Dodoma. Katika kuwezesha shule kuingiza mapato na wanafunzi kupata lishe, Mkoa wa Dodoma umeanza programu maalumu ya kupanda miti ya matunda 500 kwa kila shule.
Ili kufanikisha hilo, kila halmashauri imetenga bajeti isiyopungua Sh10 milioni kwenye mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya upandaji na utunzaji wa miti.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Kaspar Mmuya ameyasema hayo leo Ijumaa Aprili 11, 2025 wakati shughuli ya upandaji wa miti na ugawaji wa vitabu vya elimu ya fedha katika Shule ya Msingi ya Mtumba.
Jumla ya miti 500, kati ya 2,000 iliyotolewa na Chama cha Wanawake katika Sekta ya Fedha (Tawifa) imepandwa kwenye shule hiyo.
“Kwa kupanda miti ya matunda tunatarajia kiwe ni chanzo kikubwa cha familia na mtu mmoja mmoja kukuza kipato. Tumeanza na shule tano ikiwemo Shule hii ya Mtumba,” amesema Mmuya.
Amesema katika shule hizo nne, itapandwa miti 2,000 kwa mgawanyo wa miti 500 kila shule, huku lengo ni kuwafundisha watoto kuwa mapato yanawezekana kupatikana kwa kupanda miti ya matunda.
Mmuya ametoa mfano wa mti wa parachichi ambao unatoa matunda 300 kwa msimu mmoja ambayo kwa soko la Mkoa wa Dodoma unaweza kumuingiza sio chini ya Sh300,000.
“Hii ni hamasa kwa wadau wengine. Tuwapatie miti mingine watoto hawa wakapande nyumbani kwao. Mti mmoja shuleni na mwingine nyumbani, ndani ya kipindi cha miaka saba atakuwa na miti itakayompatia faraja kwa kuyaona matunda yake,”amesema.
Amesema katika kipindi cha kati ya mwaka 2017, kampeni ya kukijanaisha Mkoa wa Dodoma, imeweza kupanda miti milioni 16.
Aidha, amesema wametenga bajeti katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma kwa ajili ya upandaji wa miti kupitia programu ya ‘mti wangu birthday yangu’.
Amesema kila halmashauri imepanga bajeti isiyopungua Sh10 milioni kwa ajili ya upandaji na utunzaji wa miti hususani ya matunda katika mwaka 2025/26.
Kiongozi wa Tawifa, Fikira Ntomola amesema wameanzisha kampeni ya Mti Pesa ambayo inalenga katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
“Kupanda miti si kwa ajili ya mazingira bali ni kuchochea uchumi wetu na tumekuja na miti ya matunda 2,000 ambayo tunakwenda kushirikiana na shule kuipanda. Kwa hapa tunapanda miti 500. Na hii yote ni kuwajengea wanafunzi ile tabia kuwa akiwa na mti wa matunda anaweza kulinda mazingira,”amesema.
Pia, amesema kwa kupanda miti hiyo,kunamjenga mwanafunzi kujiwekea dhamira kuwa hakuna kitu kinachokuja kirahisi bila kufanya kazi.
Amesema shughuli ya upandaji miti, itafuatiwa na utoaji wa elimu ya fedha kwa wanawake wajasiriamali wa Mkoa wa Dodoma na mkutano mkuu wa mwaka.
Mkuu wa Shule ya Msingi ya Mtumba, Kepha Kitutu amesema upatikanaji wa miti hiyo utawasaidia kwa kiwango kikubwa katika utunzaji wa mazingira.
“Hii ni fursa kwetu kama taasisi ikiwa tutaitunza miti hii vizuri. Tukivuna matunda na kupeleka sokoni tunauwezo wa kuboresha maeneo mengine ya kitaaluma ambayo yanaweza kutusaidia. Pia, yatasaidia wanafunzi wetu kupata matunda,”amesema.