DKT.YONAZI AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MTAKWIMU MKUU WA SERIKALI, DKT. MSENGWA

Na.Mwandishi Wetu – Dodoma

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amekutana na kufanya mazungumzo na Mtakwimu Mkuu Mpya wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa, aliyefika kujitambulisha baada ya kuteuliwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivi karibuni kuchukua nafasi ya aliyekuwa Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Albina Chuwa, ambaye amestaafu rasmi utumishi wa Umma.

Kikao hicho kimefanyika tarehe 11 Aprili, 2025 katika Ofisi ya Waziri Mkuu iliyopo mtaa wa Reli jijini Dodoma.

Dkt. Yonazi amempongeza kwa uteuzi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano baina ya ofisi hizo huku akiwashukuru kwa kazi nzuri zinayofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu nchini.

“Ofisi hii inayoshughulikia masuala ya Takwimu ni muhimu sana katika nchi yetu, niwasihi mwendelee kuchapa kazi na kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha Serikali inayafikia malengo yake nasi tutaendelea kushirikiana kuhakikisha tunaliletea Taifa maendeleo,” alisema Dkt.Yonazi

Akieleza namna Ofisi yake ilivyojipanga kutekeleza majukumu,Mtakwimu Mkuu wa Serikali Dkt. Amina Msengwa amesema wapo tayari kufanya kazi huku wakihakikisha umma unapata taarifa zote muhimu zinazotakiwa kupitia program na mikakati iliyopo kwa kasi inayotakiwa.

Katika kikao hicho Mtakwimu Mkuu wa Serikali ameongozana na baadhi ya Watendaji wa Ofisi yake akiwemo Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi Bw. Daniel Masolwa,Meneja wa Takwimu za Ajira, Bei na  Mratibu wa mpango  wa TSMP  II Bw. James Mbongo, pamoja na Mratibu wa masuala ya Sensa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Adela Mpina.

Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa akizungumza wakati wa kikao na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (aliyekaa kulia) alipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi akikagua baadhi ya nyaraka alizokabidhiwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa ofisi kwake Jijini Dodoma.


Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonazi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na ugeni kutoka Ofisi ya Takwimu, ulioongozwa na Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dkt. Amina Msengwa (wa pili kutoka kushoto).

(PICHA  ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)

=MWISHO=

Related Posts