LICHA ya Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL) kuendeshwa bila kuwa na udhamini, lakini imeonyesha kuwa ndio inayoongoza kwa ubora na kuvutia mastaa kutoka sehemu mbalimbali wanaokuja kuichezea.
Ubora wa ligi hiyo unatokana na uwezo wa wachezaji wanaocheza pamoja na ushindani wa timu shiriki ambao umefanya kutoka mikoa mingine na nje ya nchi ili kuja kucheza mashindano hayo.
Baadhi ya wachezaji waliovutiwa na ligi hiyo kutoka Dodoma ni Brian Mramba, Yunzu Maige na Roma Romanus wanaoichezea Savio na baada ya mchezo hurudi Dodoma.
Upande wachezaji wa kigeni wapo kina Spocian Ngoma, Joseph Kamamba kutoka Zambia, Chary Kesseng (Cameroun) na Zadock Emanuel (Kenya) waliochezea Srelio ambapo wako katika nchi zao wakisubiri kuitwa kuichezea timu hiyo.
Ubora wa ligi hiyo pia umewavutia wachezaji kutoka DR Congo kina Marcus Tshi, Emanuel Mulumba na DanĀ Mwendela walioichezea Miyasi katika mashindano ya karibuni ya maandalizi kwa ajili ya BDL ambayo yalipewa jina la Ramadhani Star League.
Wachezaji hao waliopo nchini wameonyesha dalili ya kucheza Ligi ya Kikapu mkoani humo msimu ujao wakijifua katika maeneo tofauti.
Kwa upande wa wanawake mastaa kutoka Dodoma waliopo ni Tumwagile Joshua, Jesca Lenga na Nasra Bakari kutoka Dodoma ambao wamekuwa wakichezea DB Troncatti na baada ya mechi hurudi mkoani humo.