Watetezi haki za binadamu wataka mjadala wa kitaifa haki za watoto

Dodoma. Watetezi wa haki za binadamu nchini wameshauri kufanyika kwa mdahalo wa kitaifa kuhusu namna ya kumlinda mtoto kutokana na wingi wa matukio ya ukiukwaji wa haki za kundi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uhalifu iliyotolewa na Jeshi la Polisi, mwaka 2023, waathirika wengi wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni watoto.

Katika mwaka huo, jumla ya waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia waliripotiwa, ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo waliripotiwa waathirika 12,163.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa, amesema hayo leo Jumatatu, Aprili 7, 2025, katika mdahalo wa asasi za kiraia na taasisi zinazosimamia sheria nchini.

Mdahalo huo unaolenga kuimarisha ushirikiano kati yao ili kusukuma mbele ajenda ya haki, sheria, na uwajibikaji wa taasisi nchini.

Ole Ngurumwa amesema watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa ukiukwaji wa haki za binadamu vijijini na kwamba mfumo wa ulinzi wa watoto nchini haujakaa vizuri.

Amesema kwamba, Sheria ya Mtoto inataka kila kata kuwe na Ofisa Ustawi wa Jamii kwa ajili ya kushughulikia masuala yanayohusiana na mtoto.

Mratibu huyo amesema katika tathmini waliyoifanya, kuna uhaba wa asilimia 95 ya maofisa ustawi wa jamii kwenye kata.

Amesema maofisa hao wako katika sehemu za mijini tu, lakini vijijini wako wilayani, hali inayotatiza utekelezaji wa sheria hiyo ya mtoto.

“Migogoro ya watoto iko mingi, ukizingatia pia dawati la polisi haliko kila mahali, lakini pia uelewa ni mdogo. Nadhani tunahitaji kuwa na mjadala wa kitaifa namna gani tunaweza kumlinda mtoto. Mtoto ndiye Taifa la kesho.

“Sensa ya watu na makazi inaonyesha zaidi ya asilimia 40 ni watoto, sasa tusipowalinda tutakuwa na changamoto kubwa sana,” amesema.

Pia, ameiomba Serikali kutunga sera ya kuwalinda watetezi wa haki za binadamu nchini kwa sababu bado kuna vikwazo kwa uwepo wa watu wanaozuia uhuru wa watetezi hao.

 “Sisi tumeshatunga sera mfano ambayo tumeikabidhi kwa Waziri wa Katiba na Sheria. Tunaendelea na mkakati kuona ni namna gani tukaanza kampeni ya sera hiyo, itatusaidia sana angalau watetezi wa haki za binadamu kutambuliwa na kulindwa,” amesema.

Pia, Ole Ngurumwa amesema ukiukwaji wa haki za binadamu unaonekana kwa kiasi kikubwa katika jamii kwa sababu hakuna maandalizi ya kizazi ambacho kinaheshimu, kutambua, na kuishi haki za binadamu. Ameshauri elimu ya haki za binadamu iwepo katika mtaala wa elimu.

Amesema kampeni ya msaada wa kisheria, (Mama Samia Legal Aid) imeonyesha uhitaji mkubwa wa msaada wa kisheria, lakini mashirika yanayotoa misaada ya kisheria na wasaidizi wa kisheria ni wachache hasa vijijini.

“Tumefanya tathmini ya sheria ya msaada wa kisheria, bado ina changamoto nyingi. Tunashauri tufanye maboresho ya sheria hiyo, halafu itoe nafasi ya kuboresha utoaji wa msaada wa kisheria kule vijijini kuwafikia watu wote,” amesema.

Akijibu hoja za THRDC, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema sera ya mfano waliyoandaa kwa ajili ya kuwalinda watetezi wa haki za binadamu ataiwasilisha kwa waziri wake ili kuifanyia kazi.

Kuhusu mabadiliko ya sheria ya mtoto na ya msaada wa kisheria, amesema ni vema mapendekezo yao yakapelekwa Tume ya Kurekebisha Sheria kwa kuwa wao ndiyo wamepewa jukumu la kufanya utafiti kabla ya sheria kutungwa.

 “Tumekuwa tukisisitiza na kushauri mambo tunayopendekeza katika mabadiliko ya sheria tuyapitishe kwenye Tume ya Mabadiliko ya Sheria kwa sababu wale wamepewa mamlaka ya kufanya utafiti kabla ya sheria kutungwa,” amesema.

Sagini amesema tume hiyo imeagizwa kuangalia sheria zote zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko zifanyiwe.

Kuhusu kuwa na mitaala ya elimu ya haki za binadamu, Sagini amesema si kweli kuwa suala la haki za binadamu halizungumzwi shuleni na kuwa malezi tu yamekuwa yakizingatia haki za binadamu.

Kwa upande wa kufanya kazi kwa pamoja wanapokwenda kwenye ngazi za kimataifa, Sagini amesema suala hilo linawagusa kwa kuwa kuna wakati ripoti zinakuwa zikienda katika ngazi hizo za kimataifa bila hata waziri mwenye dhamana kujua.

“Hivi kuna ugomvi gani mkichapa mkamwambia waziri kuwa tumeona haya, kwa hiyo haya ndio yatakwenda ili naye ajiandae, lakini unakuta maandiko kule yameandika habari za Tanzania hadi unashangaa,” amesema.

Amepongeza wazo la kuwa na utaratibu wa kuwa na jukwaa la kushirikishana mambo ambayo yanakwenda katika ngazi za kimataifa kwa pamoja kama nchi.

Hata hivyo, ameonyesha hofu ya kutokubalika kwa wazo hilo na baadhi ya mashirika ya kimataifa kwa kuwaambia kuwa wameshawekwa mfukoni na Serikali kwa sababu wengine wamekuwa wakishangalia kuona mtifuano kati ya Serikali na asasi za kiraia.

Related Posts