Tajiri Simba kaweka bilioni | Mwanaspoti

SIMBA bado wanaendelea kufurahia kutinga nusu fainali kwa timu hiyo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushindwa kufanya hivyo mara tano katika misimu sita ya nyuma kila ilipotinga robo fainali, lakini bilionea wa klabu hiyo, ameongeza mzuka zaidi kwa wachezaji akiwatengea Sh1 bilioni.

Tajiri wa klabu hiyo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mohammed ‘MO’ Dewji pamoja na bodi hiyo, inaelezwa hataki kusikia kitu kingine zaidi ya kuona taji la Afrika linatua Msimbazi, lakini kama wachezaji wa timu hiyo wanataka fedha imebaki kwao tu kwa sasa.

Ile kauli ya MO Dewji kwamba shabaha yao ni kupata ubingwa wa Afrika inaelezwa tajiri huyo na wenzake wanaoiongoza Simba wanaona kama inakwenda kutimia msimu huu wakiwa tayari wameshafika nusu fainali ikisubiri kupambana na Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Kuvuka hatua hiyo, MO Dewji aliwamwagia mastaa wa timu hiyo ya Simba Sh500 milioni lakini taarifa za ndani zinasema mzigo huo uliongezwa kwa Sh200 milioni na kufikia Sh700 milioni, na hapohapo akawajaza upepo wachezaji kwa kuwaeleza watumie vyema dakika 180 za mechi zijazo watavuna zaidi ya mzigo huo.

Kwenye hesabu hizo, taarifa za ndani kabisa zinasema tajiri huyo ametenga fedha za kufuru kuhakikisha Kombe la Afrika linatua ambapo kama Simba itatinga fainali kuna uwezekano mkubwa wachezaji wa kikosi hicho wakagawana kiasi cha Sh1 bilioni moja kama bonasi.

“Hawa wachezaji kama kweli wanataka fedha huu ndio wakati wao, MO hataki masihara kuanzia hapa tulipofika, alishawaambia hata kwenye fainali kama wanataka fedha basi atatoa Sh1 bilioni anachotaka wamletee tu kombe hapa nchini,” alisema bosi huyo wa juu wa Simba na kuongeza;

“Hapa wamefuzu nusu fainali wamepata kiasi ambacho aliwaahidi, lakini lazima watawekewa fedha nyingi zaidi ya hizi walizopata sasa iwapo watatinga fainali, hivyo kilichobaki ni wao kujituma.”

Endapo MO atafanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wachezaji wa kikosi hicho wakawa wamechota kiasi cha Sh2 bilioni wakitumia mechi sita tu hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika

Hesabu hizo zinatokana na bado wachezaji wa timu hiyo wanasubiri kusikia tajiri huyo ataweka kiasi gani kwenye mchezo wa nusu fainali endapo wataiondoa Stellenbosch.

MO anajua kwamba Stellenbosch ina tajiri jeuri anayejua kumwaga fedha ambapo ameshamwaga fedha za kufuru kwenye hatua ya kuwatupa nje waliokuwa watetezi wa taji hilo la Afrika, Zamalek ya Misri kupitia mechi mbili za robo fainali, tena wakiifunga kwao Misri kwa bao 1-0.

Kwa namna hivyo nyota wa Simba wakiongozwa na Ellie Mpanzu, Kibu Denis, Jean Ahoua, Leonel Ateba na wengine wana kazi za kutumia vyema dk 180 za mechi hizo za nusu fainali ikiwamo ya nyumbani itakayopigwa siku ya Pasaka.

Related Posts