Sababu za biashara za wajasiriamali wanawake kutoimarika zatajwa

Dodoma. Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake la Mkoa wa Dodoma limesema miongoni mwa vikwazo vinavyofanya biashara za wajasiriamali wanawake kushindwa kukua ni tabia za kufanya matumizi yasiyopangwa katika bajeti.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Mkoa wa Dodoma, Mary Barnabas ameyasema hayo leo Aprili 12, 2025 wakati akizungumza katika mafunzo ya kifedha na kibiashara yaliyoandaliwa na taasisi ya Chama wa Wanawake kwenye Sekta ya Fedha (Tawifa).

Amesema ni muhimu wanawake kubadili tabia za kifedha, kuepuka matumizi yasiyopangwa kwenye bajeti na kutumia rasilimali walizonazo kwa malengo ya maendeleo ya biashara.

“Tunapaswa kuzingatia elimu tunayopewa. Tukiitumia vyema, biashara zetu zitakua na mitaji itaongezeka,” amesema Mary.

Amesema mafunzo hayo ni muhimu, lakini ni idadi ya waliopata mafunzo ni ndogo kwa kuwa jukwaa hilo lina wanawake 6,000 wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali mkoani humo.

Awali, akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala Msaidizi, Aziza Mumba amesema kuwa mafanikio ya wajasiriamali wanawake yanategemea nidhamu ya fedha na matumizi sahihi ya maarifa ya kifedha.

“Biashara haiwezi kukua kama hakuna nidhamu ya fedha. Mafunzo haya ni muhimu kwa kila mjasiriamali anayetaka kuimarika kiuchumi,” amesema.

Amesema benki nyingi ziko tayari kutoa mikopo, lakini zinahitaji kuona mwelekeo wa biashara na usimamizi mzuri wa mapato na matumizi ya mjasiriamali husika.

Rais wa chama cha Tawifa, Fikira Ntomola amesema taasisi hiyo ilianzishwa mwaka jana kwa lengo la kuinua wanawake kiuchumi kupitia elimu ya fedha, uwekezaji na usimamizi wa biashara.

“Tunahamasisha wanawake kuwekeza kwenye masoko ya mitaji na kuhakikisha wanakuwa na bima ya biashara zao kama kinga dhidi ya majanga,” amesema Ntomola.

Mafunzo hayo yamehusisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya fedha, wakiwemo wawakilishi wa benki waliotoa elimu kuhusu mikopo, marejesho na fursa za kifedha zinazopatikana kwa wanawake wajasiriamali.

Related Posts