Babu adaiwa kumuua mjukuu wake Shinyanga

Shinyanga.  Mtoto wa siku mbili mkazi wa Kijiji cha Shatimba Kata ya Nyamalogo Wilaya ya Shinyanga anadaiwa kuuawa na babu yake Maganga Mungo, baada ya kumchukua na kumbamiza chini kutokana na ugomvi wa kifamilia.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Aprili 12, 2025 Mwenyekiti wa Kijiji cha Shatimba Kalonga Shilu amesema tukio hilo lilitokea jana saa tatu usiku baada ya babu yake kuomba apatiwe mtoto ili amuone.

Amesema familia hiyo ilikuwa na ugomvi wa muda mrefu kutokana na binti wa familia hiyo kuolewa na baba yake mdogo na kuzaa naye mtoto huyo ambaye kwa sasa ni marehemu jambo ambalo limesababisha baba yake mzazi kuwa na hasira na kuchukua uamuzi huo.

“Kweli kuna mauaji yamefanyika huyo baba anayeitwa Maganga Mungo baada ya mtoto wake kutoka hospitali alipofika nyumbani aliomba kumuona mjukuu wake alipompokea alimbamiza chini kisha akasema anauwa mtoto, mama na binti yake,” amesema Mwenyekiti.

Amesema baba wa familia hiyo alipigiwa simu na mkwe wake  na kumwambia amlee mtoto huyo hadi afikishe miaka mitatu halafu atamlipa gharama zote na kumchukua kutokana na kumzuia kufika kwenye familia hiyo.

Hata hivyo, tayari amekamatwa na polisi yuko Kituo cha Polisi Iselamagazi.

Paul Maige, mkazi wa Kijiji hicho, amesema kitendo alichofanya cha kukatisha uhai wa mjukuu wake ni ukatili wa kinyama jambo ambalo halikubaliki katika Jamii, amesema ni vema suala hilo wangekaa kifamilia na kufikia mwafaka na siyo kujichukulia sheria mkononi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amesema hana taarifa ya tukio hilo na kuahidi kufuatilia.

Related Posts