidai inawaathiri kwa kupungua kwa wateja.

“Uwepo wa wamachinga nje ya maduka unasababisha wateja wengi kununua bidhaa kwao kabla ya kufika madukani. Inatufanya tukose wateja na uhuru wa kufanya biashara,” amesema Saada, mfanyabiashara kutoka Manispaa ya Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada wameahidi kuhakikisha wamachinga hao wanarudishwa katika maeneo yao rasmi ya biashara kwa utaratibu unaofaa.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara na wamachinga kuhusu kuwataka wamachinga warejee katika maeneo yao rasmi ya kufanyia biashara zao.

‎‎”Niseme tu kuwa kuanzia Jumanne Aprili 8, 2025 viongozi tutaingia barabarani kuhakikisha tunawaondoa wamachinga katika maeneo ambayo si rasmi kwao kwa kufanyia biashara,” amesema James.

Related Posts