Dar es Salaam. Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kimeibeba ajenda ya uchaguzi mkuu mwaka huu ikieleza kila hoja inayopigiwa kelele na pande mbili zinazokinzana kuhusu uchaguzi huo ina mantiki.
TLS imekwenda mbali zaidi na kueleza kuwakutanisha wadau wote wa uchaguzi ili kuwa na makubaliano ya pamoja, kabla ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 9, 2025 wakati akitangaza mkutano mkuu wa TLS utakaofanyika Mei jijini Arusha, rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amesema kipaumbele cha chama hicho katika mkutano mkuu wa mwaka huu itakuwa ni ajenda ya uchaguzi mkuu.
“Sote tunafahamu mwaka huu ni wa uchaguzi, ukiondoa kusudio la mkutano mkuu wa TLS, kipaumbele kitakuwa ni masuala yanayohusiana na sheria na uchaguzi,” amesema Mwabukusi.
Mwabukusi akigusia sintofahamu inayoendelea hasa baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuja na kampeni ya ‘No Reforms No Election’ (hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) huku upande mwingine ukitaka uchaguzi, amesema hoja za pande zote mbili zina mantiki.
“Tunaelewa kuna changamoto ya uchaguzi, sababu kuna watu wameshatengeneza position (upande), kuna wengine wanasema uchaguzi lazima ufanyike na wengine wanasema No Reforms, No Election.
“Kila hoja inayopigiwa kelele ina mantiki, anayesema uchaguzi ufanyike yuko sahihi kwani kwa mujibu wa Katiba kila baada ya miaka mitano tunafanya uchaguzi.”
“Anayesema no reforms, no election naye yupo sahihi kwa sababu hakuna Mtanzania ambaye hakuona kilichotokea mwaka 2019 (kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa) na mwaka 2020 (kwenye uchaguzi mkuu),” amesema.
Amesema katika pande mbili zinazokinzana kuhusu uchaguzi mkuu, jukumu lao TLS sio kuchochea bali ni kutafuta majawabu, ambayo amesisitiza yatapatikana kwa kukaa mezani na pande zote ili kukubaliana na kupata majawabu.
“Mnaweza kuwa na makubaliano yakawa mazuri kuliko sheria na katiba, tunaamini kura zinatakiwa zichague mtu? hivi ndivyo vitu tunatakiwa tuvizungumze.
“Lazima turudi mezani tujue wapi tunakosea na twende vipi, kwani hizi pande mbili kila mmoja ana sababu zake na sababu zake zilizo sawa,” amesisitiza.
Amesema katika masuala ya msingi yanayolihusu Taifa, asitokee mtu wa kusema muda hautoshi. Kwani Taifa ni muhimu kuliko kitu chochote.
Mwabukusi amedai, katika uchaguzi huu, vyama vya siasa na Serikali vielewe tu kwamba hakutakuwa na mbuzi kafara akibainisha TLS inasimama upande wa umma, bila kuogopa mtu wala cheo kwani ukiwa mwanasiasa hiyo ni dhamana tu umepewa.
“Hatua ya uchaguzi si ya kivita ni ya sera, karatasi za kupigia kura, masanduku ya kura na watu kujinadi,” amesema.
Amesema muda uliopo unatosha kupata majawabu na wote kwenda kwenye uchaguzi Oktoba 2025 kwa kufanya mabadiliko madogo yanayohitajika, akieleza kwa kufanya mabadiliko hayo angalau kutaleta usawa.
“Tunaweza kukubaliana ni mambo gani ya msingi, mfano wa mambo hayo ni msimamizi kwenye kituo, kwa nini alazimishwe akaapishwe kwa mkurugenzi wakati hasimamii kura zako,” amehoji Mwabukusi na kufafanua hoja hiyo kwamba.
“Kila mtu aapishe mtu wake, sababu yeye ndiye analinda siri zako sio akaape kwa mkurugenzi. Jambo jingine la kukubaliana ni kwa nini ukate mgombea?, kuna zile sifa zimetajwa kisheria sawa, lakini mtu kaandika K ndogo badala ya kubwa unamkata?.
“Kwa nini kimewekwa kifungu msimamizi awe mtumishi wa umma? Pia suala la chaguzi zote kupingwa mahakamani linawezeka, hayo ni machache kati ya mengi mbayo yanawezekana tukakubaliana ili sote twende kwenye uchaguzi,” amesema.
Akizungumzia kuhusu mkutano mkuu wa TLS ambao mwaka huu utafanyika Mei 8-10, kwenye ukumbi wa mikutano wa AICC jijini Arusha, Mwabukusi amesema utawakutanisha wanachama zaidi ya 3,000 kutoka kote nchini.
Amesema wanatarajia makamu wa Rais, Dk Philip Mpango kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mkutano huo.
“Tunawaomba wadau, marafiki wa TLS na taasisi na mashirika mbalimbali yajitokeze kuudhamini mkutano huu,” amesema Mwabukusi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TLS, Mariam Othman amesema mkutano huo utatanguliwa na semina na warsha mbalimbali kuanzia Mei 5 hadi 7, kabla ya kufunguliwa kwa mkutano mkuu (AGM) Mei 8 na kuhitimishwa Mei 10.
Kwa mujibu wa Mariam, mkutano mkuu wa TLS mwaka huu una kauli mbiu ya uchaguzi na utawala wa sheria.
Amesema kabla ya kuanza mkutano mkuu, Mei 7 jioni jijini Arusha kutafanyika chaguzi za kikanda za TLS.
“Kama mnavyojua Baraza la uongozi litakaa madarakani hadi 2027, lakini viongozi wa kikanda wanafanya uchaguzi jioni ya Mei 7, jijini Arusha,” amesema.
Kwa mujibu wa Mariam, Aprili 11 hadi 23 mwaka huu pia kutafanyika uchaguzi wa TLS ngazi ya mikoa.
“Mikoa yetu 21 ya TLS itafanya uchaguzi na viongozi watakaopatikana wataapishwa Mei 10 kwenye mkutano mkuu,” amesema.