Dodoma. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeainisha mambo yanayotakiwa na yasiyoruhusiwa kufanywa wakati wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Mambo hayo yako katika Kanuni za Maadili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani zilizosainiwa na vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Serikali na INEC leo Aprili 12, 2025.
Vyama 18 ndivyo vilivyosaini kanuni hizo ambavyo ni AAFP, ACT Wazalendo, ADA-Tadea, ADC, CCK, CCM, Chaumma, CUF, Demokrasia Makini, NLD, NRA, SAU, TLP, UDP, UMD na UPDP.
Chadema kupitia Katibu Mkuu wake, John Mnyika kilishatangaza hakitasaini kanuni hizo.

Kanuni za maadili zimeandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka INEC baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni, uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele amesema kuzingatia masharti ya kifungu cha 162 cha sheria ya uchaguzi Tume iliandaa rasimu ya kanuni hizo na kuziwasilisha kwa vyama vya siasa na Serikali kwa ajili ya kuzipitia na maoni yao yamejumuishwa kwenye kanuni za maadili ya uchaguzi za mwaka 2025.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhani Kailima akizungumza baada ya kusainiwa kwa kanuni hizo amesema zimeanisha maadili ya vyama vya siasa ya kuzingatia wakati uchaguzi na taratibu za utekelezaji wa maadili hayo.

Amesema kwa mujibu wa kifungu namba 162 cha sheria ya uchaguzi kila chama cha siasa, mgombea wa nafasi ya Rais, ubunge na udiwani anapaswa kusaini fomu namba 10 ili kuheshimu maadili hayo.
Amesema mambo muhimu yaliyopo kwenye kanuni ni wajibu wa vyama vya siasa kuheshimu na kufuata Katiba, sheria za uchaguzi, kanuni za uchaguzi na kanuni za maadili ya uchaguzi.

Pia, kuzingatia ratiba za kampeni, kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki, uhuru na amani na kuepuka vitendo vya kuvuruga uchaguzi vya aina yoyote.
“Mambo yanayotakiwa ni kuepusha kufanya fujo, lugha za matusi, kejeli na udhalilishaji, vitendo vinavyoashiria unyanyasaji wa kijinsia, kuepuka kufanya kampeni kwenye majengo ya ibada, kutoa rushwa na mengine yaliyopo kwenye kanuni,” amesema.
Amesema wajibu wa Serikali kwenye kanuni hizo ni kutoa fursa sawa kwa wadau wa uchaguzi ili kuendesha shughuli za kisiasa kwa uhuru na kuzingatia sheria za nchi.

Pia, kuhakikisha kunakuwapo hali ya usalama, amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi, kutoa fursa sawa kwa vyama vya siasa vyenye wagombea wa nafasi ya urais na makamu wake kutumia vyombo vya habari vya umma kutangaza sera zao.
Kailima amesema wajibu mwingine ni kuhakikisha viongozi na watendaji wanazingatia ipasavyo ukomo wa mamlaka na madaraka yao katika shughuli za uchaguzi.

Yasiyotakiwa kufanywa na Serikali ni kuingilia na kuzuia isivyo halali mikutano iliyoitishwa na vyama vya siasa na wagombea kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi, vyombo vya ulinzi na usalama visitumie madaraka yao kukandamiza wagombea, wafuasi au chama cha siasa, mtumishi yeyote wa serikali anayehusika hahamishwi kutoka eneo la uchaguzi hadi utakapokamilika.
Tume inatakiwa na kanuni kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria za uchaguzi na za nchi katika usimamizi wa uchaguzi, kusimamia na kuendesha uchaguzi katika misingi inayowezesha uchaguzi kuwa huru na wa haki.

INEC inatakiwa kuvipatia vyama vya siasa ratiba na taarifa za uchaguzi kwa wakati na kutoa elimu ya mpigakura nchi nzima.
Pia, kuvipatia vyama vya siasa kanuni, maelekezo, nakala za daftari la kudumu la wapigakura na nyaraka nyingine zinazohusu masuala ya uchaguzi kwa wakati.
“Kukemea vitendo vyenye nia ya kuharibu uchaguzi vinavyoweza kufanywa na viongozi wa vyama vya siasa, wagombea na wafuasi,” amesema za kuongeza:
“Mambo ambayo Tume haitakiwi kufanya ni kupendelea chama chochote cha siasa au mgombea yeyote, kubadilisha ratiba za kampeni za uchaguzi bila kushirikisha vyama vya siasa vyenye wagombea.”

Pia, haipaswi kuchelewa au kutokupeleka vifaa pungufu katika vituo vya kupigia kura bila sababu za msingi.
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Addo Shaibu licha ya kusaini kanuni hizo, amehoji ni kwa nini chama kisichosaini kanuni za maadili hakitashiriki uchaguzi mkuu.
Pia, alitaka ufafanuzi kuhusu wapigakura kuondoka eneo la kupigia kura, akitaka wakae angalau mita 100 hasa wakati wa kuandika matokeo. Pia mawakala wawe na simu kwenye vituo vya kupigia kura ili kurahisisha mawasiliano.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Kailima amesema maswali hayo yatajibiwa kwa maandishi.
Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, amesema vyama vya siasa vimeshiriki vya kutosha katika mchakato wa kutoa maoni.
“Hili ni suala muhimu la kitaifa kwa vyama vya siasa. Nimeridhia na ninaomba mchakato uendelee kwa sababu jambo limeeleweka,” Doyo.

Katibu Mkuu wa NCCR Mageuzi, Evaline Munisi amesema kanuni zimetengeneza utaratibu wa kisheria wakati wa kampeni na uchaguzi ambao chama na kila mgombea wanapaswa kuzingatia.
“Uchaguzi una mambo mazuri na mabaya, hivyo ukienda vibaya kanuni zitatumika kupitia kamati za maadili kuanzia ngazi za kata hadi Taifa,” amesema.

Katibu Mkuu wa CUF, Husna Abdallah amesema chama hicho kimeridhia kanuni kwa sababu kimeshirikishwa katika hatua zote na kwamba, zimeweka ulinzi kwa wagombea.