Utitiri wa mifuko ya uwezeshaji wananchi wawaibua wabunge

Dodoma. Utitiri wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi nchini ambayo mingine haijulikani kwa wananchi, umewaibua wabunge wakitaka iundwe tume ama mamlaka ya kusimamia suala hilo.

Wabunge wameyasema hayo leo Ijumaa, Aprili 11, 2025 wakati wakichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26.

Aprili 9, 2025, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliliomba Bunge liidhinishie Sh782.08 bilioni kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge.

Mbunge wa Vunjo, Dk Charles Kimei wakati akichangia mjadala wa makadilio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Ijumaa Aprili 11, 2025 bungeni, Dodoma.

Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Vunjo (CCM), Dk Charles Kimei amesema mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi haifahamiki na wanapokutana bungeni, kinachozungumzwa ni mikopo ya asilimia 10 tu inayotolewa na halmashauri nchini.

“Na hii ni kwa sababu watu hawaifahamu, hakuna mtu anayeiuza mifuko hii, naamini imekaa mahali ambapo si sehemu yake. Ninaamini lazima tuunde mamlaka ambayo itasimamia suala zima la uwezeshaji wananchi,” amesema.

Dk Kimei ameshauri kufanyika kwa tathmini ya awali itakayobainisha ni watu gani waliokopeshwa tayari, kabla ya kuanzishwa kwa mfumo mpya wa utoaji mikopo.

Amesisitiza kuwa mfumo huo unapaswa kuwawezesha watu kuomba na kupata mikopo binafsi bila kulazimika kujiunga na vikundi, ambavyo kwa baadhi ya matukio vimekuwa chanzo cha matatizo na kuharibu nia njema ya utoaji wa mikopo.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Sylvia Sigula amesema ndani ya Serikali kuna mifuko ambayo inatoa mikopo moja kwa moja kwa walengwa zaidi ya 22, mifuko inayotoa ruzuku 26 na programu za uwezeshaji kiuchumi zaidi ya tisa.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Sylvia Sigula, akichangia mjadala wa makadilio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Ijumaa Aprili 11, 2025 bungeni, Dodoma.

Hata hivyo, amesema vijana hawana taarifa sahihi kuhusu mifuko hiyo na kuwa wanatamani kuona Serikali inaweka programu maalumu ya kuwanufaisha vijana moja kwa moja.

Ameomba mifuko hiyo ishuke hadi katika halmashauri ama iunganishwe na mikopo ya asilimia 10.

Kuhusu mikopo inayotolewa na halmashauri, alisema bado kuna changamoto na kwamba vijana wanatamani itolewe kwa mtu mmoja mmoja na si vikundi ambao inawafanya wengi wanakosa fursa.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Neema Mwandabila amesema kumekuwa na mikopo ya pembejeo, mingine inatolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pia na Nishati, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu na halmashauri.

Amesema dhamira ya Rais ni nzuri ya kuwakwamua wananchi kiuchumi, lakini bado nia ya dhati ya watu waliopewa dhamana ya kusimamia haionekani katika kuwafikia wananchi.

“Hata sisi wabunge pia hatufahamu vizuri na kutokana na mikopo hii niashauri basi iundwe tume ambayo itasaidia kuwezesha utoaji mikopo kwa wananchi,”amesema.

Amesema kwa kufanya hivyo hata gharama za uendeshaji kuwafikia wananchi zitapungua.

Mbunge wa Viti Maalum kupitia CCM, Janejelly Ntate, amesema Halmashauri ya Temeke jijini Dar es Salaam iliwapatia madaktari bingwa watano mkopo wa Sh250 milioni.

Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Janejelly Ntate akichangia mjadala wa makadilio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Ijumaa Aprili 11, 2025 bungeni, Dodoma.

Amesema kupitia mkopo huo, madaktari hao waliweza kuanzisha kliniki na kutoa ajira kwa watu 20 ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Ameshauri kuwa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ielekezwe kwa vijana waliomaliza masomo, lakini hawana ajira, kwa kuwawezesha kuunda vikundi na kupatiwa mitaji, hatua ambayo itawasaidia sio tu kujiajiri bali pia kuwaajiri wenzao.

Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedatus Manyinyi amesema Tanzania ina nguvu kubwa ya vijana ambao wamekuwa wakisomeshwa, lakini ajira ni chache na hivyo kuna kila sababu ya kuangalia utaratibu mpya wa namna ambayo wanaweza kuajiri vijana wengi kwenye kilimo, biashara na ujasiriamali.

“Ndio maana hata ukiangalia wako wageni wengi sasa wanaingia nchini wanachukua ajira za wale vijana wetu na hao vijana unawakuta saa sita za mchana wako katika pool kwa sababu hawana kazi za kufanya wala mitaji,” amesema.

Mbunge wa Musoma Mjini (CCM), Vedatus Manyinyi akichangia mjadala wa makadilio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2025/26 leo Ijumaa Aprili 11, 2025 bungeni, Dodoma.

Ameshauri katika bajeti zijazo, Serikali iangalie jinsi ya kuboresha maisha ya vijana ili maisha yao yaweze kuendelea.

Mbunge wa Sumve (CCM), Kasalali Mageni amesema katika maeneo mengi watu wanapata ajira kwa kujuana ndiyo maana zikitangazwa nafasi za ajira watu wanaanza kutuma jumbe fupi (sms) kwa wabunge wao.

“Serikali ikitangaza nafasi za ajira simu za wabunge zinaanza kujaa sms watu wakiomba kusaidiwa kupana nafasi, huu utaratibu wa utoaji wa ajira unatakiwa kuangaliwa upya,” amesema Mageni.

Mbunge huyo ameomba Ofisi ya Waziri Mkuu itazame kwenye eneo hilo na kuweka utaratibu mzuri ili kuondoa kilio cha watu nchini na kuifuta dhana ya ajira kwa kupeana.

Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu ametaka vijana wafanyiwe mafunzo ya kujitambua, mambo ya maadili na wawezeshwe kiuchumi.

“Huko tunakokwenda jamani ikitolewe hata kitrilioni kimoja kipelekwe kwa vijana wakachakachue uchumi sio kuanzishwa (miradi), hata wale waliopo katika kilimo, ufundi tuwaongezee uwezo, tuwajenge ujuzi na mitaji tuwaongezee hawa ndio future ya taifa letu,”amesema.

Ametaka pia wapewe elimu na kulindwa kwa kuwa hao ndio wanaoathirika kikubwa wa maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (HIV) na kuwa takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 34 ya watu 60,000 wanaopata maambukizi mapya ni vijana wenye umri 15-25.

“Vijana wanalindwa vipi jamani, hebu tuliangalie. Lakini, watoto wetu hawa wengi wanaathirika katika pombe, zipo pombe zilizochafuliwa. Nchi hii ina watu wengi wanakunywa pombe zilizochafuliwa,”amesema.

“Pombe hazijapimwa kitaalamu kwa kukosa chombo cha kudhibiti usalama wa chakula, watu wanatengeneza pombe wanavyotaka wao. Naomba hili tuangalie ili kuwalinda vijana,”amesema.

Kauli za wabunge hao zinakuja wakati kukiwa na maelfu ya vijana wanaojitokeza kuomba ajira zilizotangazwa hivi karibuni za katika kada mbalimbali za ualimu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Jeshi la Zimamoto na Ukoaji.

Sakata la ajira katika kada ya ualimu lilizua mjadala kiasi cha kusababisha kuibuka kwa Umoja wa Walimu Wasio na Ajira Tanzania (Neto) kuanzia mwaka 2015 hadi 2025 wakilalamikia changamoto ya upatikanaji wa ajira.

Related Posts