Dodoma. Wanandoa wamefikishwa katika ofisi ya Kata ya Tambukareli, jijini Dodoma, wakikabiliwa na tuhuma za kumjeruhi mtoto wa miaka minne, tukio ambalo limesababisha mtoto huyo kushonwa nyuzi tisa kichwani.
Akizungumza leo Aprili 12, 2025, Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Tambukareli, Zamaradi Kaunje amesema alipata taarifa ya tukio hilo kupitia wafanyakazi wa taasisi za mikopo walikwenda kukusanya marejesho.
“Huyo mtoto alikuwa anaenda kucheza eneo ambalo wamama wanakaa vikao vyao. Mfanyakazi huyo aliona majeraha hayo akaenda kuongea na mtu mwingine kuuliza kama mtaa una viongozi,” amesema.
Amesema mfanyakazi huyo alionyeshwa kiongozi mmoja ambaye alipeleka taarifa kwa viongozi wengine kuhusu changamoto za mtoto huyo.

Zamaradi amesema viongozi hao waliamua kwenda eneo la tukio na kuzungumza na mtoto huyo pamoja na wazazi wake.
“Tukamuuliza mtoto, mama yupo wapi, akatuambia yupo ndani. Kitendo cha mama kutoka nje, mtoto alikimbia na kujificha kwenye bajaji. Tukaanza kuhisi kuna tatizo, tukamwambia mke amuite mume wake, akamuita,”amesema.
Amesema baada ya hapo walimvua nguo mtoto na kumuhoji ni nani aliyemuumiza ambapo aliwaeleza kuwa ni baba yake.
“Baadaye tukamtafuta balozi (wa nyumba kumi kumi) wao ili kupata maelezo zaidi. Tulipomuuliza akasema hiyo sio mara ya kwanza na alishawaonya kiujirani, lakini waliendelea kufanya hivyo,”amesema.
Zamaradi amesema walivyoenda na wazazi hao katika ofisi ya kata, walieleza kuwa mtoto huyo alijigonga katika cherehani na kuwa walimpeleka kupata matibabu katika zahanati iliyopo jirani.
Amesema walipokwenda kufuatilia katika zahanati hiyo, walikiri kumtibia mtoto huyo bila kuwa na PF3.
“Kwa umri wa mtoto huyu ni mdogo sana, hivyo hawa watu walitakiwa kupewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine. Lakini, kwa wanawake wenzangu unapoondoka kwa mwanaume usikubali kuacha mtoto wako hasa akiwa na umri mdogo unaohitaji uangalizi,” amesema.

Zamaradi amesema wazazi hao, wanasema sababu za kumpiga mtoto huyo ni kujisaidia na kula kinyesi chake. Hata hivyo, mtoto huyo anaishi na mama wa kambo baada ya mama yake mzazi kuondoka kwa mumewe na kumuacha.
Diwani wa Kata ya Tambukareli, Juma Mazengo amesema wamekuwa wakijitahidi kuzungumza na jamii ili isiendelee kuwa na tabia ya ukatili.
“Wao wanasema walikuwa wanamuadhibu kwa kuwa ni mtoto waliyekuwa wanamuona ni mtundu, lakini adhabu waliyompa ni kubwa sana na wameacha alama mbalimbali kwenye mwili wake,” amesema.
Mazengo amesema mtoto ana adhabu zake anazotakiwa kupewa na sio kama walizotumia wazazi hao.
Mjumbe wa nyumba kumi, Lucy Gabriel amesema aliletewa mashtaka kuwa kuna mtoto ananyanyasika na walienda kama majirani kumuonya.
“Uamuzi wetu ni kumuweka kwenye uangalizi kwanza kama akiendelea tutampeleka dawati. Huwa anatabia ya kumfungia ndani, hachezi na wenzie, hivyo tumemkanya tumemwambia amtoe nje acheze na wenzie ili achangamke,”amesema.
Alipoulizwa mama wa kambo wa mtoto huyo, Rose Masweli amesema mtoto huyo anatabia ya kula vinyesi na aliyemuadhibu alikuwa ni baba yake.
“Tunakiri kosa hatutarudia tena. Wakati baba anamchapa nilikuwa namwambia amuache asimchape. Mimi ni binadamu, nina mapungufu, naomba mnisamehe sitorudia tena,” amesema.
Hata hivyo, amesema jeraha la kichwani ambalo limemsababisha kushonwa nyuzi tisa lilitokana na kupasuka baada ya kujigonga.
Amesema baada ya kujeruhiwa walimpeleka hospitali ambapo alitibiwa na kushonwa nyuzi tisa.
“Tulikuwa tunampiga kwa kutumia waya wa chaji ya simu na mimi nilikuwa na mfinya. Tukio hili limenifundisha kulea watoto katika maadili yanayotakiwa. Nakiri sitarudia kufanya ukatili wa kijinsia kama hivi, nitalea watoto wangu kwa misingi mizuri na halitajirudia na nitakuwa mfano bora katika jamii,”amesema.

Baba wa mtoto huyo ambaye ni dereva wa bajaji, David Masweli amesema amegundua kitendo alichokifanya sio kizuri.
“Wakati nampiga niliona niko sawa, lakini sasa hivi nimejua kuwa nilitoa adhabu kubwa kwa mtoto. Nawashukuru viongozi kwa kutuita na kutueleza. Nawaahidi kuwa wameniongezea kitu kikubwa katika malezi na namna ya kuishi na watoto na jamii nzima,” amesema.
Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Tambukareli, Mariam Nyirenda amesema athari inayoweza kumpata mtoto anayelelewa kwenye malezi kama hayo ni kutengeneza kizazi kitakachokuwa na ukatili.
“Tunatoa elimu sana ili kupinga ukatili, lakini mtoto anapolelewa kwenye mazingira kama hayo ina maana tunapelekea na yeye akikuwa aje kuwa mkatili. Hii ni kwa sababu amelelewa kwenye mazingira magumu,” amesema.
Amesema athari nyingine ni ya kisaokolojia ambayo akili yake inavurugika na anaweza kuwa na uwoga akipata uonevu wowote mwingine hataweza kujikinga au kutoa taarifa kwa wahusika ili aweze kusaidika.
Mariam amesema athari nyingine ambayo ni ya kimwili ni ya maumivu yanayotokana na majeraha aliyoyapata.
“Kutokana na elimu zinazotolewa shuleni, mtaani na kwenye vikao mbalimbali, matukio ya ukatili yanapungua na yamebaki machache. Tunaendelea kupokea moja moja siyo kama zamani. Watoto wanajielewa, wanajitambua na wana uwezo wa kusemea changamoto zao,”amesema.
Kuhusu tukio hilo, Mariam amesema hatua inayofuata ni kuwapeleka kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika.
Amesema mtoto huyo watampeleka ustawi wa jamii ili waone kwa siku ambazo kesi inaendelea anapata malezi yanayostahili.
“Tunaendelea kutoa wito kwa wazazi, majirani, tuwe ni mabalozi wa kupinga ukatili, tukiona matukio haya tutoe taarifa mapema. Tukiona kuna viashiria vya ukatili pia tutoe taarifa kunapostahiki, tusisubiri mpaka ukatili utokee watoto waumie au wakinamama, wakinababa,”amesema.
Ripoti ya takwimu za uhalifu na usalama barabarani ya mwaka 2023, iliyotolewa na Jeshi la Polisi Tanzania ya kipindi cha Januari hadi Desemba mwaka 2023, waathirika 15,301 wa ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto waliripotiwa ikilinganishwa na waathirika 12,163 katika kipindi hicho mwaka 2022.
Idadi hiyo ni ongezeko la waathirika 3138 sawa na asilimia 25.8.