ABSA BANK TANZANIA YAZINDUA ‘AKAUNTI YA MZAWA’ – SULUHISHO LA KIBUNIFU KWA WATANZANIA WAISHIO UGHAIBUNI

 

Na Mwandihi Wetu 

Absa Bank Tanzania  imezindua rasmi Akaunti ya Mzawa,
huduma kamili ya kibenki kwa Watanzania waishio, wanaofanya kazi na kusoma nje
ya nchi.

Uzinduzi huo umefanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency
jijini Dar es Salaam kwa njia ya mseto (“phygital”) ambapo wadau muhimu
walihudhuria ana kwa ana huku wengine wengi kutoka ughaibuni wakijiunga kwa
njia ya mtandao.

Akaunti ya Mzawa imelenga kuondoa changamoto
zilizodumu kwa muda mrefu zinazowakabili Watanzania waishio nje ya nchi, ikiwa
ni pamoja na ugumu wa kupata huduma za kifedha, changamoto za kufungua akaunti
za fedha za kigeni, pamoja na upungufu wa taarifa za fursa na msaada wa mbali.
Huduma hii inatoa upatikanaji wa kimataifa wa akaunti kwa sarafu tano (TZS,
USD, GBP, EUR, na ZAR), kufanikisha miamala rahisi, fursa za uwekezaji, na
huduma za bima kupitia Absa Bima.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mgeni rasmi katika
hafla hiyo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Cosato David Chumi  alikiri mchango mkubwa wa diaspora pamoja na
changamoto wanazokumbana nazo: “Diaspora yetu haijajitenga – imewekeza kwa
dhati.

Lakini kwa bahati mbaya, hawapati fursa za
kutosha kushiriki ipasavyo. Na sisi kama serikali tunasema tumewasikia.
tunawaona. na tunachukua hatua. Chini ya uongozi wa . Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan, serikali imepiga hatua kubwa kupitia huduma za ubalozi kwa njia ya
kidijitali, majukwaa ya uwekezaji ughaibuni, na sasa kuhimiza mabenki kama Absa
kuunda huduma mahsusi kwa diaspora.”

Naibu Waziri pia alipongeza Absa kwa kutoa suluhisho
la wakati, jumuishi na lenye tija: “Akaunti ya Mzawa ya Absa inaleta pamoja
kila kitu ambacho diaspora imekuwa ikikiomba. Kwa Watanzania wote waishio nje
ya nchi, nawaambia: muda ni huu. Miundombinu inajengwa. Msaada unazidi
kuongezeka. Tuchukue hatua sasa – tujenge nyumba, tufungue biashara, tuwekeze,
na tujikite nyumbani Tanzania.”

 U

zinduzi wa Akaunti ya Mzawa unaendeleza pia
huduma ya awali ya
Mkopo wa Nyumba kwa Diaspora kutoka Absa, ikiwapa
Watanzania wa ughaibuni uwezo wa kudhibiti fedha zao huku wakiwekeza kwenye
maendeleo ya muda mrefu nyumbani.

Kwa kuzingatia ahadi yake ya chapa, “Stori yako ina
thamani’” na dhamira ya shirika “Kuiwezesha Afrika ya Kesho, pamoja,
stori moja baada ya nyingine”, Absa Bank Tanzania inaendelea kutoa
suluhisho bora zinazomlenga mteja, ili kuwaunganisha Watanzania wote na fursa
zilizopo nyumbani – popote walipo duniani.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Masuala ya
Diaspora, inakadiriwa kuwa zaidi ya Watanzania 400,000 wanaishi nje ya
nchi, wakiwa wengi wao wako Marekani, Uingereza, Kanada, Ulaya, Mashariki ya
Kati, na kusini mwa Afrika. Mwaka 2022 pekee, Watanzania waishio
ughaibuni walituma zaidi ya USD milioni 598 kurudi nyumbani, sawa na
zaidi ya TSh trilioni 1.4, huku zaidi ya TSh bilioni 6.4
zikitumika kununua mali.

Related Posts