Dodoma. Kwa mara nyingine Serikali imeshindwa kusema ni lini itaanza ujenzi wa Daraja la Godegode katika Wilaya ya Mpwapwa ambalo ni kilio cha muda mrefu.
Daraja hilo ambalo linaunganisha majimbo ya Mpwapwa, Kibakwe na Kilosa na limekuwa ni tatizo la miaka mingi na wananchi wamekuwa wakikosa mawasiliano kipindi cha mvua.
Mbunge wa Mpwapwa, George Malima ameuliza swali leo Ijumaa Aprili 11, 2025 ni lini Serikali itaanza ujenzi wa daraja hilo ikizingatiwa ni tatizo la muda mrefu na mkandarasi ameshapatikana.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali imekamilisha taratibu za manunuzi ya mkandarasi wa ujenzi wa daraja hilo.
“Kwa sasa, Serikali iko katika hatua ya kukamilisha taratibu za kusaini mkataba wa ujenzi na mara baada ya mkataba kusainiwa kazi za ujenzi zitaanza,” amesema Naibu Waziri.
Kwa nyakati tofauti wabunge waliopitia jimbo hilo, George Lubeleje, Gregory Teu (marehemu) na sasa Malima wamekuwa wakilizungumzia daraja hilo na kila mmoja kwa wakati wake hueleza linavyobeba kura zake.
Katika kipindi cha uongozi Lubeleje, mara kadhaa alisema kinachomponza hata kukosa kura za wananchi ni Daraja la Godegode ambalo limebeba uchumi mkubwa wa Wilaya ya Mpwapwa.