Maana ya pointi 7 Yanga

YANGA imeichapa Coastal Union bao 1-0 na kuweka gepu la pointi saba dhidi ya Simba inayofuatia kwa ukaribu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara.

Wakati Yanga ikiiacha Simba kwa pointi saba, pia mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara inazo pointi 13 mbele ya Azam iliyopo nafasi ya tatu.

Ushindi huo wa umetokana na bao la Pacome Zouzoua katika dakika ya 35 akimalizia kwa kichwa krosi ya Maxi Nzengelei na kuiimarisha Yanga kileleni ikifikisha pointi 64 baada ya mechi 24 ikibakisha na sita kumaliza msimu huu. Pacome ameboresha rekodi binafsi akifikisha mabao 8 na asisti 8.

POINTI 7 ZINAMAANISHA NINI?

Kabla ya kuingia mwezi huu Aprili, Yanga na Simba zilikuwa zimeshuka dimbani mara 22, huku zikipishana pointi moja kwenye nafasi ya kwanza na ya pili.

Yanga iliyokuwa na ponti 58 kileleni, mwezi huu tayari imecheza mechi mbili dhidi ya Tabora United na Coastal Union huku ikishinda zote na kukusanya pointi sita zilizowafanya kufikisha 64.

Wakati Yanga ikicheza mechi hizo, Simba ina majukumu ya kimataifa, hivyo ratiba yake ya ligi inaonyesha itakuwa na mechi Mei 2 mwaka huu dhidi ya Mashujaa.

Kukaa mwezi mzima bila ya kucheza mechi ya ligi huku akiwa na mashindano mengine ya Kombe la Shirikisho, FA na Muungano, kunaipa mwanya Yanga kukusanya pointi ambazo baadaye zinakuja kuwa presha kwa wapinzani wao itakapoanza kushughulikia viporo vyake.

Yanga ambayo sasa imeiacha Simba pointi saba, bado ina nafasi ya kuongeza gepu hilo na kufika kumi endapo ikiifunga Azam katika mchezo ujao utakaokuwa wa mwisho kwao mwezi huu kabla ya kuendelea mechi tano zilizosalia mwezi Mei ikiwamo Kariakoo Dabi yao iliyoahirishwa huku ikitarajiwa kupangiwa tarehe nyingine.

Kitendo cha Yanga kuendelea kuzichanga vizuri karata katika kukusanya pointi, inamaanisha Simba inatakiwa kuwa makini sana kwani ikiteleza kidogo tu hata kwa kupata sare, itazidi kutoa mwanya kwa Yanga kuukaribia ubingwa wa nne mfululizo.

Ndani ya siku tisa, ratiba inaonyesha Yanga ina michezo mitatu ambayo tayari imecheza na kubakiwa na mmoja.

Baada ya kutoka kuichapa Coastal Union, Alhamisi Yanga itapambana na Azam, kisha itapumzika hadi Aprili 15 kucheza mechi ya robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Stand United, itarudi tena kwenye kipute cha ligi Aprili 20 ugenini dhidi ya Fountain Gate, hivyo kuwa na wigo mpana wa kujiandaa kutoka mechi moja baada ya nyingine.

Endapo Yanga itazifunga Azam na Fountain Gate katika michezo miwili ya kufunga mwezi huu, itafikisha pointi 70, huku Simba ikiendelea kusalia na pointi 57 tofauti ya pointi 13, jambo litakalozidisha presha zaidi kwa kikosi hicho cha Msimbazi kinachosaka ubingwa huo baada ya kuukosa kwa misimu mitatu.

Mtihani wa Simba utakuwa mwezi Mei kwani timu hiyo italazimika kucheza mechi nne mfululizo ndani ya siku 10 huku Yanga ikiwa inawasikilizia tu kwani wao mechi ijayo ya ligi baada ya Aprili 20, itakuwa Mei 13 dhidi ya Namungo.

Related Posts