22 wanusurika kifo daladala ikitumbukia mtaroni Dar

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 22, wamenusika kifo baada ya kutokea ajali ya daladala inayofanya safari zake kati ya Mbagala-Ubungo Simu 2000.

Ajali hiyo imetokea leo Jumamosi Aprili 12, maeneo ya Tabara Relini Mwananchi, Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam ikihusisha gari aina ya Eicher. Gari hiyo ilikuwa ikitokea Ubungo kuelekea Mbagala, iliacha njia na kudumbikia mtaroni.

Baadhi ya abiria wakitoa ushuhuda wao, akiwemo Ester Luwole amesema gai  hiyo ilionekana kuwa mbovu tangu wanaipanda kituo walichoanzia safari cha UbungoSimu2000.

“Wakati tukianza safari kituoni pale tulitembea kama hatua kumi baadaye gari hiyo ikawa inazima ambapo dereva na konda wake wakawa wanaishtua.

“Hata hivyo baadaye anasema ilitembea lakini kwa bahati mbaya mimi nilipitiwa na usingizi, japo nikiwa usingizini nilihisi gari hiyo kukipita kitu ambacho sikuweza kukiona hadi nilipojikuta na abiria wenzangu tupo mtaroni,” amesema Ester..

Naye Regina George mkazi wa Mbagala, amesema kilichotokea hakujua zaidi ya kushtuka wapo mtaroni kwani yeye alikuwa ameketi siti za nyuma.

Regina amesema alikuwa kwenye usafiri huo akitokea mawasiliano kufuata mahindi mabichi kwa ajili ya kwenda kuyachoma.

Fatuma Mohamed, mkazi wa Mbagala Kizinga, amesema alipanda gari hiyo kituo cha External na  aliishuhudia gari ikiingia kwenye mtaro na wala hakukuwa na kitu chochote ambacho  dereva alikuwa anakikwepa.

Faustino Agrey  mkazi wa Kisemvule, amesema dereva alikuwa anaipita bajaji, na katika kuipita alivyokata kurudi upande wake alikata nyingi hadi kujikuta anaingia mtaroni.

Mchungaji Issac Sogani amesema hajajua nini kilichotokea zaidi kujikuta yupo mtarani anapambana kuweza kutoka ndani ya gari hiyo baada ya kudumbukia mtaroni.

“Nashukuru tu nimetoka salama licha ya kuwa nimepata  majeraha madogo hususani usoni na pia nimepoteza simu yangu ambayo nahangaika hapa niweze kuifunga kabla ya wahalifu hawajafanya yao,” amesema Mchungaji huyo.

Mwananchi Digital iliyokuwa maeneo hayo ilishuhudia baadhi ya abiria walikuwa wamelala chini baada ya kutolewa na wasamaria wema katika gari hilo.

Pia, askari polisi wapatao watano walifika katika eneo hilo kwa ajili  ya kuchukua taarifa za majeruhi na abiria wengine waliokuwepo kwenye gari hilo huku wengine wakipakiwa kwenye bajaji kwa ajili ya kupelekwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mmoja wa maaskari aliyekuwepo eneo hilo a kutotaka kutajwa jina lake, kwa kuwa sio msemaji wa Polisi, amesema wameandika majina ya majeruhi zaidi ya 22.

Related Posts