PURA yawanoa waandishi, wahariri masuala ya mafuta, gesi asilia

Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imetoa mafunzo ya siku moja kwa waandishi na wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, kwa lengo la kuwaongezea uelewa kuhusu masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Mafunzo hayo yamefanyika Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na waandishi na wahariri wa habari kumi na tano (15) kutoka vyombo vya habari vya umma na binafsi hapa nchini.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA Bw. Shigela Malosha amesema kuwa waandishi na wahariri wa habari ni nguzo muhimu katika kuhabarisha na kuelimisha umma, hivyo ni muhimu kwa mamlaka kuwajengea uwezo katika maeneo mbalimbali ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

“Kwa kutambua umuhimu wa kada ya habari katika kuelimisha umma, PURA imekuwa ikiendesha mafunzo kwa kundi hili kwa lengo la kuwajengea uwezo katika masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini” alieleza Shigela.

Pamoja na mafunzo, Shigela alieleza kuwa, PURA pia huwaandalia wadau hao ziara za kikazi katika maeneo ambayo gesi asilia inazalishwa na kuchakatwa ili kutoa fursa ya kujionea uhalisia wa shughuli hizo zinavyotekelezwa.

Alieleza kuwa PURA huendesha mafunzo hayo mara kwa mara ili kutoa fursa kwa waandishi na wahariri wengi kushiriki.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Mwandamizi kutoka Idara ya Habari Maelezo, Bi. Grace Semfuko ambaye alishiriki mafunzo hayo alisema kuwa elimu ya mafuta na gesi asilia iliyotolewa imemfanya kuelewa masuala hayo kwa kina na itamwezesha kuandaa taarifa bora zaidi za sekta hii muhimu katika uchumi.

“Masuala mengi ya mkondo wa juu wa petroli yamekaa kitaalamu sana na wakati mwingine utoaji wa taarifa kwa lugha rahisi ni changamoto. Mafunzo tuliyopatiwa siku ya leo yametuwezesha kuelewa masuala haya kwa mapana. Uelewa tulioupata utatusaidia sana wakati wa kutekeleza majukumu yetu ya kuhabarisha umma” alieleza Bi. Grace.

Naye Bw. Idd Uwesu kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Sauti Amerika (VOA) aliishukuru PURA kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa mada zilizowasilishwa zimeongeza mawanda ya kile walichokuwa wakikifahamu na pia wamepata kujifunza mengine mengi zaidi ambayo hawakuwa wanayafahamu hapo awali.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA Bw. Shigela Malosha (katikati walioketi) katika picha ya pamoja na waandishi wa habari na wahariri walioshiriki mafunzo yaliyoratibiwa na PURA. Pichani pia kuna baadhi ya watumishi na aanagezi kutoka PURA.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Bw. Shigela Malosha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi na wahariri wa habari yaliyofanyika Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao katika masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Mhandisi Ndau Ndau kutoka PURA akiwasilisha mada kuhusu historia ya utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini wakati wakati wa mafunzo kwa waandishi na wahariri wa habari  yaliyofanyika Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao kuhusu sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Bw. Shigela Malosha wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi na wahariri wa habari yaliyofanyika Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza uelewa wa wadau hao katika masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini

.

Mwanasheria Mwandamizi kutoka PURA, Bw. Abbas Kisuju akiwasilisha mada kuhusu duru ya tano ya kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini wakati wa mafunzo kwa waandishi na wahariri wa habari yaliyofanyika Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam. Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na PURA yalilenga kuongeza uelewa wa wadau hao katika masuala ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Related Posts