Katikati mwenye shati ya Bluu ni Mhandisi Isaack Mgeni,Mkurugenzi wa mamlaka ya Maji mjini Chato(Chawassa).
Na Daniel Limbe,Chato
ZAIDI ya wakazi 100,000 wilayani Chato mkoani Geita,wanatarajia kunufaika na mradi mkubwa wa maji safi na salama kabla ya sikukuu za Krismas na mwaka mpya 2026.
Hatua hiyo inatajwa kuwa Mapinduzi makubwa ya kimaendeleo ambayo yametekelezwa na serikali ya awamu wa sita chini ya Utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akiwa katika ukaguzi wa mradi huo ambao utekekezaji wake ulianza Aprili 14, 2023 kwa gharama ya dola za marekani milioni 16.49, Mkuu wa wilaya ya Chato Louis Bura, mbali na kumpongeza Rais Samia kwa uthubutu wake wa kumtua mama ndogo kichwani, amesema upatikanaji wa huduma hiyo utasaidia kuinua uchumi na kuchochea maendeleo ya wananchi.
Amesema kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo,imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo ambao tayali umewanufaisha wananchi wa mji wa Chato kwa aslimia 67 na kwamba inatarajiwa kufikia Desemba 10,2025 zaidi ya aslimia 100 ya wananchi hao watanufaika kwa kupata huduma ya maji safi na salama majumbani mwao.
Aidha Bura, ametoa maelekezo kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Chato (Chawassa) kuhakikisha inawafikia baadhi ya wananchi ambao wanahudumiwa na mfuko wa kaya maskini ( Tasaf) ili kuwa miongoni mwa wanufaika 500 wanaotarajiwa kupata msamaha wa malipo ya kuvuta maji ikiwa ni kurejesha shukrani kwa jamii inayozunguka maeneo ya mradi huo.
Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo,Isaack Mgeni,amesema mradi huo utahudumia watu zaidi ya 100,000 katika hatua ya kwanza na kwamba upanuzi wake utaendelea kwa mji wa Bwanga na Muganza ili kuongeza wigo wa wananchi kunufaika na huduma hiyo muhimu.
Katika mradi huo mkubwa ambao unatekelezwa katika miji 28 nchini ikiwemo wilaya ya Chato mkoani Geita,umehusisha ujenzi wa tenki kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi maji takribani lita milioni 3,ujenzi wa mtandao wa maji km 34.18,ujenzi wa bomba kuu la kusafirisha maji km 17, ujenzi wa choteo la maji lenye uwezo wa kufyonza lita 11,000 kwa siku pamoja na ujenzi wa mtambo wa kutibu maji wenye uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa siku.
“Mpaka sasa ujenzi wa tenki hilo umefikia aslimia 95,ujenzi wa mtandao wa maji km 5, bomba kuu la kusafirisha maji km 7, choteo la maji aslimia 20 na mtambo wa kutibu maji aslimia 25,” amesema
“Kadhalika utekelezaji wa mradi huu umefikia aslimia 41 na mkandarasi anaendelea na kazi ya kulaza mabomba,ukamilishaji wa tenki na uchimbaji wa msingi eneo la chanzo cha maji hayo kilichopo kwenye kijiji cha Buzirayombo” amesema Mhandisi Mgeni.
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Mandia Kihiyo, ametumia fursa hiyo kumpongeza rais Samia kwa kazi kubwa ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo ikiwa ni pamoja na kurejesha amani na utulivu katika ndoa za wananchi hao kutokana na uwepo wa migogoro ya wanawake kutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji safi.
Amesema halmashauri hiyo inatarajia kuondokana kabisa na changamoto ya uhaba wa maji baada ya Mradi huo kukamilika kwa aslimia 100 huku maeneo mengine ya vijijini yakihudumiwa na Ruwasa na kwamba hatua hiyo itasaidia kuimalisha afya za jamii na kupunguza gharama za kutibu magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji machafu.
Kwa upande wake,Msimamizi na Mhandisi mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya Wapcos Ltd, Riddhiman Dey, ameipongeza serikali kwa usimamizi wake madhubuti ikiwa ni pamoja na kutoa malipo ya Mradi huo kwa wakati jambo ambalo limesaidia kazi kuendelea kwa kasi kubwa pasipo kukwama.
Hata hivyo ameahidi kuendelea na usimamizi wa kazi hiyo kwa ubora wa hali ya juu, na kwamba ni matarajio yake kuwa mradi utakamilika kabla au baada ya muda uliopangwa katika mkataba wa ujenzi.
Kulia ni mkuu wa wilaya ya Chato,Louis Bura na katikati mwenye shati ya Bluu ni Mhandisi Isaack Mgeni,akitoa ufafanuzi.
Katibu tawala wa wilaya ya Chato,Thomas Dimme,akiwa katika ukaguzi wa mradi wa maji wa miji 28 wilayani hapa.
Mwisho