Wachimbaji wataka kifungu cha sheria ya madini kibadilishwe

Mwanza. Baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini nchini wameiomba Serikali kufanya marekebisho au kufuta kabisa Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, kinachoruhusu mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji kuingia makubaliano ya msaada wa kiufundi na raia wa kigeni.

Wamedai kifungu hicho kimekuwa kikwazo kwao, kwani baadhi ya wageni wanaoingia kwa mwamvuli wa msaada wa kiufundi wamekuwa wakijitwalia mamlaka makubwa kiasi cha kuwageuza wachimbaji wa ndani kuwa “wageni” katika migodi yao wenyewe.

Wakizungumza leo Ijumaa, Aprili 11, 2025, katika kikao cha kukusanya maoni kuhusu msaada wa kiufundi kwa wadau wa sekta ya madini jijini Mwanza, wachimbaji hao wameitaka Wizara ya Madini kulitazama suala hilo ili kulinda masilahi ya wachimbaji wadogo dhidi ya ukandamizaji na unyonyaji.

Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Yahya Samamba akizungumza na wadau wa sekta ya madini katika kikao cha kupokea maoni ya msaada wa kiufundi jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Mchimbaji mdogo kutoka mkoani Mwanza, Victor Batule, alisema:

“Tumekuwa tukikumbana na vitendo vya manyanyaso kutoka kwa wageni tuliodhani wangetusaidia. Wanapopata nafasi, wanatutenga sisi wamiliki na hata kuwafukuza Watanzania waliokuwa wamepata ajira kwenye migodi hiyo.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wachimbaji Madini Vijana nchini, Magreth Ezekiel, amesisitiza umuhimu wa marekebisho ya kifungu hicho, lakini akasisitiza kuwa lazima yahusishe pia ujenzi wa uwezo kwa vijana.

“Kifungu kinapaswa kufanyiwa marekebisho, lakini baada ya sisi kujengewa uwezo wa kitaalamu. Vijana wapewe mafunzo na mikopo rahisi ili waweze kujitegemea. Tukishajijenga, ndipo tuwe na majadiliano ya kweli na wageni,” alisema Magreth.

Baadhi ya wachimbaji na wadau wa sekta ya madini wakiwa katika kikao cha kutoa na kupokea maoni ya msaada wa kiufundi jijini Mwanza kilichoandaliwa na Femata. Picha na Saada Amir

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mwanza, Sabana Salinja, ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizopo, bado baadhi ya wachimbaji wamenufaika kupitia ushirikiano huo.

“Ni kweli changamoto zipo, lakini kupitia mikataba hii, wachimbaji hupata mafanikio kama vile elimu ya kiufundi na msaada wa kifedha unaoongeza uzalishaji na ufanisi,” alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Yahya Samamba, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, ameeleza kuwa kifungu hicho kilianzishwa kutokana na maoni ya wachimbaji wenyewe waliotaka kushirikiana na wageni ili kujifunza teknolojia ya kisasa.

“Lengo lilikuwa kuwawezesha wachimbaji wa ndani kufaidika na mitambo na mbinu bora. Msaada wa kiufundi siyo tatizo, bali changamoto ipo kwa baadhi ya wageni waliogeuka kuwa kero baada ya kuingia mikataba,” alisema.

Related Posts