CCM YATANGAZA MCHAKATO WA KUCHUKUA FOMU KWA WATIA NIA KUANZA RASMI

By Ngilisho Tv

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimepuliza kipyenga kwa wanachama wake wanaotaka kuomba kuteuliwa katika nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani,kikiwaelekeza utaratibu na mahali pa kuchukua fomu.

Taarifa iliyotolewa Aprili 10,2025 na Katibu Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi,Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla, imeeleza kuwa mchakato huo ni wa ndani ya chama na utaanza rasmi Mei mosi, 2025.

Imefafanua kuwa mchakato huo unahusisha uteuzi wa wagombea nafasi za Ubunge, Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na Udiwani, kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, ambao utaanza rasmi tarehe Mei mosi, 2025 saa 2:00 asubuhi hadi saa 10: 00 jioni kwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu za maombi ya kuteuliwa kugombea nafasi hizo. 

“Utaratibu wa kuchukua na kurejesha fomu za maombi utakuwa kama ifuatavyo: anaogombea nafasi ya Ubunge au Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa Wilaya husika.

“Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi, kupitia kundi la UWT pamoja na makundi maalumu (NGOS, WA?wafanyakazi, Wasomi na Walemavu) watachukua fomu na kurudisha kwa Katibu wa UWT wa Mkoa unaohusika.

“Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia jumuiya ya UVCCM watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UVCCM Mkoa unaohusika.

“Wanaogombea nafasi za Viti Maalumu vya wanawake katika Bunge au Baraza la Wawakilishi kupitia Jumuiya ya Wazazi watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa Wazazi Mkoa unaohusika.

“Waanaogombea nafasi ya Diwani wa Kata (Bara) au Wadi (Zanzibar) watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa CCM wa Kata/Wadi inayohusika.

“Wanaogombea nafasi ya Udiwani Viti Maalumu vya Wanawake watachukua na kurudisha fomu kwa Katibu wa UWT wa Wilaya inayohusika.”

Related Posts