Rais Samia asisitiza amani kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 2025

Unguja. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haitakubali atokee mtu yeyote kuvuruga amani na kusababisha mpasuko miongoni mwa wananchi hususani katika kipindi cha uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Amesema Taifa linapaswa kujifunza umuhimu wa amani kwa kuangalia nchi ambazo zimeikosa kwa kipindi kirefu, namna wananchi wake wanavyoathirika, jambo linalorudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Aprili 12, 2025 katika hotuba yake iliyosomwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alipomwakilisha katika hafla ya maadhimisho ya maombi ya dunia ya Umoja wa Wanawake wa Kikristo Zanzibar yaliyofanyika katika Kanisa Kuu la Anglikana Mkunazini Zanzibar.

Wakati Rais Samia akitoa kauli hiyo, Kamati ya Amani Zanzibar, imekabidhi kitabu cha mwongozo utakaotumika katika kuendesha kazi za kamati hususani katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Kitabu hicho kimeelezea haki, uadililifu na amani kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili kuifanya nchi kuwa salama na yenye utulivu wakati wote.

Katika hotuba hiyo, Rais Samia ametolea mifano kama ya nchi za Somalia, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambazo zimekumbwa na machafuko ya amani huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake na watoto.

“Serikali zote mbili hazitamvumilia mtu yoyote au kikundi cha watu ambacho kitabainika kuleta viashiria vya uvunjifu wa amani nchini, tumeona namna ambayo mataifa haya amani imeondoka na changamoto wanazipotia,” amesema.

Kauli kama hii, Rais Samia aliitoa Machi 31, 2025 wakati wa Baraza la Idd lililofanyika jijini Dar es Salaam akiwa mgeni rasmi kwa mwaliko wa Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir.

Katika kusisitiza hilo amesema: “Tuendelee kutunza amani na mshikamano wetu uliopo bila kujali itikadi zetu za dini wala vyama, linapokuja suala la umoja na amani basi tusimame pamoja.”

Amesema amani inapotoweka kuna athari kubwa za kibinadamu na kimazingira kwani watu hutaabika kwa kupoteza makazi na wengine kupoteza maisha, hivyo wasikubali iwapo kuna viashiria vyovyote vya kufanya hivyo.

Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuwataka wanawake wajitokeze katika fursa mbalimbali zinazojitokeza bila kubaki nyuma kwani wanaweza na wataungwa mkono katika jitihada zao.

Ameupongeza umoja huo wa wanawake wa kikristo Zanzibar kwa kuweka utaratibu wa kila mwaka kuliombea Taifa na kuwataka kuendelea na utaratibu wao huo ili Taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano na kupiga hatua kubwa zaidi za kimaendeleo katika nyanja  za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia.

Amesema umoja huo umekuwa ukifanya kazi kubwa katika kuisaidia jamii na kupata mafanikio ikiwa ni pamoja na kuwafikia wanafunzi 2,600 wa shule mbalimbali za msingi na sekondari kwa kuwapatia elimu ya kupinga udhalilishaji shuleni na maeneo mengine.

Kadhalika, kuwafariji watoto wanaoishi katika mazingira magumu na kuwapatia elimu wajasiriamali 280 tangu mwaka 2022 hadi 2024.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa Zanzibar, Askofu Augustino Shao amesema amani inayoimbwa na kuombewa wanawake ndio kiini kikubwa na msingi wake amani hiyo.

Amesema wanawake ndio walinzi wakubwa wa amani katika nchi yoyote ile duniani, hivyo ameutaka umoja huo kuzidisha juhudi katika kuiombea nchi amani pamoja na viongozi wakuu wananchi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

“Bila nyie (wanawake) hakika ulimwengu hauwezi kuwa kama ulivyo, amani tunayoomba sisi na tunayoomba muiombee dada zangu ninyi ndio kiini na msingi mkubwa wa kulinda amani yetu, hatuna shaka akina mama wengi wanapohusika hakika kuna amani,” amesema.

“Amani ni mbinu ya utume wao kwa sabbau wanakuwa na uchungu tangu wanapozaa na kulea watoto wakiwa wadogo, amani ni sala ya shghuli zao,” amesema.

Askofu Shao ametilia mkazo ombi la wanawake wa Kikristo waliloomba kupitia risala yao kupatiwa eneo la kujenga ofisi kubwa itakayotumiwa na wanawake wote pasipo kujali itikadi zao kwa lengo la kuendeleza shughuli mbalimbali za maendeleo nchini.

Mapema akisoma risala ya umoja wa wanawake hao, mwenyekiti wa umoja huo, Lucy Mwakyembe amesema wamekuwa wakifanya maombi kila mwaka kuliombea taifa kuepukana na majanga mbalimbali ikiwemo maradhi, ukame na udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto ili Taifa liweze kuzidi kupiga hatua kimaendeleo.

Lucy amesema kwa mwaka huu jukumu kubwa la umoja huo ni kuiombe nchi kuendelea kuwa na amani  hasa katika kipindi cha uchaguzi mkuu ili ufanyike katika hali ya utulivu na kuwaomba wanawake wote  wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wakati utakapofika.

Hata hivyo, amesema wanakabiliwa na changamoto ya eneo kwa ajili kuendeshea shguli zao kwani wamekuwa wakijitoa kwenye jamii na kuisaidia katika changamoto mbalimbali.

Kamati yakabidhi mwongozo

Wakati huohuo, kamati ya amani Zanzibar imekabidhi kitabu cha mwongozo utakaotumika kuendeshea kazi za kamati hususani katika mchakato mzima wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kitabu hicho kimeelezea haki, uadililifu na Amani kabla ya uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi ili kuifanya nchi kuwa salama na yenye utulivu wakati wote.

Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema kamati hiyo imejipanga kuwafikia viongozi wa vyama vya siasa kuzungumza nao juu ya kudumisha amani na utulivu uliopo nchini pamoja na  matumizi ya lugha nzuri katika kipindi chote  cha kampeni zinazotarajiwa kufanyika mwaka huu ili kuepuka kuchafuana na kushushiana hadhi hasa ikizingatiwa kuna maisha baada ya uchaguzi.

Sheikh Mfaume amesema kuelekea katika uchaguzi mkuu, amani ni suala muhimu ambalo litasababisha kufanyika kwa uchaguzi katika hali ya utulivu na kupata viongozi bora watakaondelea kuiongoza nchi na kuiletea maendeleo endelevu kwa wananchi wote.

Kwa upande wake Mchungaji Lusungu Mbilinyi kutoka Kanisa la KKKT Zanzibar, amesema kamati imeandaa kitabu chenye muongozo wa kufanyia kazi zao ambacho kimeelezea mambo mbalimbali ikiwemo dhana nzima ya uchaguzi mkuu, wajibu wa kila raia wa Tanzania katika kipindi hicho.

“Kitabu hiki kina miongozo katika kipindi cha uchaguzi, mizozo na utatuzi wake, makundi yenye ushawishi katika uchaguzi na wajibu wao pamoja na kuyaangalia makundi yanayoathirika katika kupindi cha uchaguzi ambayo hayawezi kujisemea na pia hukosa watetezi wa kuwapizia sauti zao,” amesema

Akipokea kitabu hicho ofisini kwake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla ameitaka kamati hiyo kutumia njia mbalimbali kuhubiri amani ili idumu.

Amesema kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kuhubiri na kuidumisha amani iliyopo nchini ili kuweza kuvisaidia vizazi vijavyo kuweza kuikuta nchi ipo katika hali ya amani na utulivu.

Hemed amewataka viongozi wa  Serikali, viongozi wa dini na viongozi wa vyama vya siasa kutumia majukwaa kwa lengo la  kuwakubusha wafuasi wao juu ya umuhimu wa kuidumisha amani iliyopo nchini pamoja na kutumia lugha zenye kujenga na sio kuleta viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kamati hiyo imejumuisha viongozi mbalimbali wa dini kutoka Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ofisi ya Kadhi Mkuu, Kamisheni ya Wakfu, Chuo cha Kiislamu, Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Kanisa la Anglikana, Kanisa katholiki, KKKT, Pentakoste na vyombo vya habari.

Related Posts