WIZI WA MILIONI 400 ZA BODABODA ARUSHA, MTUHUMIWA MUHIMU ATIWA MBARONI ,DIWANI WA VITI MAALUM AKAANGWA TAKUKURU KUHUSU MILIONI 120.

 Na Joseph Ngilisho Arusha

Wakati kilio cha muda mrefu cha wizi wa sh, milioni 400 za waendesha pikipiki maarufu bodaboda Mkoa wa Arusha zilizochangwa na wadau mwaka 2017 ,zipo taarifa za uhakika za kushikiliwa kwa mwenyekiti wa zamani wa umoja wa bodaboda Arusha (UBOJA),Maulid Makongoro.

Vyombo vya dola vililazimika kuzinduka usingizini mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Paul Makonda kulivalia njuga suala hilo na kuagiza wahusika watafutwe popote walipo  wakamatwe na waeleze fedha zilipo.

Makongoro na wenzake walilazimika kufutika mkoani Arusha baada ya sekeseke la upotevu wa fedha hizo kuibuliwa na uongozi wa sasa wa waendesha pikipiki ,ambao mara kwa mara wamekuwa wakilalamikia fedha hizo.

Kupitia kikao cha ushauri cha Mkoa ,(RCC), mwenyekiti wa umoja wa bodaboda mkoa wa Arusha UBOMA,Hakim Msemo alitoa malalamiko mazito juu ya upotevu wa fedha hizo zilizokuwa zikichukuliwa kwa nyakati tofauti kupitia matawi ya benki ya NMB .

Katika kikao hicho cha RCC,Mkuu wa Mkoa Makonda aliagiza Mbunge wa Arusha ,Mrisho Gambo ahojiwe baada ya kuwepo kwa mianya inayoonyesha  kuhusika na wizi wa fedha hizo.

Pia Makonda aligiza Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa Takukuru kuwasaka wahusika wa tukio hilo na kuwahoji .

Taarifa zinadai kwamba tayari vyombo vya dola vina mshikilia Makongoro na pia Takukuru imemkamata na kumhoji diwani wa viti maalumu ccm, Saumu Kasimu akihusishwa kupokea  kiasi cha sh, milioni 120 kupitia chama chao hewa cha UWAWAJA zinazodaiwa  kuamuriwa kuchotwa na Gambo ambaye amekuwa akijigamba kufanikisha kupatikana kwa fedha hizo kupitia wadau mbalimbali.

Hatua ya RC Makonda kulivalia njuga na kuamuri upelelezi wa jambo hilo uanze upya kunatoa matumaini  mapya na huenda mwizi akapatikana na fedha zikaokolewa .

Ends .

Related Posts