‘Wazanzibari endeleeni kudumisha mshikamano’ | Mwananchi

Unguja. Wakati viongozi na watendaji wakitakiwa kumuenzi hayati Abeid Aman Karume kwa kuendeleza maono yake kwa kutenda haki bila ubaguzi, wananchi wametakiwa kudumisha amani, upendo na mshikamano ili kupata maendeleo ya kweli kama alivyotamani mwasisi wa Taifa la Zanzibar.

Dua ya kumbukizi ya miaka 53 ya kifo cha hayati Karume imefanyika leo Aprili 7, 2025 Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kwa viongozi na wananchi wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye yupo Uingereza kwa ziara ya kikazi.

Karume aliuawa Aprili 7, 1972 kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro Shiraz, Kisiwandui, Zanzibar.

Akizungumza kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania Bara, Sheikh Abubakar Zubeir katika dua ya kumuombea Karume, Naibu Kadhi, Sheikh Ally Khamis amesema mbali na jambo hilo la kidini kumuombea dua, lakini ni darasa kwa vizazi vijavyo kuwa na utaratibu wa kuwaombea viongozi waliopigania Taifa hili.

Sheikh Khamis ametumia fursa hiyo kuwataka Wazanzibari kuendelea kuishi kwa umoja, amani na mshikamano kama alivyotaka mwasisi wa Taifa hilo.

“Kiongozi wetu huyu (Karume) alileta amani katika Taifa letu, kwa hiyo katika kumuenzi, mufti mkuu anawataka Wazanzibari kuendelea kuwa wamoja, kuwa na mshikamano, kupendana na kusaidiana ili tupate maendeleo, bila haya nchi yetu haiwezi kuendelea,” amesema Sheikh Khamis.

 “Bila amani hakuna maisha, kwa hiyo hili ni jambo muhimu, tuendelee kulienzi na kulifanya kwa ajili ya vizazi vijavyo maana ni darasa tosha,” amesema.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Chama cha Wananchi (CUF), Abdallah Hamad Hassan amesema kuna haja viongozi kufuata matakwa ya Karume kwa kuwa, hakubagua mtu, alipenda kushirikisha wananchi hata kama ni wa hali ya chini na changamoto alizifanyia kazi bila kujali mtu yupo vipi.

“Karume alikuwa mtu wa watu, alitatua changamoto za watu, awe mkubwa kwa mdogo. Alileta elimu bure, afya watu walitibiwa bure akawapa na wananchi makazi bure, kwa hiyo aliguswa na maisha ya wananchi wanyonge,” amesema Hassan.

“Kwa hiyo, hata sisi na viongozi wengine tunapaswa kutanguliza masilahi ya wananchi, tunaweza kutofautiana kiitikadi na kisiasa, lakini linapokuja suala la wananchi tunapaswa kuwa kitu kimoja,” amesema Hassan.

Pamoja na kujali masilahi ya wananchi, Hassan ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CUF, amewataka viongozi wakuu na chama tawala kuvishirikisha vyama vingine katika kujenga nchi na kuleta maendeleo ya wananchi kwa sababu wanahudumiwa wote, wenye vyama na wasiokuwa na vyama.

“Alama aliyoiweka Karume ni kubwa, bado hatujapata viongozi wa kufanana naye, kwa sababu alisimama imara kuwatetea wanyonge na alifanikiwa katika hilo,” amesema Hassan.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira amesema alimuona Karume akiwa na umri wa miaka 26, mwaka 1971 akiwa mbunge kijana walipokwenda kumtembelea ofisini kwake Zanzibar akiwa na vijana wabunge wenzake Mustafa Nyangai na Joseph Mungai.

Amesema baada ya kuonana naye, aliwapa wosia kwamba, wafanye mambo makubwa kabla hawajafa kwa ajili ya nchi.

“Alituambia maneno yafuatayo, vijana wa Tanzania fanyeni mambo makubwa kabla hamjafa, na mwaka mmoja baadaye tangu alipotuambia hivyo, yeye aliuawa baada ya kuwa amefanya mambo makubwa kwa nchi yake,” amesema Wasira.

“Kwa hiyo alikuwa anatupa wosia tufuate nyayo zake, hili la kwanza, lakini la pili tunamkumbuka Karume kama mpigania uhuru wa Afrika katika nchi yake, lakini kwa ajili ya Afrika, alikuwa akihudhuria mikutano yote ya Pan Africanism iliyokuwa inawaleta pamoja viongozi wapigania uhuru.”

Kuhusu weledi na haki, Wasira amesema viongozi wanajaribu kuleta watu pamoja na ndio ilikuwa falsafa ya Karume aliyotaka maana alifanya mapinduzi ili kuondoa dhuluma iliyokuwa imekithiri. Amesema, aliamini watu wote wawe kitu kimoja na wapewe haki sawa.

Katika msingi huo, Wasira amesema ndiyo maana Karume aliwahi kuunda wizara inaitwa Hali ya Kuweka Wananchi Sawa.

“Kwa hiyo, viongozi tunawajibu wa kufuata nyayo zake za uzalendo, haki na kuwatumikia wananchi kwa usawa bila ubaguzi,” amesema Wasira.

Wasira amesema maendeleo makubwa yanayoonekana Zanzibar mpaka sasa yanatokana na maono yake kwa sababu aliendeleza ilani ya Afro Shiraz iliyotaka watoto wote Wazanzibari wasome bila malipo na watibiwe bila malipo.

Balozi Ali Karume ambaye ni mtoto wa Karume, amesema mwasisi huyo wa Taifa ndio alileta uhuru wa kweli Zanzibar baada ya kupigana na walipata fursa ya kuchagua mkuu wa nchi na mkuu wa Serikali kwa mara ya kwanza kwa kuwa, kabla ya mapinduzi aliachiwa Sultan atawale.

“Mzee Karume alitusaidia sana kwamba tunakuwa na demokrasia mpya, unamchagua Rais wako ndio kiongozi mkuu na unachagua wabunge wawakilishi alieneza hilo,” amesema Balozi Ali.

Mwakilishi wa Konde, Zawadi Nassor amesema maono na mtazamo wa hayati Karume, viongozi wote wanaowajibu kuyaendeleza.

“Viongozi wanapaswa wawe wazalendo, Karume alipambania nchi yake akiwa na kundi la watu wachache, kwa hiyo na sisi tuipambanie nchi yetu kama alivyofanya,” amesema Nassor.

 “Lakini pia alikuwa na hekima na busara, aliweka maono ya kudumisha umoja na mshikamano wa nchi yetu, hata historia inaonyesha aliuawa kwa sababu ya uzalendo wake.”

Naye Haji Ali Ussi, mkazi wa Kwa Haji Tumbo amesema: “Umoja wetu wa Zanzibar umechochewa kwa kiasi kikubwa na mizizi iliyojengwa na hayati Abeid Amani Karume, alikuwa kiongozi mwenye maono makubwa na aliyesimama mstari wa mbele kuijenga Zanzibar moja.”

Amesema Wazanzibari daima wataendelea kumkumbuka kuleta maendeleo ambayo viongozi waliofuatia licha ya kujitahidi kufanya, lakini hawakufikia kiwango chake tena ikizingatiwa alitawala kwa kipindi cha miaka michache kuliko awamu zingine zilizofuatia.

Baadhi ya viongozi wengine wakuu waliohudhuria ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na marais wastaafu wa Zanzibar, Aman Abeid Karume na Dk Ali Mohamed Shein.

Wengine ni wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Tanzania bara na Visiwani, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Maulid na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na wananchi na viongozi wengine wa vyama vya siasa na Serikali.

Related Posts