ALLIANCE Girls ya mkoani Mwanza imesema haitaki mambo mengi Ligi Kuu ya Wanawake na inachokitaka ni kubaki tu msimu ujao.
Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza nafasi ya nane kwa tofauti ya idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ikilingana pointi na Baobab Queens iliyoshuka daraja sambamba na Geita Gold Queens.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha wa timu hiyo, Sultan Juma alisema malengo ya timu tangu anakabidhiwa dirisha dogo ni kusalia ligi kuu.
Aliongeza haijalishi timu hiyo itamaliza nafasi ya ngapi kikubwa malengo ya timu ya kubaki ligi kuu isalie.
“Wakati nafika niliambiwa timu haiko nafasi nzuri, ya tisa, mipango ilikuwa hivyo na kwa asilimia 90 imefanikiwa na ligi ikiisha nadhani naweza kuondoka kwa sababu mkataba wangu unamalizika, nilisaini wa muda mfupi kama kuwashikia tu,” alisema Sultan na kuongeza.
“Nilitoa wiki mbili za mapumziko na Jumatatu tunarudi kambini kwa maandalizi mapya, tumepanga kucheza mechi za kirafiki kwa sababu ligi itarejea mwishoni.”
Alliance iko nafasi ya sita na pointi 15 kwenye mechi 14 ilizocheza ushindi mechi nne, sare tatu na kupoteza mechi saba.