*****
Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya
Mwanga Lembrus Mchome amesema amemuomba Msajili wa vyama vya siasa kutengua
maamuzi ya Baraza Kuu la chama hicho yaliyofanyika kwenye kikao cha Baraza Kuu
kilichofanyika Januari 22, 2025 kwa kuwa kilikuwa na kasoro.
Akizungumza na wanahabari leo April 8, Mchome amesema Baraza
kuu halikuwa halali kwani akidi haikutimia lakini pia ndani yake kulikuwemo na
watu ambao sio wajumbe halali wa Baraza kuu kwa mujibu wa katiba ya CHADEMA.
Mchome ameeleza kuwa amemuomba Msajili abatilishe vikao
vyote vya kamati kuu viliyokaliwa kuanzia baada ya tarehe 22 kwani wajumbe wake
akiwemo Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu Bara na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar
uteuzi wao sio halali.
Aidha ameongeza kuwa amepokea barua leo kutoka kwa Msajili
wa Vyama Vyama Siasa ikimjibu maombi yake kuwa Msajili amemtaka Katibu Mkuu wa
CHADEMA John Mnyika kujibu malalamiko ya Mchome ndani ya siku tatu.
Katika hatua nyingine Mchome amesema anashangazwa na namna
ambavyo Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu amekuwa akijibu wanachama
wanaotoa maoni tofauti kuwa hatumii lugha nzuri wala namna nzuri.
Mchome amemtolea mfano Mwenyekiti aliyepita Freeman Mbowe kuwa alikuwa kiongozi
ambaye alipokea maoni hata mbadala bila kuchukulia kwa ubaya “tulikuwa na
Kiongozi aliyepita Mzee wetu Freeman Mbowe alikubali kupokea yote, alikubali
kukosolewa aliyapokea yote”