Dar es Salaam. Wakati utafiti ukibaini uwepo wa masalia ya dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV) kwenye nyama na damu za kuku wa kisasa, nguruwe na vyakula vya mifugo, vyama vya wafugaji vimeitaka Serikali kuchukua hatua, huku wataalamu wa dawa wakitoa angalizo.
Utafiti huo umefanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) mwaka 2024 kwenye wilaya tisa nchini na kuchapishwa Machi 28, 2025 katika jarida la kimataifa la Springeropen, ukihusisha sampuli 196.
Sampuli 131 sawa na asilimia 66.8 zilibainika kuwa na ARV aina ya Lamivudine. Masalia ya dawa hiyo yalionekana kwenye sampuli za nyama na damu kwa kiwango cha (7.58mg/kg), huku kukiwa na kiwango kidogo cha 0.001 mg/kg kwenye chakula cha kuku wa kisasa.
Kwa dawa aina ya Nevirapine na Efavirenz hazikubainika kwenye sampuli zilizokusanywa wala kwenye maji waliyonyweshwa mifugo hao.
Kwa mujibu wa utafiti hao, wakulima wanaoishi na VVU huenda wanatumia ARV wanazopewa kuwapa wanyama, jambo ambalo linaweza kusababisha kutofuata maelekezo ya matumizi yake ipasavyo na kuibuka kwa usugu wa dawa.
Mbali na matatizo ya moja kwa moja ya afya ya binadamu na wanyama, mabaki hayo kwenye chakula cha wanyama na kinyesi, yanaweza kusababisha uchafuzi wa mazingira na kuleta madhara kadhaa.
Ushauri uliotolewa na watafiti hao ni kupiga marufuku matumizi ya ARV za binadamu kwa kuwapa wanyama.
Pia ifanyike tafiti nyingine kubaini sababu za kijamii na zingine zinazosababisha matumizi ya ARV kwa wanyama na kutafuta suluhisho la kudumu.
Kutokana na matokeo hayo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafugaji Nguruwe Tanzania (Tapifa), Doreen Maro amesema wameliona chapisho la utafiti huo na wamewasiliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kufuatilia ukweli wake ili hatua zichukuliwe.
“Kama ni kweli wapo wanaotumia dawa hizo nawaomba waache, upo utaratibu mzuri wa ufugaji na unapata matokeo. Kwanza ni kuwa na mbegu bora, chakula bora na usimamizi mzuri unampata nguruwe mwenye uzito mkubwa, hakuna njia nyingine tofauti ya kupata matokeo kwenye ufugaji,” amesema.
Ameonya kama wapo wafugaji wanaotumia dawa ambazo haziruhusiwi waache mara moja, kwani wanaisababishia jamii madhara mengine ya kiafya.
Doreen amesisitiza Serikali ikibaini ukweli, hatua kali zichukuliwe ili iwe fundisho kwa watu wachache wanaotaka kuharibu soko la bidhaa za nyama nchini.
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT), Mgembe Nkonosenema naye amesema hatua za haraka zichukuliwe na Wizara ya Mifugo na Wizara ya Afya kunusuru Watanzania wasipate madhara zaidi.
“Hatua za haraka zinahitajika, hili litaleta athari mbaya kwa wafugaji wengine soko likiharibiwa na watu wachache, kama ina madhara kwa watumiaji wa nyama, maziwa na bidhaa zingine zitokanazo na wanyama, udhibiti ufanyike kwa haraka,” amesema.
Amesema wafugaji nchini wanaweza kutumia mbinu zisizofaa kuharakisha kipato, kwa kunenepesha wanyama ili wauze kwa haraka kinyume cha dunia ya leo yenye kuhitaji vitu vya asili ambavyo havijatumia kemikali.
“Nimekuwa muumini wa uzalishaji ambao hauchanganyi aina ya kemikali. Kwenye soko la leo hatuwezi kushindana kukiwa na madhaifu lazima tuwe vizuri. Tanzania ni nchi yenye idadi kubwa ya mifugo na wauzaji mazao hayo kwa kiwango kikubwa. Wanaotuzunguka kwa matumizi ya ARV ni kitu kibaya kinachoweza kuathiri soko,” amesema.
Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST), Fadhili Hezekiah amesema wamesoma chapisho la utafiti huo kwamba masalia ya dawa yamekutwa zaidi kwenye nyama, kuliko kwenye chakula, hivyo imewapa maswali.
“Wataalamu wa dawa tumejiuliza wingi wa masalia ya dawa kwenye nyama na damu umetokana na chakula au kuna njia zingine? Kupata masalia kwenye mazao yatokanayo na wanyama ni ishara kwamba imetumika kwao kama dawa au matumizi mengine ambayo hayakuelezwa.
“Wasiwasi wetu kama kuna miongozo inayohusu uwepo wa dawa hizi kwenye vyakula au kuonekana katika miili ya hawa wanyama, basi ni makosa kufanya hivyo na wanyama hawa wanaliwa,” amesema.
Hezekiah amesema bahati mbaya utafiti haujaonyesha ni kwa kiwango gani cha dawa kilionekana baada ya nyama za kuku wa kisasa na nguruwe kupitia mchakato wa kuandaliwa kabla ya kuliwa na binadamu, hivyo eneo hilo linahitaji utafiti zaidi.
Amesema iwapo viwango vya masalia ya dawa vitaonekana ni vilevile, ni hatari kwani ni sawasawa na mtu kumeza dawa kwa kiwango kidogo-kidogo wakati hazihitaji.
Alipoulizwa na Mwananchi nini kifanyike, amesema ni muhimu kujiridhisha na matumizi ya dawa husika yalilenga kufanya nini, na iwapo ni sahihi kukuza mazao ya nyama kwa muda mfupi, uchunguzi wa vyakula wanavyotumia na namna ya kuwakuza.
Mtaalamu wa dawa za mifugo, Julenda Nassor amesema matumizi ya dawa za binadamu kwa wanyama hayashauriwi na ni hatari, kwani ni njia ya kutengeneza usugu wa dawa mwilini.
“Ukiona hakuna matokeo kwenye mifugo yako, wasiliana na wataalamu wa mifugo tukushauri nini unapaswa ufanye, dawa gani utumie isiyo na madhara kwa binadamu.
“Ukichukua ARV ukaenda kutumia kuwalisha mifugo, maana yake unalisha watu dawa hiyo na wewe unapaswa kuchukuliwa hatua kama unashiriki kuua watu,” amesema Dk Nassor.
Daktari wa binadamu, Rajabu Mlaluko amesema utafiti uliofanyika ni wa kitaalamu na umeonyesha uhalisia uliopo kwenye jamii.
Amesema unaonyesha wafugaji wengi si waaminifu, hali ambayo ni hatari kwa afya za walaji, kwani inaweza kuwa chanzo cha VVU kujenga usugu dhidi ya dawa na kutofanya kazi kwa wagonjwa.
“Hii ni hatari, kwa kipindi hiki ambacho dunia inapambana kudhibiti usugu wa dawa zikiwamo antibiotiki, Wizara ya Afya na Wizara ya Mifugo zijikite kufuatilia kwa ukaribu matukio hayo ya matumizi ya ARV kwa mifugo kama nguruwe na kuku,” amesema.
Wakati suala la usugu wa dawa likitajwa, matokeo ya utafiti mwingine wa Muhas yaliyotolewa Septemba 2024 yalionyesha asilimia 5.8 ya watu wanaoishi na VVU na wanaotumia dawa, wanakabiliwa na tatizo la usugu wa vimelea dhidi ya dawa za ARV.
Utafiti huo ulifanyika mwaka 2020 katika mikoa 22 ya Tanzania Bara, ikiwamo Songwe, Mbeya, Iringa na Njombe.
Utafiti mwingine uliofanywa katika mikoa 19 nchini mwaka 2019 na Shirika lisilo la kiserikali la Management Development for Health (MDH) na Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa Marekani (CDC) ulionyesha ARV zimejenga usugu kwa asilimia 27.5 kwa kina mama waliogundulika na maambukizi ya VVU wakati wa ujauzito, ambao hawajaanza kutumia dawa na asilimia 79.2 kwa wale ambao tayari walikuwa kwenye matumizi ya ARV.
Kwa mujibu wa wataalamu virusi vya Ukimwi vinapojenga usugu dhidi ya ARV, maana yake dawa hizo hazitaweza tena kupambana hivyo kuvizuia kuendelea kuzaliana na hivyo kinga za mgonjwa (CD4) kushuka, na ndipo mwathirika anaanza kupata magonjwa nyemelezi, yaani Ukimwi.