Dar es Salaam. Ripoti mpya ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kuhusu mwelekeo wa jinsia katika ajira, imebainisha kuwa wanawake waliotalikiana, walioachika au wajane wanakumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii, hali inayowaweka kwenye hatari kubwa ya kuishi katika umaskini.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Machi 2025, kundi hili linawakilisha karibu asilimia 20 ya wanawake wote nchini wenye umri wa miaka 15 na kuendelea, na wengi wao hukosa fursa sawa za kijamii na kiuchumi kama ilivyo kwa wengine.
Ripoti imebainisha kuwa wanawake hao huachiwa mzigo wa kulea watoto wao bila ushirikiano kutoka kwa wenza wao.
Jambo hilo limetajwa kuchangiwa na sababu kadhaa, kama kutoelewana kwa wazazi na kukosekana kwa mifumo imara ya ulinzi wa haki zao.
“Wanawake katika makundi haya wana uwezekano mkubwa wa kupoteza haki zao za kijamii na kiuchumi na kuangukia katika umaskini, huku wakibeba jukumu la kulea watoto na kuendesha maisha ya familia,” imesema ripoti hiyo.
Wajane, ambao ni asilimia 11 ya wanawake wote, wako katika hatari kubwa zaidi ya umaskini kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Ripoti imependekeza kuwapatia msingi imara uliozingatia usawa wa kijinsia, kupitia sheria na sera ili kuhakikisha maendeleo ya haki na usawa kwa wote.
Ripoti hiyo inaonyesha takribani nusu ya watu wenye umri wa miaka 15 na zaidi nchini wameoa au kuolewa. Wale ambao hawajawahi kuoa au kuolewa wanachukua sehemu ya pili kwa ukubwa, yaani asilimia 30.1, wakiwa ni zaidi ni wanaume (asilimia 36.1) ikilinganishwa na wanawake asilimia 24.6.
“Katika maeneo yote, wanawake wana uwezekano mkubwa wa kupoteza wenza wao na kuwa wajane kuliko wanaume. Watu waliotalikiana au kuachana na wenza wao wa ndoa wanachangia jumla ya asilimia 6.4,” imeeleza ripoti hiyo.
Mkazi wa Mbezi Luis, Rahma Omary akizungumzia hali hiyo, amesema changamoto hiyo inawakumba wanawake wengi wanaokosa msaada wa kisheria, akitolea mfano masahibu yaliyowahi kumkuta yeye.
“Mtu unamshitaki baba mtoto wako, unatinga ustawi wa jamii mpaka miguu unapasuka gaga, halafu unakuja kupewa Sh50, 000 kwa mwezi, utanunua nini kwa maisha ya sasa,m tunanyanyasika sana wanawake,” amesema Rahma.
Mkazi wa Chanika, Aisha Kintu amesema fedha ambazo mwanamke angezipata akiwa na mwenzake, wangegawana majukumu, anajikuta hela hiyohiyo anaipeleka kwa ajili ya watoto kwenda shule, chakula nyumbani na kulipa bili mbalimbali.
“Jukumu la watu wawili anafanya mtu mmoja, changamoto kama hizo lazima ziwepo. Familia nyingi mtoto wa kike ndiye anayewakumbuka wazazi, ikilinganishwa na wa kiume, ukimpeleka mtoto wa kike shule umeikomboa familia.
“Sasa huyu binti ana familia yake na nyumbani anapotoka, kipato nacho kidogo mjini analipa kodi, watoto hawajavaa, hawajaumwa, hawajasoma na mwisho wa siku uvumilivu unawashinda wanaangukia kwenye shughuli zisizo halali, ili wakidhi mahitaji ya familia,” amesema Aisha.
Aisha ameshauri wanaume kuhakikisha wanatunza watoto wao, licha ya mikwaruzo iliyopo baina yao kama wazazi.
Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku amesema inapotokea hali hiyo, jukumu la kuhakikisha familia inakua, mtoto anaenda shule, anatibiwa linabaki kuwa la mwanamke, fedha ambayo ingeweza kwenda kwenye maendeleo na kuwekeza zinatumika katika matumizi ya kila siku.
“Mwanamke wa aina hii akipata mtu anayemuongoza na kumsaidia hufanikiwa lakini akikosa elimu, wengi wanaingia kwenye vikundi ambavyo baadaye vinakuwa msumari kwao,” amesema.
Nduku amesema kuna umuhimu wa kuutazama mfumo kwenye umiliki wa mali, kwani nyingi huandikwa majina ya waume, hivyo wanapotangulia mbele za haki, familia ya upande wa mume inachukua vitu vyote, sheria haijamtambua na wengine hawana uelewa wa sheria.
Katika mifumo ya elimu, ripoti hiyo imeonyesha kiwango cha elimu ni cha chini zaidi katika maeneo ya vijijini ikilinganishwa na maeneo ya mijini huku wanawake wakiongoza kwa kukosa elimu.
Asilimia 25 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 na kuendelea wanaoishi vijijini hawana elimu kabisa, ikilinganishwa na asilimia nane ya wanawake wa umri huo wanaoishi mijini.
Vilevile, asilimia 15 ya wanaume wa vijijini wenye umri wa miaka 15 na zaidi hawana elimu, ikilinganishwa na asilimia tatu ya wanaume wa mijini wa umri huo.
Ripoti pia imeonyesha karibu asilimia 20 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 na kuendelea hawana elimu yoyote, ikilinganishwa na karibu asilimia 11 ya wanaume.
“Pengo la kijinsia linaonekana katika ngazi zote za elimu, na tofauti kubwa zaidi ikiwa katika ngazi ya msingi ambapo kuna tofauti ya asilimia 3.5, sawa na asilimia 60.8 kwa wanaume na asilimia 57.3 kwa wanawake,” imeonyesha ripoti hiyo.
Takriban asilimia 59 ya watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea nchini wana elimu ya msingi.
Watu wenye elimu ya chuo kikuu ni asilimia 1.9 tu ya watu wote wenye umri wa miaka 15 na zaidi, huku idadi ikiwa juu zaidi kwa wanaume kwa asilimia 2.4, ikilinganishwa na wanawake asilimia 1.4.
“Mfumo huu pia unaonekana Tanzania Bara. Zanzibar, zaidi ya nusu ya watu wenye umri wa miaka 15 na kuendelea wamefikia elimu ya sekondari ya chini au ya juu, na takriban asilimia 3.6 wamepata elimu ya chuo kikuu, ingawa karibu asilimia 15 ya wanawake hawana elimu ikilinganishwa na asilimia saba ya wanaume,” inaonyesha ripoti hiyo.
Katika eneo la ukosefu wa ajira na matumizi duni ya nguvu kazi, ripoti imeonyesha kwa ujumla, viwango vya ukosefu wa ajira kwa wanawake ni vya juu kuliko kwa wanaume. Ripoti imeonyesha asilimia 12.7 kwa wanawake na asilimia 5.8 kwa wanaume nchini.
Tofauti za kijinsia katika viwango vya ukosefu wa ajira huwa kubwa zaidi katika kundi la umri wa miaka 25 hadi 44, ambapo kiwango cha ukosefu wa ajira kwa wanawake kiko juu kwa takribani alama 10 za asilimia, ikilinganishwa na wanaume.
Matokeo pia yanaonyesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira kwa wanawake kiko juu zaidi mijini kuliko vijijini, huku hali ikiwa kinyume kwa wanaume Tanzania Bara na Zanzibar.
Kuhusu watu wenye ulemavu, kiwango cha jumla cha ukosefu wa ajira kwa kundi hili ni asilimia 5.9, ambapo wanawake wana kiwango cha juu (asilimia 7.1) kuliko wanaume (asilimia 4.3).
Hata hivyo, ripoti inasema matumizi duni ya nguvu kazi yanatoa taswira kuhusu tabia na hali ya wanaume na wanawake katika soko la ajira, hasa katika kutafuta ajira au ubora wa ajira walizonazo.