Shule mpya ya wavulana kuchukua wanafunzi zaidi ya 300

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa shule mpya ya wavulana  ya kidato cha tano na sita itakapokamilika, itakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi kati ya 300 hadi 350 kwa mwaka.

Shule hiyo itajengwa katika eneo la Kikombo, jijini Dodoma na itahusisha ujenzi wa mabweni, maktaba ya kisasa, bwalo kubwa la chakula, viwanja vya michezo pamoja na nyumba za walimu.

Akizungumza leo Aprili 12, 2025, katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma, wakati wa mbio za hisani za Bunge Marathon 2025, Waziri Mkuu ameeleza kuwa mbio hizo zimeandaliwa kwa lengo la kukusanya Sh3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Bunge ya Wavulana.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongoza matembezi ya mbio za kilomita tano, katika mbio za hisani za Bunge Marathon 2025.

“Ujenzi wa shule hiyo ya bweni unalenga kuunga mkono juhudi za mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini,” amesema Majaliwa.

Majaliwa alibainisha kuwa shule hiyo ya kisasa itakuwa na maabara nne (Biolojia, Kemia, Fizikia na Jiografia), maktaba ya kisasa, bwalo kubwa la chakula, nyumba za walimu, na miundombinu bora ya michezo.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema kuwa ujenzi wa shule hiyo ni mwendelezo wa mafanikio ya Shule ya Bunge ya Wasichana, iliyojengwa mwaka 2020 na wabunge wanawake.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa na Spika wa bunge la Jamhuri ya muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson kwenye picha ya pamoja na washindi wa mbio za kilomita 21, katika mbio za hisani za Bunge Marathon 2025. Picha na Hamis Mniha

Amesema hatua hiyo ni ishara ya usawa wa kijinsia na dhamira ya kuendeleza watoto wote wa Tanzania bila ubaguzi.

“Watoto wote ni wetu, na ndiyo maana tumeona ni muhimu kujenga shule ya wavulana. Nawashukuru washiriki wote kwa kujitokeza na kuchangia azma hii muhimu,” amesema Dk Tulia.

Aidha, ameongeza kuwa mbio hizo zimekuwa pia jukwaa la kujenga afya, mshikamano na uzalendo miongoni mwa Watanzania.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Bunge Marathon 2025, Festo Sanga, amesema mbio za mwaka huu zimevutia washiriki zaidi ya 4,000, ongezeko kubwa ikilinganishwa na washiriki 3,000 mwaka 2024.

“Tumefurahishwa na mwitikio wa mwaka huu. Watu wamehamasika, wamejitokeza kwa wingi, na tukio limevuka matarajio yetu. Tunajivunia mafanikio haya,” amesema Sanga.

Mbio hizo zilihusisha makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo watu wenye ulemavu, wazee wa miaka 60 na kuendelea, pamoja na watoto, jambo lililoleta mshikamano wa aina yake katika kujenga taifa kupitia elimu.

Related Posts